Na Mwandishi Wetu, Meatu
MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Anthony
Mtaka amefanikiwa kumaliza mgogoro wa muda mrefu kati ya mwekezaji
katika Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) Makao iliyopo wilayani
Meatu, na baadhi ya vijiji vinavyounda jumuiya hiyo. Mwekezaji huyo
Mwiba Holdings, amekuwa na mgogoro wa mipaka, mkataba wa kumiliki ardhi
na uanzishaji wa ranchi na baadhi ya vijiji hivyo kiasi cha kusababisha
kuwa na mahusiano mabaya na wananchi ambao wamekuwa wakisusia misaada
mbalimbali inayotolewa na mwekezaji huyo.
Hata hivyo, chanzo halisi cha
mgogoro huo kimegundulika kuwa ni viongozi wa baadhi ya vijiji ambao
wamekuwa wakipigania maslahi yao binafsi huku wakisambaza taarifa za
upotoshaji juu ya mwekezaji huyo na kujenga chuki kwa wananchi. Vijiji
vinavyounda WMA ya Makao ni pamoja na Makao, Iramba ndogo, Sapa,
Mwangudo, Jinamo, Lukale, Mbushi, Mwabagimu na Sunga.
Baadhi ya viongozi hao wa vijiji
pia wamekuwa wakisambaza taarifa potofu kwa wananchi kwamba Mkuu huyo wa
mkoa na mkuu wa wilaya ya Meatu wamehongwa na mwekezaji ili
kuwakandamiza wananchi, jambo lililothibitika kuwa si la kweli.
Kutokana na mgogoro huo kuzidi
kuota mizizi huku uongozi wa CCM Mkoa wa Simiyu nao ukichukua upande,
Mtaka alilazimika kuitisha kikao cha usuluhishi kilichoshirikisha wadau
wote wakiwamo Kamati ya Siasa ya CCM mkoa na wilaya, viongozi na
watendaji wa serikali ngazi ya mkoa na wilaya, viongozi wa vijiji tisa
vinavyounda WMA Makao, mwekezaji na wadau wengine akiwamo Mbunge wa
Meatu na Mwakilishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu.
Akizungumza katika kikao hicho
kilichofanyika mwishoni mwa wiki mjini hapa, Mtaka aliwakemea viongozi
wanaoeneza taarifa potofu wilayani humo na kusababisha shughuli za
maendeleo kukwama huku akiahidi kuwachukulia hatua zinazostahili
viongozi wa namna hiyo.
“Katika masuala ya maendeleo ya
wananchi sina mzaha. Nipo tayari kuwa kiongozi unpopular (asiyependwa)
ili mradi shughuli za maendeleo za wananchi zinaenda mbele.
“Mgogoro na Mwiba umekuwa kama
mkuki mnaojichoma wenyewe kila siku kwa sababu wenyewe ndiyo mlioingia
mikataba na mwekezaji wakati sisi hatukuwapo na wala hatuna maslahi
yoyote binafsi hivyo acheni maneno maneno, kaeni chini mzungumze tusonge
mbele,” alisisitiza Mkuu huyo wa mkoa.
“Mmefikisha malalamiko, tena kwa
maandishi hadi kwa Waziri Mkuu lakini uhalisia ni kuwa mengi mliyopeleka
hayana ukweli, ni hisia na mengine ni fitna tu. Sasa wekeni kila kitu
hadharani hapa, tumalize suala hili leo na tujikite zaidi katika mambo
ya maendeleo,” alisema.
