Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaasa waandishi wa habari nchini
kuandika habari zinazohamasisha maendeleo ya nchi badala ya kuandika
habari ambazo hazina manufaa kwa taifa.
Akizungumza wakati ya hafla ya
kuwaapisha mawaziri, mabalozi pamoja na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu
jijini Dar es Salaam leo, Rais Magufuli alisema kuwa waandishi wa habari
wanatakiwa kuwa wazalendo kwa kuandika habari za kuhamasisha wananchi
kushiriki katika
shughuli za maendeleo pamoja na kuunga mkono jitihada
mbalimbali za Serikali.
“Nchi yetu ina sifa nzuri nje,
Rais wa Benki ya Dunia alipotembelea katika nchi yetu hivi karibuni
alitupatia jumla ya shilingi trilioni 1.74 na benki hiyo ipo mbioni
kutupatia fedha nyingine shilingi trilioni 2.8, lakini vyombo vyetu vya
habari haviandiki kwa mapani juu ya taarifa ” alisema Rais Magufuli.
Alibainisha kuwa fedha hizo
zitatumika katika miradi ya Ujenzi wa barabara za juu eneo la Ubungo,
maboresho ya miji, pamoja na Vyuo Vikuu vya Sokoine na Mandela na
kuleta maendeleo ya nchi yetu lakini taarifa zake hazikupewa uzito
unaostahiki katika vyombo vya habari.
Rais Magufuli aliwataka wamiliki
wa vyombo vya habari pamoja na waandishi wa habari kufuata uweledi wa
taaluma ya habari pamoja na kuweka mbele maslahi ya taifa badala ya
maslahi ya mtu mmoja mmoja.
Aidha, Rais Magufuli amewapongeza
viongozi aliowaapisha na kuwataka kufanyakazi kwa bidii na juhudi ili
kutimiza azma ya serikali ya kuwa nchi ya uchumi wa kati kwa kutekeleza
agenda ya viwanda.
Viongozi walioapishwa ni Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe, Waziri wa
Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais,
Alfayo Kidata.
Wengine ni Balozi wa Tanzania
nchini Ujerumani Dkt. Abdallah Possi, Balozi wa Tanzania nchini Israel
Job Masima, Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Sylvester Mabumba pamoja
na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Stellah Mugasha.
No comments :
Post a Comment