NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imepanga kuondoka katika
uchumi wa chini na kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025 ambapo katika
kufikia azma hiyo imeweka juhudi kwenye uanzishwaji wa viwanda
mbalimbali kuanzia vidogo hadi vikubwa.
Mpango wa kufikia uchumi wa kati
unalenga kuiwezesha serikali kujitegemea na tayari hatua mbalimbali
zimechukuliwa ili kuweza kufikia azma hiyo.
Dira ya Taifa ya Maendeleo,
imeainisha malengo mbalimbali ikiwa ni pamoja na
kujenge uchumi imara
wenye uwezo wa kukabiliana na ushindani.
Katika kuhakikisha mkakati huo
unafanikiwa Serikali imeweka sera na mazingira mazuri kwa ajili ya
kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza kwenye viwanda.
Hivi karibuni Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa alikwenda nchini Mauritius kumwakilisha Rais Dk. John
Magufuli kwenye uzinduzi wa Jukwaa la Uchumi Barani Afrika (AEP).
Baada ya kumaliza uzinduzi huo
Waziri Mkuu alipata fursa ya kutembelea viwanda mbalimbali nchini
Mauritius na kuhamasisha wawekezaji waje nchini ili kuongeza uzalishaji
utakaokuza uchumi na kuongeza pato la taifa.
KIWANDA CHA SUKARI CHA ALTEO
Akiwa kiwandani hapo Waziri Mkuu
alipata maelezo ya uendeshaji wake kuanzia hatua ya utayarishaji wa
mashamba ya miwa hadi uzalishaji wa sukari.
Waziri Mkuu alifurahishwa na
teknolojia ya kisasa inayotumika kiwandani hapo hali iliyomfanya
ashawishike kuwashawishi wawekezaji hao kuja nchini kupanua uwekezaji
kwa kuongeza mashamba ya miwa na uzalishaji wa sukari.
Kiwanda cha sukari
kinachomilikiwa na kampuni ya Alteo kina uwezo wa kukamua tani 400 za
miwa kwa saa na kuzalisha tani 170,000 za sukari kwa mwaka.
Kampuni ya Alteo inamiliki
kiwanda cha sukari cha TPC mkoani Kilimanjaro kwa ubia na Serikali ya
Tanzania na kinazalisha tani 110,000 kwa mwaka.
Aidha, Waziri Mkuu amefanya mazungumzo na uongozi wa kiwanda hicho na kuwashawishi waongeze maeneo ya uwekezaji nchini.
“Tekonolojia wanayoitumia
katika uendeshaji wa kiwanda chao ni nzuri hivyo tumewashawishi waje
kuongeza maeneo ya uzalishaji wa sukari nchini ili tuweze kukidhi
mahitaji,” amesema.
Waziri Mkuu amesema Tanzania
kuna viwanda vitano vya sukari ambavyo ni Mtibwa, Mahonda (Zanzibar),
TPC, Kilombero na Kagera ambavyo uzalisha tani 320,000 kwa mwaka wakati
mahitaji ya ndani ya nchi kwa mwaka ni tani 420,000.
Kwa upande wake Waziri wa
Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Khalid Salum
Mohammed amesema Zanzibar kuna kiwanda kimoja cha sukari ambacho
uzalishaji wake haukidhi mahitaji kutokana na uhaba wa malighafi.
Dk. Khalid amewakaribisha
kampuni ya Alteo kwenda Zanzibar kushirikiana na Serikali katika
uwekezaji hususani kwenye viwanda vya sukari.
Naye Mtendaji Mkuu wa Kampuni
hiyo Bw. Patrick de Labauve amesema wamekubali kuongeza maeneo ya
uwekezaji wa mashamba ya miwa nchini.
Pia ameomba Serikali iwapatie
fursa ya uwekezaji katika sekta ya utalii mkoani Kilimanjaro kwani kuna
vivutio vingi vya utalii ukiwemo mlima Kilimanjaro.
Akizungumzia kuhusu ajira
amesema kiwanda cha TPC kimeajiri wafanyakazi 3,000 wakiwemo 1,900 wa
kudumu wa ndani utakaotosheleza mahitaji na kupata ziada.
Kusimamia mfumo mzima wa
usambazaji wa sukari nchini ikiwa ni pamoja na kuwadhibiti
wafanyabishara wenye tabia ya kuhodhi soko la sukari kwa lengo la
kusababisha upungufu usio halisi wa sukari (artificial shortage).
Kuendelea kuhamasisha na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwa wazalishaji wa sukari wa ndani ya nchi.
KIWANDA CHA SAMAKI
Waziri Mkuu pia alitembelea
kiwanda cha kusindika samaki aina ya jodari na kuwakaribisha viongozi wa
kiwanda hicho kuja nchini kuangalia maeneo ya uwekezaji wa viwanda vya
samaki.