Kuhusu mgogoro wa mpaka hasa
katika kijiji cha Buhongoja ambako alama ya mpaka yenye
namba 314
inadaiwa kusogezwa kinyemela kwa umbali wa kilomita 10, Mkuu huyo wa
mkoa alizitaka pande zinazohusika kukutana na kutatua tatizo hilo kwa
kurejea katika eneo la awali bila ya mikwaruzano yoyote. Aliamuru pia
pande zinazohusika katika suala la mkataba wa umiliki wa ardhi,kukaa
meza moja na kuacha mambo ya kukimbilia kwa wasuluhishi ambao wamekuwa
wakidai fedha nyingi ambazo zingeweza kutumika kwa maendeleo ya vijiji
au wilaya ya Meatu.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu,
Jumanne Sagini aliahidi kupeleka wataalam watatu watakaosaidiana kutatua
mgogoro huo wa umiliki wa ardhi watakaosaidiana na wake wa wilaya ili
kutatua suala hilo ndani ya wiki mbili.
Awali, Mwenyekiti wa Kijiji cha
Makao, Anthony Phillipo alieleza kuwa kijiji kilazimika kupelaka suala
hilo kwenye Tume ya Usuluhishi wa Migogoro Dar es Salaam ambako kijiji
walishindwa kulipa gharama za usuluhishi huo walizotozwa na Jaji Mstaafu
Thomas Mihayo. Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, Dk. Titus Kamani
alieleza chama hicho tawala kusikitishwa na mgogoro huo unaokwamisha
shughuli za maendeleo ya wananchi na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya
chama hicho.
“Ndugu zangu, sisi tunajiandaa
kushinda katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 na uchaguzi
mkuu wa mwaka 2020, kwa hiyo tunawaomba tusikubali kuingizwa katika
migogoro kama hii ambayo haina tija kwa wananchi.
“Tunataka wakati wa uchaguzi
utakapofika tushinde pila pressure (msukumo) yoyote na tunachotaka ni
mshikamano,maelewano mazuri baina ya wadau wote ili tufanye shughuli za
maendeleo kwa faida ya mkoa wetu wa Simiyu na wilaya ya Meatu,”
alisisitiza.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais (Mazingira) Mpina Luhaga ambaye pia ni mbunge wa Kisesa
wilayani Meatu alisema katikA kikao hicho kuwa mwekezaji huyo amekuwa
akifuata sheria zote za nchi katika utekelezaji wa majukumu yake na ni
wazi kwamba wananchi watashindwa katika madai yote wanayofungua katika
Tume ya Usuluhishi wa migogoro.
“Mimi nimefuatilia malalamiko haya
ya wananchi serikalini na hasa Wizara ya Maliasili na Utalii na hawa
jamaa wamefuata taratibu zote na wanalipa tozo zote wanazostahili kulipa
hivyo tunapaswa kuwa waangalifu,” alisema.
Mkurugenzi wa Mwiba Holdings,
Abdulkadir Mohamed Luta alisema kuwa Kampuni hiyo ipo tayari kukaa meza
moja na kusaidia usuluhishi wa mgogoro wowote ili wajikite zaidi katika
shughuli za maendeleo ya wananchi. Aliongeza kwamba kampuni hiyo ilikuwa
tayari kugharamia hata suala la mkataba wa umiliki wa ardhi
lililofikishwa Tume ya Usuluhishi wa Migogoro ili mradi tu suala hilo
liishe na waendelee na mambo ya maendeleo
Alisema watazifanyia kazi hoja
zote zilizotolewa na wananchi katika kikao hicho na kwamba sera ya
kampuni hiyo ni kushirikiana na wananchi na wamekuwa wakitekeleza sera
hiyo kwa vitendo.
Mbunge wa Meatu, Salum Khamis
maarufu kwa jina la Mbuzi, alisema kuwa hana mgogoro na mwekezaji yoyote
lakini hatakaa kimya kutetea maslahi ya wananchi wake ambao ndio
waajiri wake kila atakapoona kuna sababu ya kufanya hivyo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Wilaya ya Meatu, Pius Machungwa aliahidi kuipatia kiwanja cha kujenga
ofisi Kampuni ya Mwiba Holdings katika makao Makuu ya wilaya hiyo ili
iwe karibu na wananchi, na kwamba watashirikiana na kampuni hiyo katika
shughuli za maendeleo wilayani humo.
No comments :
Post a Comment