Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Amali Zanzibar Riziki Pembe Juma akifungua Kongamano la maazimisho ya
siku ya Kifua kikuu Duniani katika ukumbi wa sanaa Rahaleo (kulia)
mwakilishi wa WHO Zanzibar Dkt. Ghirman na (kushoto) Mkurugenzi Mkuu wa
Wizara ya Afya Dkt. Jamala Taib.
Baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu
walioshiriki Kongamano la maazimisho ya siku ya Kifua kikuu Duniani
katika Ukumbi wa sanaa Rahaleo wakimsikiliza Waziri wa Elimu na Mafunzo
ya Amali alipokuwa akifungua Kongamano hilo.
Mratibu kitengo cha ufuatiliaji
na tathmini mwenendo wa maradhi ya Ukimwi, Kifua Kikuu na Ukoma Zanzibar
Asha Ussi Khamis akitoa mada yake ya matokeo ya utafiti juu ya uelewa,
tabia na matendo juu ya kifua kikuu Zanzibar katika ukumbi wa sanaa
Rahaleo Mjini Zanzibar.
Mmoja wawashiriki wa kongamano la
kuazimisha siku ya Kifua kikuu Duniani kutoka Skuli ya Afya na Sayansi
ya Tiba (SUZA) Mariam Ali Mansour akichangia moja ya mada
zilizowasilishwa.
Picha na Makame Mshenga-Maelezo.
……………..
Na Ramadhani Ali/Maelezo Zanzibar
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Amali Riziki Pembe Juma amewataka vijana wasomi kujikita
katika kufanya
tafiti mbali mbali ili kupata majibu sahihi ya matatizo yanyoikabili
nchi ikiwemo maradhi.
Amesema yapo matatizo mengi
yanayoikabili jamii ya Zanzibar na yanahitaji majibu ya kisayansi ili
kusaidia kupiga hatua katika kufikia maendeleo.
Waziri Riziki alieleza hayo
alipokuwa akifungua kongamano la maadhimisho ya siku ya Kifua Kikuu
Duniani lililowashirikisha wanafunzi wa Vyuo vikuu Zanzibar katika
Ukumbi wa Wasanii Rahaleo
Alisema maradhi ya kifua kikuu ni
miongoni mwa maradhi hatari duniani na kwa mujibu wa takwimu za Shirika
la Afya (WHO) mwaka 2015 watu milioni 10.4 waliugua ambapo milioni 1.8
walifariki.
Aliitaja Tanzania kuwa ni miongoni
mwa nchi 30 Duniani zinazoongoza kwa maradhi ya kifua kikuu hivyo
juhudi zaidi zinahitajika katika kukabiliana na maradhi hayo.
Waziri Riziki ambae pia ni Kaimu
Waziri wa Afya alisema hali sio nzuri pia kwa Zanzibar na watu 700 hadi
800 wanaugua kifua kikuu kila mwaka na baadhi yao hupoteza maisha.
Alizitaja dalili za maradhi ya
Kifua kikuu kuwa ni kukohoa kwa kipindi kirefu, kutoa makohozi yenye
damu, homa za mara kwa mara hasa wakati wa jioni, kutokwa na jasho jingi
wakati wa usiku, kukosa hamu ya kula na hatimae kupungua uzito.
Aliwashauri wananchi wasisite
kufika katika vituo vya afya wanapoona dalili hizo ili kupata matibabu
katika hatua za awali kwani maradhi hayo yanatibika kwa urahisi na dawa
zake zinapatikana bila malipo.
Alisema miongoni mwa sababu
zinazopelekea kupata maradhi hayo ni msongamano wa watu hasa sehemu za
mijini ujenzi holela wa nyumba za kuishi kwa vile maradhi hayo
yanaambukizwa kwa njia ya hewa.
Akitoa salamu za Shirika la Afya
Duniani (WHO), Mwakilishi wa Shirika hilo Zanzibar Dkt. Ghirman
Andermichael alisema kifua kikuu ni janga la Dunia hivyo kila mmoja
anawajibu wa kushiriki katika kuhakikisha maradhi hayo yanapungua kwa
asilimia 30 ifikapo mwaka 2025.
Baadhi ya wanafunzi walioshiriki
Kongamano hilo waliishauri Wizara ya Afya kuandaa wataalamu na vifaa vya
kutosha vya kuchunguza maradhi hayo katika Hospitali na vituo vikubwa
vya Afya.
Dunia huadhimisha siku ya Kifua
kikuu kila ifikapo Machi 24 na kaulimbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu
ni Kifua kikuu ni janga la Taifa. Tuungane kutokomeza Kifua
kikuu.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
No comments :
Post a Comment