Amesema Serikali imeweka sera
nzuri za uwekezaji na pia ina maeneo mengi na mazuri kwa ajili ya
uwekezaji wa viwanda vya samaki, ambayo ni bahari, mito na maziwa ambayo
aina mbalimbali za samaki.
Waziri Mkuu amesema hayo
wakati alipotembelea kiwanda cha samaki cha Mer des Mascareignes
kilichoko jijini Port Louis nchini Mauritius.
“Tanzania kuna fursa nyingi
za uwekezaji hasa kutokana na mazingira yake. Mnaweza kuja kuwekeza
kwenye viwanda vya usindikaji wa samaki tuna bahari, mito na maziwa
yenye samaki wa aina mbalimbali,” alisema.
Majaliwa alisema Serikali
imedhamiria kuimarisha uchumi wake kupitia sekta ya viwanda ili kuongeza
tija kwa Taifa na kwa wananchi kiujumla hivyo wanahitaji wawekezaji
waliotayari kuja kuwekeza nchini.
Kwa upande wake Waziri wa
Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Khalid Salum
Mohammed alisema Tanzania inahitaji wawekezaji watakaowekeza kwenye
uvuvi wa kina kirefu na ujenzi wa viwanda vya samaki.
Dk. Khalid alisema lengo la
uwekezaji huo ni kukuza uchumi wa Taifa pamoja kupanua soko la ajira na
kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi wake.
Naye Meneja Mkuu wa kiwanda
hicho, Bw. Patrick Hill alisema wamefurahia mualiko wa kuja Tanzania kwa
ajili ya kuangalia fursa na uwekezaji na kwamba wako tayari
kushirikiana na Serikali.
Alisema kampuni yao
inajishughulisha na usindikaji wa samaki aina moja tu ya jodari na
wananunua kutoka kwa makampuni makubwa ya uvuvi huku wateja wao wakubwa
wakiwa ni bara la Ulaya.
KIWANDA CHA NGUO
Akiwa kwenye kiwanda cha nguo cha
Compagnie Mauricienne De Textile Ltee kinachotengeneza nguo kwa kutumia
teknolojia ya kisasa nchini Mauritius chenye uwezo wa kutengeneza tani
milioni 40 hadi 50 kwa mwaka.
Waziri Mkuu aliwakaribisha
wawekezaji hao kuja nchini kuwekeza katika viwanda vya kutengeneza nyuzi
na nguo kwa kuwa kuna malighafi za kutosha kwa ajili ya uzalishaji huo.
“Tumefarijika na uwekezaji
wenu na tumejionea namna ambavyo mnavyoendesha kiwanda chenu kuanzia
utengenezaji wa nyuzi hadi nguo, hivyo tunahitaji viwanda kama hivi
nchini Tanzania kwa sababu sisi tunazalisha pamba nyingi na yenye ubora
unaokubalika kimataifa,” alisema.
Waziri Mkuu alisema madhumuni
ya kuwakaribisha wawekezaji hao kuja Tanzania na kuwekeza katika
viwanda vya kutengeneza nyuzi yanalenga kuboresha kilimo cha pamba na
kuwawezesha wakulima kupata tija.
“Tunalima pamba nzuri na hawa
hawalimi wananunua kutoka nje ya nchi yao, hivyo wakija kuwekeza
Tanzania itawarahisishia kupata malighafi ya uhakika na kwa urahisi ”
alisema.
Alisema viwanda hivyo vitasaidia
maendeleo ya kilimo cha pamba kwa sababu vitatoa ajira kwa wananchi
wengi hivyo kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umasikini
wa kipato.
Mbali na kuwakaribisha
wawekezaji hao, Waziri Mkuu alitoa wito kwa wananchi wenye uwezo
kuhakikisha wanajenga viwanda vya nyuzi kwenye mikoa yote inayozalisha
pamba ili waweze kuiongezea thamani kabla ya kuiuza.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Fedha wa kiwanda hicho David Too Sai Voon alisema wamefurahishwa na
mualiko wa kuja Tanzania kwa ajili ya kuangalia maeneo ya uwekezaji wa
viwanda vya nyuzi na nguo.
David alisema kiwanda chao
kilianzishwa mwaka 1986 na kwa sasa kimeajiri wafanyakazi 18,000 ambapo
mauzo yao kwa ni dola milioni 200. “Nguo tunazotengeza ni za kiwango cha
kimataifa na tunauza katika maduka makubwa barani Ulaya,”
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
SLP 980, DODOMA
ALHAMISI, MACHI 31, 2017.
No comments :
Post a Comment