Mkutano na waandishi wa habari ukiendelea.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Taarifa kuhusu ziara ya Waziri Mkuu wa Ethiopia nchini
Waziri Mkuu wa Shirikisho la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ethiopia, Mheshimiwa Hailemariam Dessalegn
anatarajiwa kufanya ziara ya kitaifa ya siku mbili nchini tarehe 31
Machi hadi tarehe 1 Aprili 2017 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Ziara
ya Mhe. Dessalegn inakuja kufuatia mkutano kati yake na Mhe. Dkt.
Magufuli uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Kawaida wa 28 wa Wakuu wa
Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia
mapema mwaka huu.
Mhe.
Dessalegn anatarajiwa kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere tarehe 31 Machi, 2017 asubuhi na atapokelewa na Mhe. Rais
Magufuli.
Madhumuni
ya ziara hiyo ni kukuza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Tanzania na
Ethiopia pamoja na kujadili fursa zaidi za ushirikiano katika maeneo
mbalimbali ikiwemo uwekezaji na biashara.
Wakati
wa ziara hiyo, Mhe. Dessalegn atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mazungumzo ya
faragha yatakayofuatiwa na mazungumzo rasmi yatakayowahusisha wajumbe wa
pande mbili. Aidha, Viongozi hao watashuhudia uwekwaji saini wa
mikataba ya ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali kabla ya kuzungumza na
Waandishi wa Habari.
Jioni
ya siku hiyo, Mhe. Dessalegn na ujumbe wake watashiriki Dhifa ya
Kitaifa ya Chakula cha jioni kilichoandaliwa Ikulu kwa heshima yake na
Mhe. Rais Magufuli.
Tarehe
01 Aprili, 2017 Mhe. Dessalegn ataendelea na ziara yake kwa kutembelea
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na kujionea shughuli mbalimbali
Bandarini hapo. Mhe. Dessalegn na ujumbe wake wataondoka siku hiyohiyo
kurejea Ethiopia.
Mahusiano ya Tanzania na Ethiopia
Mahusiano
ya Tanzania na Ethiopia ni mazuri. Ethiopia imeonesha nia ya kufungua
Ubalozi wake hapa nchini hivi karibuni. Kwa sasa Ethiopia inawakilishwa
nchini na Balozi wake aliyepo Nairobi, Kenya.
Aidha,
kumekuwa na ziara za viongozi wa ngazi mbalimbali wa nchi hizi mbili
ili kukuza na kudumisha mahusiano. Ziara hizo ni pamoja na ile ya Rais
Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mhe. Benjamin Mkapa nchini Ethiopia mwaka
2005. Wakati wa ziara hii Mhe. Mkapa na aliyekuwa Waziri Mkuu wa
Ethiopia wakati huo, Hayati Meles Zenawi walisaini Mkataba wa Jumla wa
Ushirikiano.
Vile
vile, mwaka 2015 Mhe. Dessalegn alitembelea Tanzania na kushiriki
uzinduzi wa Kiwanda cha kutengeneza dawa za kuua viluwiluwi vya mbu
wanaoeneza Malaria kilichojengwa Kibaha, Pwani kwa ufadhili wa Serikali
ya Cuba. Pia, Mhe. Dessalegn alishiriki sherehe za kuapishwa kwa Rais wa
Awamu ya Tano wa Tanzania, Mhe. Rais Magufuli zilizofanyika mwezi
Novemba, 2015 Jijini Dar es Salaam.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam
30 Machi, 2017
|
No comments :
Post a Comment