Husna Saidi na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Kampuni
ya Harusi Trade Fair imejipanga kukutanisha wafanyabiashara na watoa
huduma wa bidhaa za harusi ili waweze kufahamiana na kuonesha bidhaa
zao.
Meneja
Biashara wa Kampuni hiyo, Hamis Omary ameyabainisha hayo leo Jijini Dar
es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maonesho
ya Harusi Trade Fair yanayotarajia kufanyika Mei 12 hadi 13 mwaka huu
katika ukumbi wa Golden Tulip.
Omary alisema maonesho hayo ya tisa ya bidhaa na huduma za harusi ni moja ya maonesho makubwa ambayo hufanyika mara moja au mbili kila mwaka na yanashirikisha wadau mbalimbali kutoka nchi za Afrika Mashariki na Pwani.
“Tunapenda
kuwatangazia wananchi kujumuika na sisi katika maonesho haya kwani ni
ya kipekee, yanavutia, yanaburudisha pamoja na kurahisisha maharusi
kuandaa harusi zao.Vile vile kutakuwa na mitindo mipya kutoka kwa
wauzaji bora katika sekta ya harusi” alisema Omary.
Meneja huyo aliongeza kuwa kadri maonesho hayo yanavyoendelea kukua mwaka hadi mwaka yanazidi kuwa maonesho bora kwani wanajifunza njia mbalimbali za kutatua changamoto zinazojitokeza katika maonesho hayo.
Kwa
upande wake Mratibu wa maonesho hayo, Naomi Godwin alisema kuwa lengo
la maonesho hayo ni kuwapa maharusi mahitaji yao muhimu hivyo ni vizuri
kuona na kutumia bidhaa na huduma hizo ili kupendezesha sherehe zao.
”Maonesho
haya yatafanyika bure hivyo huu utakua muda mzuri kwa maharusi pamoja
na familia zao kukutana na wabunifu mbalimbali watakaowabunia sherehe
zinazoendana na wakati”alisema Naomi.
Nae
Meneja Msaidizi kutoka Golden Tulip Hotel, Adele Johnson amesema kuwa
wameamua kudhamini maonesho hayo ili kuwavutia wananchi wengi kufika
katika eneo hilo.
Maonesho
hayo yanatarajiwa kuhudhuriwa na wafanyabiashara zaidi ya 30
wanaohusika na huduma za harusi wakiwemo wapiga picha, huduma za
vyakula,wapambaji ukumbi,huduma za nywele, wapamba nyuso, pamoja na
wamiliki wa kumbi za sherehe.
No comments :
Post a Comment