Na Mwandishi wetu
Serikali yawabwaga wanaopinga
Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 baada ya Mahakama Kuu ya
Tanzania Kanda ya Mwanza kutupilia mbali pingamizi hilo.
Akizungumza na Mwandishi wa habari
hii, Wakili wa Serikali Evordy Kyando alisema kuwa Mahakama Kuu Kanda
ya Mwanza imetupilia mbali pingamizi lililotolewa na baadhi ya wadau wa
habari wakipinga baadhi ya vifungu katika Sheria hiyo baada ya kukosa
mashiko.
Alisema kuwa katika kesi hiyo
namba 2 ya mwaka 2017, walalamikaji wanadai kuwa kuna baadhi ya vifungu
vya sheria hiyo vinakandamiza uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza na
vinakiuka Ibara ya 18 ya katiba ya nchi.
Aidha, Wakili Kyando alibainisha
baadhi ya vifungu katika sheria hiyo vilivyolalamikiwa ni pamoja na 7
(2) (B) (III) (IV) and (V), 7 (3) (A), (B), (C), (F), (G), (H), (I),
(J),8, 9(B), 10(2), 11(4), 13, 14, 19, 20, 21, 24, 25, 26, 35, 36, 37,
38, 39, 40, 50, 52, 53, 54 58 na 59 vya Sheria ya Huduma za Habari Na.
12 ya 2016.
Akifafanua zaidi, Wakili Kyando
alisema kuwa kuna baadhi ya hoja zilizopelekea Shauri hilo kutupiliwa
mbali ikiwemo vifungu vya Sheria vilivyolalamikiwa viliandikwa vibaya
kulingana na Sheria yenyewe ilivyo, viapo vilivyowasilishwa katika
kufungua shauri vilikuwa na makosa, jambo lililolalamikiwa halina
mashiko, si la kisheria kutokana na malalamiko ambayo hayaoneshi msingi
ulipo ikiwa lengo la Sheria ni kuboresha mazingira mazuri ya waandishi,
Elimu, mishaara na vitambulisho.
Jopo la wanasheria linalowakilisha
upande wa Serikali liliongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali kutoka Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Makao Makuu, Mark Mulwambo, Wakili
Mwandamizi wa Serikali toka Kanda ya Mwanza Ndamugoba Castus na Wakili
wa Serikali Evordy Kyando.
Kesi hiyo iliyofunguliwa na Umoja
wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na kampuni ya Hali
Halisi Publishers Limited, wakipinga baadhi ya vipengele vya Sheria ya
Huduma za Habari 2016.
No comments :
Post a Comment