Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kushoto), akimsikiliza Meneja wa
Mamlaka ya Bandari Kanda ya Ziwa, Bw. Abel Moyo, alipokagua gati ya
Bandari ya Bukoba, mkoani humo jana.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa mmoja wa Afisa
Fedha kutoka Mamlaka ya Bandari (TPA), katika Bandari ya Bukoba
alipokagua utendaji wa bandari hiyo na kubaini utaratibu mbovu wa
ukusanyaji mapato.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akiongea na mafundi wanaofanya
ukarabati katika bandari ya Bukoba, alipokagua utendaji wa bandari hiyo
Mkoani Kagera.
Baadhi ya Watumishi wanaofanya
kazi katika taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mkoani Kagera, wakimsikiliza Waziri wa Wizara hiyo, Profesa
Makame Mbarawa (hayupo pichani), alipooongea nao mkoani humo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (katikati waliokaa), akiwa katika
picha ya pamoja na Watumishi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mkoani Kagera, mara baada ya kuongea
nao na kuwaeleza mikakati mbalimbali ya WIzara hiyo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
………………
Serikali imewatoa wasiwasi wakazi
na wafanyabishara wa Kanda ya Ziwa Victoria kuwa iko
katika hatua za
mwisho za kukamilisha taratibu za ujenzi wa meli mpya kubwa na ya kisasa
ambayo itakuwa na uwezo wa kuchukua mizigo tani 300, magari 25 na
madaraja matatu kwa ajili ya sehemu ya kukaa abiria.
Akizungumza na waandishi wa habari
mara baada ya kukagua bandari ya Bukoba, mkoani Kagera, Waziri Profesa
Mbarawa amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo umechelewa kutokana na
kukosa sifa kwa Makandarasi wawili waliojitokeza mwanzoni kwa ajili ya
kutekeleza mradi huo wa ujenzi.
“Nataka kujenga meli ya kisasa ili
kuweza kufupisha safari kutoka masaa 10 hadi matano kutoka Bukoba hadi
Mwanza na hivyo kufanya usafiri wa majini kuwa wa kuaminika na salama”,
amesema Prof. Mbarawa.
Aidha, Waziri Mbarawa amefafanua
kuwa kutokana na utendaji mbovu wa bandari hiyo anatarajia kuleta
wafanyakazi makini kwa ajili ya kupitia taaria za kifedha za utoaji na
usafirishwaji wa mizigo bandarini hapo.
Naye, Meneja wa Mamlaka ya Bandari
Kanda ya Ziwa, Bw. Abel Moyo ameiomba Serikali kufanya ukarabati wa
Meli nchini hasa zilizopo Kanda ya Ziwa ili kuweza kuondoa adha
wanazozipata wakazi wa mikoa hiyo.
Katika hatua nyingine, Waziri
Prof. Mbarawa amekagua Shirika la Posta mkoani humo na kuahidi kupeleka
wakaguzi wa ndani kwa ajili ya kukagua na kujiridhisha juu ya mapato na
matumizi ili kubaini ubadhilifu unaofanywa na watendaji wa Posta.
“Tunataka Posta iwe safi na
kupunguza changamoto zinazoikabili kwani ni Shirika kubwa na lenye
Rasilimali nyingi ambazo zikitumiwa vizuri zinaweza kuinua mapato ya
Shirika hilo”, amesisitiza Waziri Mbarawa.
Akiwa katika ofisi za Wakala wa
Ufundi na Umeme (TEMESA), mkoani humo, Waziri Prof. Mbarawa ameuagiza
Wakala huo kuzingatia viwango na ubora unaotakiwa katika utengenezaji wa
magari yanayokuja kupata huduma katika karakana yao.
Kwa upande wake, Meneja wa TEMESA,
Eng, Zephrine Bahyona amemuomba Waziri kusaidia kusisitiza Taasisi za
Serikali kupeleka magari yao kwenye karakana zao na kulipa madeni kwa
wakati ili kupunguzia Wakala huo mzigo wa madeni kutoka katika taasisi
hizo.
Waziri Prof. Mbarawa yupo katika
ziara ya kikazi wilayani Bukoba, mkoani Kagera ambapo ametembelea na
kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Taasisi zilizo chini ya
Wizara yake.
No comments :
Post a Comment