Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Waziri Mkuu wa Shirikisho la
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ethiopia, Mheshimiwa Hailemariam Dessalegn
anatarajiwa kuwasili nchini kesho, Machi 31 kwa ziara ya kitaifa ya
siku mbili kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Akizungumza na waandishi wa
habari leo jijini Dar es salaam, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiao wa Afrika Mashariki, Dkt. Suzan Kolimba alisema kuwa ziara
ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Mhe. Dessalegn imetokana na mkutano kati yake
na Mhe. Dkt. Magufuli uliofanyika baada ya mkutano wa kawaida wa 28 wa
Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika hivi karibuni
huko nchini Ethiopia.
Aliongeza kuwa madhumuni ya ziara
hiyo ni pamoja na kukuza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Tanzania na
Ethiopia pamoja na kujadili fursa zaidi za ushirikiano katika maeneo
mbalimbali ikiwemo uwekezaji na biashara.
“Mahusiano ya Tanzania na
Ethiopia ni mazuri, Ethiopia imeonesha nia ya kufungua Ubalozi wake hapa
nchini hivi karibuni. Kwa sasa Ethiopia inawakilishwa nchini na Balozi
wake aliyepo Nairobi nchini Kenya” alisema Naibu Waziri Kolimba.
Wakati wa ziara hiyo, Mhe.
Dessalegn atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.
John Pombe Joseph Magufuli kwa mazungumzo, watashuhudia uwekwaji saini
wa mikataba ya ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali kabla ya kuzungumza
na Waandishi wa Habari.
Aprili 01 mwaka huu, Waziri mkuu
huyo wa Ethiopia atatembelea Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na
kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa Bandarini hapo. Mhe. Dessalegn
na ujumbe wake wataondoka siku hiyohiyo kurejea Ethiopia.
Mwaka 2015 Waziri Mkuu wa Ethipia
Mhe. Dessalegn alitembelea Tanzania na kushiriki uzinduzi wa Kiwanda
cha kutengeneza dawa za kuua viluwiluwi vya mbu wanaoeneza Malaria
kilichojengwa Kibaha, Pwani kwa ufadhili wa Serikali ya Cuba.
No comments :
Post a Comment