Mahakama Kuu ya Mzuzu nchini
Malawi jana tarehe 12 Aprili 2017 iliwaachia huru Watanzania wanane
waliokuwa wanashikiliwa nchini humo kwa kosa la kuingia kinyume cha
sheria kwenye mgodi wa urani wa Kayerekera.
Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya
Mzuzu, Bw. Texious Masoamphambe alitoa hukumu
ya kifungo cha mwezi mmoja
kwa kosa la kuingia kinyume cha sheria kwenye mgodi wa urani wa
Kayerekera (trespass) na kifungo cha miezi mitatu kwa kosa la kufanya
ujasusi (reconnaissance).
Makosa hayo mawili, kifungo chake
kinakwenda pamoja na kwa mujibu wa Hakimu huyo watuhumiwa tayari
wameshatumikia kifungo hicho na kuamuru waachiliwe huru. Aidha, Hakimu
aliamuru Wizara ya Mambo ya Ndani na Usalama wa Ndani kuhakikisha kuwa
Watanzania hao wanasafirishwa na kurejeshwa makwao haraka iwezekanavyo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka
Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi, Watanzania hao wamesafirishwa leo
tarehe 13 Aprili 2017, kutoka Mzuzu hadi Mpaka wa Songwe/Kasumulu kati
ya Tanzania na Malawi.
Watanzania hao ambao ni Walasa
Mwasangu, 30, Binto Materinus, 32, Ashura Yasiri, 63, Christian Msoli,
38, Layinali Kumba, 47, Maliyu Mkobe, Gilbert Mahumdi, 32, na Martin
Jodomusole, 25 walikuwa wamekamatwa na kushikiliwa na vyombo vya usalama
vya Malawi tokea tarehe 20 Desemba 2016.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 13 Aprili 2017.
No comments :
Post a Comment