Friday, April 21, 2017

KUANZISHWA KWA PROGRAMU YA ELIMU YA MUUNGANO KWA UMMA.

Coat_of_arms_of_Tanzania.svg
Jovina  Bujulu-MAELEZO
Mnamo Aprili 26, 1964, nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya  watu wa Zanzibar  ziliungana na kuzaa taifa jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambalo mwaka huu linatimiza miaka 53.
Juhudi za kuunganisha nchi hizo mbili zilitokana na makubaliano ya waasisi wa taifa ambao ni
Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Mzee Abeid Amani Karume. Lengo la kuunganisha nchi hizo mbili lilikuwa ni kuwa na taifa moja lenye nguvu kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Muungano huu umedumu kama taifa moja lenye amani, umoja, utulivu na mshikamano kwa miaka 53, jambo ambalo baadhi ya nchi nyingine duniani limewashinda. Mfano wa Nchi hizo ni Senegal na Gambia na Misri na Syria. Hivyo Muungano wetu ni wa pekee na mfano wa kuigwa katika bara la Afrika na duniani pote.
Ili kuhakikisha kuwa historia  na masuala yote yanayohusu Muungano  yanahifadhiwa  na kufahamika kwa wananchi wa pande zote za Muungano, Idara ya Muungano iliyo  chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais ilianzisha  “Programu  ya kutoa elimu kwa umma kuhusu Muungano” ambayo ilianzishwa mwaka 2014.
Akiongea katika mahojiano maalum kuhusu Muungano, Mkurugenzi wa Muungano kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, ndugu Baraka Rajab Baraka, anasema kuwa madhumuni ya kuanzisha programu hiyo ni kuhakikisha kuwa historia ya tulikotoka, tulipo na tuendako, umuhimu na faida ya Muungano inajulikana kwa Watanzania walio wengi, na  pia elimu ya uraia na uzalendo inatolewa kwa wanafunzi wa sekondari na vyuo nchini ili  kuwajengea uelewa mpana kuhusu Muungano wa huo.
“Miongoni mwa majukumu ya Idara ya Muungano ni pamoja na kuhakikisha kuwa umma  unakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu Muungano pamoja  na kuondoa kabisa taswira  mbaya kuhusu Muungano na kuwasaidia wanafunzi kuwa na uzalendo na kuwa raia wema kwa nchi yao  na  kutambua kuwa amani iliyopo nchini ni moja ya manufaa ya Muungano”,  alisema ndugu Baraka.
Aliongeza kuwa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020 imeweka msisitizo zaidi wa kutoa elimu ya uraia na uzalendo kwa makundi ya vijana ikiwemo wanafunzi wa sekondari na vyuo pamoja na makundi mbalimbali katika jamii.
Mwaka 2014 program hiyo ilifanikiwa kutoa elimu ya Muungano kwa wajumbe wa kamati za kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za Uchumi na Fedha pamoja na Katiba na Sheria.
Aidha, elimu hiyo ilitolewa kwa baadhi ya wanafunzi wa Vyuo vya elimu ya juu kutoka Zanzibar na mikoa ya Dodoma, ambapo vyuo vikuu vilivyoshiriki ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini, Chuo cha Mtakatifu John, Chuo cha Madini, Chuo cha Elimu ya Biashara ,  Chuo cha Ustawi wa Jamii na Chuo cha Serikali za Mitaa cha Hombolo.
Katika  mkoa wa  Mbeya wanafunzi kutoka vyuo vikuu vya Mzumbe, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Chuo Kikuu cha Teophil Kisanji, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia, Taasisi ya Uhasibu na Chuo cha Elimu ya Biashara pamoja na vyuo vikuu vya mkoani Iringa  walishiriki kupata elimu ya Muungano kwa njia ya makongamano.
Pamoja na elimu hii kutolewa kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu, pia wanafunzi wa  shule za msingi wa mkoa wa Dar es salaam  zaidi ya  300 walipatiwa elimu hiyo  kwa njia ya maigizo, nyimbo, ngonjera na mashairi.
Vyombo vya habari pia vilitoa elimu ya Muungano kupitia katika vipindi mbalimbali, ambapo mwaka 2015 redio Uhuru, TBC, Upendo na Televisheni za Azam, ITV na wadau mbalimbali waliongelea masuala ya Muungano na hivyo kuwapa ufahamu zaidi wananchi.
Ndugu Baraka anasema kuwa katika kutoa elimu hiyo, Idara yake huandaa makongamano ambapo mada mbalimbali huwasilishwa kwa kina. Mada hizo huwa zinahusu  uchumi, siasa, masuala ya  kijamii yanayohusu pande zote mbili na umuhimu wa watu kuishi pamoja na kushirikiana.
Akizungumzia mwitikio wa elimu hiyo kwa walengwa, ndugu Baraka alisema kuwa ni mzuri sana na wamegundua kuwa watu wengi hawafahamu masuala muhimu ya Muungano, hasa faida zake.
Naye mwanafunzi Nadhifa Hassan kutoka  Zanzibar  alisema kuwa elimu ya Muungano ni nzuri na wameipokea kwa mikono miwili kwani wamekuwa wakielezwa taswira  mbaya  kuhusu  Muungano kuwa ni mbaya na unawaonea wananchi wa Zanzibar.
“Tumekuwa tukielezwa  mtazamo tofauti kuhusu Muungano kuwa unawanufaisha watu wa Tanzania Bara na kwa upande wa Zanzibar hauna faida yoyote  bali unawakandamiza” alisema Nadhifa.
Kuhusu maadhimisho ya mwaka huu, ndugu Baraka alisema Idara yake imejipanga kutoa elimu hiyo kwa wanafunzi wa shule za msingi kutoka mkoani Dar es Salaam.
“Lengo ni kuwafanya wanafunzi hao waone kuwa nchi yetu ni moja na kuwa na mawazo chanya kuhusu Muungano.” anasema ndugu Baraka.
Akizungumzia faida za Muungano anasema unawaunganisha wananchi wa pande zote mbili, kushirikiana katika nyanja mbalimbali kiuchumi, kijamii na kisiasa na kuwa na taifa moja lenye nguvu kiuchumi na kijamii na kiulinzi.
Baadhi ya wananchi waliokwishahudhuria midahalo na kupata elimu juu ya Muungano walitoa maoni yao kuwa ni vizuri baadhi ya viongozi wa siasa wakawa na dhamira ya kweli ya kuuimarisha Muungano  ili mwenendo wa Muungano usiwe na mwelekeo wa kuuvunja na waliwataka   wahusuka kupeleka   elimu hii vijijini ili umuhimu wake ufahamike kwa watu wote.

No comments :

Post a Comment