Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri
Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Eric Shitindi,
akiwahutubia wafanyakazi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi
(OSHA) katika kikao chao cha baraza. Kulia ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa
Wakala Bi. Khadija Mwenda na viongozi wa baraza hilo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri
Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Eric Shitindi, akiwa
katika picha ya pamoja na watumishi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali
pa Kazi (OSHA) mara baada ya kufungua kikao chao cha baraza.)
Wafanyakazi wa Wakala wa Usalama
na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) wakifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu Ofisi
ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Eric Shitindi
(hayupo pichani) alipofungua kikao cha baraza lao mjini Dodoma jana.
…………………….
Na Mwandishi Wetu
Mabadiliko ya mazingira ya
ufanyaji biashara yanayoletwa na maendeleo ya uchumi wa viwanda pamoja
na mnyororo wa thamani, yameelezwa kuwa changamoto kubwa katika
jitihada
za kuimarisha hali ya usalama na afya za wafanyakazi katika sehemu za
kazi hapa nchini.
Changamoto hiyo imetolewa na
Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Watu
Wenye Ulemavu, Bw, Eric Shitindi, wakati akifungua kikao cha Baraza la
Wafanyakazi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) mjini
Dodoma leo.
Amesema mabadiliko hayo
yanahusisha matumizi ya teknolojia za kisasa na ongezeko kubwa la idadi
ya wafanyakazi katika sekta zote za umma na za binafsi jambo ambalo
linahitaji utaalamu mkubwa katika kuweka na kusimamia mifumo ya kulinda
afya na kuwahakikishia usalama wafanyakazi wote wanapokuwa katika sehemu
zao za kazi.
“Hivyo mkiwa kama wataalamu katika
masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi mnatakiwa kuwa na mikakati
mipya ya kukabiliana na changamoto hizo. Hii itakuwa ni pamoja na
kubadilika kifikra na kimtazamo katika utendaji kazi,” alisema Katibu
mkuu Shitindi.
Katibu mkuu huyo amesisitiza
muhimu wa kutafuta mbinu mbadala ya kuweza kupanua wigo wa kufanya kazi
hasa kwa kuzingatia ukubwa wa kazi zilizopo.
Aidha Bw. Shitindi ameupongeza
OSHA kwa mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa mpango kazi wake
katika kipindi cha robo tatu za mwaka huu wa fedha (2016/2017) ambapo
kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa katika baraza hilo, taasisi
imevuka malengo katika kaguzi, utoaji wa mafunzo ya usalama na afya
kazini pamoja na huduma mbali mbali zitolewazo mahali pa kazi.
Katika hotuba yake, Katibu Mkuu
aliahidi kuendelea kuisaidia OSHA kutatua changamoto zilizopo zikiwemo
za kiutendaji na kuwaasa watumishi wa Wakala kuzingatia maadili ya
utumishi wa umma ikiwemo kuepuka kujihusisha na vitendo vya upokeaji
rushwa wanapotekeleza majukumu yao.
“Wizara imekuwa ikipokea
malalamiko mengi ya namna mnavyohudumia wateja na kushuka kwa maadili ya
kiutendaji miongoni mwa watumishi, mfano masuala ya rushwa, hivyo
wakati tunaendelea kushughulikia matatizo hayo ni vyema sasa mkaanza
kubadilika kwa kufuata sheria, taratibu, kanuni na miongozo mbalimbali
ya utendaji kazi katika taasisi,” amesisitiza Bw, Shitindi.
Kikao hicho cha baraza la wafanyakazi wa OSHA ambacho kimeanza leo kitamalizika kesho ambapo pamoja na mambo mengine kitapitia na kujadili makadirio ya bajeti ya mwaka wa fedha wa (2017/2018) ili kujiridhisha kama itawawezesha kufanikisha utekelezaji wa malengo ya wakala yaliyowekwa.
No comments :
Post a Comment