Na Nuru Juma na Husna Saidi – MAELEZO
Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin William Mkapa amewataka
viongozi wa nchi kuzingatia maadili na miiko ya uongozi ikiwa ni njia ya
kumuenzi Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
Rai hiyo imetolewa leo wakati wa
Kongamano la Maadhimisho ya Kumbukizi ya Mwl Nyerere lililofanyika
katika ukumbi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwl. Nyerere Jijini Dar es
Salaam.
Mkapa alisema kuwa katika kumuenzi
Mwl. Nyerere ni vyema viongozi wakamuenzi kwa kufuata maadili na miiko
ya uongozi jambo litakalo pelekea kuwa viongozi bora katika jamii.
“Urithi wa Mwl. Nyerere katika
uongozi ni kufuata yale aliyokuwa akiyafanya na katika uongozi wake
aliweza kutekeleza na kuzingatia maadili na miiko ya uongozi kwa
kuwaongoza wananchi kwa usawa na haki, hivyo katika kumuenzi hatuna
budi kufuata yale aliyoyafanya, ” alisema Mkapa.
Aidha Mkapa alitoa pongezi kwa
uongozi wa chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kwa kuweza kukiinua
tena chuo hicho kwani kipindi cha kati chuo kililega na kupoteza
mwelekeo.
Pia aliwataka Watanzania kuacha
kubuni mambo wasiyoyajua na badala yake wapende sana kusoma na kuelewa
historia ya nchi na Serikali kwa ujumla ikiwa ni njia mojawapo ya
kumuenzi baba wa Taifa.
“Napenda kuwasihi Watanzania
wapende sana kusoma ili kuweza kutanua upeo wao wa kufikiri kwani Baba
wa Taifa alipenda sana kusoma makala za ndani ya nchi, vitabu na makala
za nje ya nchi ili kuweza kupanua upeo wake kwa ajili ya kutatua
matatizo ya hapa na matatizo ya Kimataifa” aliongeza Mkapa.
Kwa upande wake Waziri Mkuu
Mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba alisema kuwa sifa za uongozi bora ni
pamoja kuthamini utu, uzalendo, uchapakazi na aliye na hofu ya Mungu.
“Sifa ya kiongozi bora ni lazima
awe mtu anayethamini utu wa mtu na anayeamini binadamu wote ni sawa, awe
mzalendo, muadilifu, mchapa kazi na ana hofu ya mungu,anashirikiana na
kuwashirikisha viongozi wenzake.” Alisema Jaji Warioba.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama
cha Mapinduzi (CCM) Bara, Phillip Mangula alisema kuwa cheo ni dhamana
unayopewa na wananchi hivyo kiongozi bora ni yule atakaye ongoza kwa
usawa.
”Cheo ni dhamana unayopewa na
wananchi ili uweze kuongoza kwa usawa kwani kiongozi bora atawaongoza
watu kwa usawa,” alisema Mangula.
Mangula alisema kuwa katika
kipindi cha uongozi wa Mwalimu Nyerere alikuwa ni kiongozi anayejali
sana wananchi wake akiamini kuwa binadamu wote ni sawa jambo ambalo
analiona linajirudia katika Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Dkt.
John Pombe Magufuli ambaye naye amejipambanua kwa kuwajali wanyonge.
Kongamano hili lililohudhuriwa na
viongozi mbalimbali wastaafu wakiongozwa na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa,
Salim Ahmed Salim,Spika Mstaafu Anne Makinda, Jaji Warioba, Jaji
Agustino Ramadhan, na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa nchini.Kauli
mbiu ya Kongamano hilo ilikuwa ni “Urithi wa Mwalimu Nyerere Katika Uongozi, Maadili ya Uwajibikaji Kwenye Ujenzi wa Taifa.”
No comments :
Post a Comment