Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima
ya Afya (NHIF) Mkoa wa Dodoma, Salome Manyama akipokea cheti cha
ushiriki wa Maonesho ya Mifuko ya Uwezashaji kutoka kwa Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu
Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Antony
Mavunde akimsikiliza Meneja wa NHIF, Mkoa wa Dodoma Salome Manyama
alipotembelea banda la Mfuko katika Maonesho ya Mifuko ya Uwezeshaji.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu
Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Antony
Mavunde akisaini kitabu cha wageni katika banda la NHIF.
Ofisa wa NHIF, Enock Humba akitoa elimu kwa wananchi waliofika bandani hapo.
Maofisa wa NHIF, Grace Michael na
Enock Humba wakihudumia wananchi waliofika bandani hapo kupata
ufafanuzi wa mambo mbalimbali yanayohusu huduma za Mfuko.
……………………………………………………………………
Na Grace Michael,Dodoma
Wananchi wa Mkoa wa Dodoma
wamepongeza mpango unaotekelezwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
(NHIF) unaojulikana kama Toto Afya Kadi kwa kuwa ni msaada mkubwa kwa...
watoto chini ya umri wa miaka 18.
Mbali na mpango huo, wamesema
kuwa hatua kubwa ya uboreshaji wa huduma za matibabu uliofikiwa na Mfuko
huo kwa sasa unatoa hamasa kwa Watanzania kujiunga na huduma zake na
kunufaika nazo.
Hayo wameyasema kwa nyakati
tofauti mjini hapa wakati wa maonesho ya Mifuko ya Uwezeshaji ambayo
yalizinduliwa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa ambayo
yatahitimishwa Aprili 22, mwaka huu.
“Kwa kweli NHIF kwa sasa
tunawapongeza sana hasa kwa kuwa na madirisha mengi ambayo yanamwezesha
kila mwananchi kujiunga na kutumia huduma za Mfuko huu…awali Mfuko
ulihudumia watumishi wa Umma tu lakini kwa sasa tunashukuru na
tunawapongeza kwa hili,” alisema Bw. Sebastian Kingu.
Akizungumzia huduma za matibabu
mmoja wa wanachama waliotembelea banda la Mfuko, Bi. Prisca Peter
alisema kuwa Mfuko umekuwa mkombozi mkubwa wa afya za wananchi wengi na
imesaidia kwa kiasi kikubwa hasa wanachama wake wanapopatwa na maradhi
yanayohitaji fedha nyingi.
“Mimi binafsi niushukuru sana
Mfuko huu maana mpaka sasa katika familia yangu tumepata huduma ya
upasuaji tena mkubwa ambao bila Mfuko ingeleta shida kubwa ndani ya
familia lakini kwa kuwa tunahudumiwa na Mfuko tulipata matibabu vizuri
kabisa bila kutoa hata shilingi moja,” alisema Bi. Prisca.
Alipotembelea banda hilo, Naibu
Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na
Watu wenye Ulemavu, Antony Mavunde alisema kuwa lengo la Serikali ni
kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa na utaratibu huu wa kupata huduma
kupitia Bima za Afya hivyo akautaka Mfuko kuongeza kasi ya utoaji elimu
na uhamasishaji kwa wananchi.
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
umekuwa ukishiriki shughuli mbalimbali zinazofanyika kwa wananchi kwa
lengo la kuwafikia Watanzania wengi na kutoa huduma bora ya matibabu.
Katika maonesho hayo, Mfuko
unatoa elimu na kuhamasisha wananchi kujiunga na Mfuko kupitia makundi
yaliyowekwa ili wanufaike na huduma za matibabu.
Akizungumzia hilo, Meneja wa
NHIF, Mkoa wa Dodoma Bi. Salome Manyama alisema kuwa Mfuko umejipanga
kuhakikisha unatoa huduma nzuri na bora zaidi kwa wanachama wake lakini
pia kuhakikisha unahamasisha wananchi kujiunga ili wanufaike na huduma
zinazotolewa.
No comments :
Post a Comment