Serikali Wilayani Serengeti Mkoa
wa Mara yalenga kuimarisha mahusiano yenye tija na hoteli za kitalii
zilizopo ndani na nje ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Hayo yamebainika katika ziara
iliyofanywa na Kamati ya fedha, uongozi na mipango inayoongozwa na
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Mhe. Juma Porini Keya
ilipofanya ziara kuzitembelea hoteli za kitalii katika hifadhi ya
Serengeti.
Katika ziara hiyo
iliyogawanayishwa katika makundi 4, jumla ya hoteli 15
za kitalii na ofisi za Shirika la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti
(SENAPA) zilitembelewa.
“Kwa
muda mrefu sasa hoteli nyingi za kitalii katika hifadhi ya taifa ya
Serengeti zimekuwa hazilipi tozo stahiki hivyo kupunguza vyanzo vya
mapato vya Halmashauri; tukiboresha mahusiano, tutaweza kukusanya vizuri
mapato ya serikali” alisema Mhe Porini alipokuwa anazungumza na afisa
utalii wa hifadhi ya Taifa ya Serengeti Bw. Aldo Mgude.
Katika
kuweka mikakati ya kudhibiti ukwepaji wa kulipa ushuru, kamati
imeliomba Shirika kuandaa kikao na kuwakutanisha kwa pamoja na wamiliki
wa hoteli za kitalii ili kuboresha mahusiano na kuweka misingi imara ya
usimamiaji wa mapato.
Aidha
kamati imebaini kiwango kidogo cha upatikanaji wa ajira kwa wakazi wa
Serengeti na kuziomba hoteli na kambi za kitalii ndani na nje ya hifadhi
ya Serengeti kutoa ajira kwa wakazi wa Serengeti.
Kamati
imezipongeza hoteli za kitalii kwa jitihada kubwa wanazofanya kutangaza
utalii katika hifadhi ya Serengeti na kuzisaidia jamii zinazoizunguka
hifadhi ya Serengeti kwa kutoa misaada ya kielimu pamoja na ujenzi wa
miundombinu.
Imetolewa na
ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji
Kitengo cha TEHAMA & UHUSIANO
Kwa habari zaidi tembelea www.serengetidc.go.tz
ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji
Kitengo cha TEHAMA & UHUSIANO
Kwa habari zaidi tembelea www.serengetidc.go.tz
No comments :
Post a Comment