Wednesday, March 29, 2017

RAIS MAGUFULI AKUTANA NA MAWAZIRI WA NISHATI NA MADINI WA TANZANIA NA UGANDA


v 1
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akifungua kikao cha pamoja cha Mawaziri wa Serikali za Tanzania na Uganda pamoja na wadau kuzungumzia mradi wa ujenzi wa Bomba la Kusafirishia Mafuta Ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga.
Mkutano huo, uliofanyika Ikulu, Dar es salaam, Jumanne Machi 28, 2017, ulihudhuriwa na Mawaziri wa Nishati na Madini pamoja na Mawaziri wa Ardhi wa nchi hizo mbili, Wanasheria wa Serikali  na kampuni washirika wa mradi huo Lake Albert (CNOOC, TOTAL na TULLOW).
v
Pamoja na mambo mengine, Mawaziri, Maafisa na Wataalam wa pande zote husika walikaa na kukubaliana kwamba rasimu ya  makubaliano rasmi ya kuanza kwa mradi yawe yamekamilika na kuwa tayari katika kipindi cha wiki mbili ili kuwezesha Marais wa Tanzania na Uganda kuweka jiwe la msingi kuashiria kuanza ujenzi wa kihistoria wa mradi huo wa
bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga, Tanzania. 
PICHA NA IKULU.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 28 Machi, 2017 alikutana na Mawaziri wa Nishati na Madini wa Serikali za Tanzania na Uganda katika Ukumbi wa Baraza la Mawaziri Ikulu, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili Maendeleo ya Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima Nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga – Tanzania, hususan katika masuala ya kikodi yatakayotumika katika mradi huo.
Mawaziri hao ni pamoja na Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini Nchini Uganda, Mhandisi Irene Muloni pamoja na ujumbe wake na Waziri wa Nishati na Madini Nchini  Tanzania Profesa Sospeter Muhongo pamoja na wataalam kutoka Serikali zote mbili.
Wajumbe wengine ni pamoja na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. John Lukuvi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Mcheche Masaju pamoja na Makampuni ya Uwekezaji ya Mkondo wa Juu wa Ziwa Albert Nchini Uganda ya TOTAL, CNOOC na TULLOW.
Masuala ya kikodi ni moja ya vipengele muhimu katika ukamilishwaji wa mkataba wa kimataifa kati ya nchi ya Tanzania na Uganda.
Mbali na kukaribisha washiriki wa mkutano huo, Mhe. Dkt. Magufuli  alisisitiza ahadi yake na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Museveni ya kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika kwa wakati.
Aidha, Dkt. Magufuli  aliagiza wawekezaji kutekeleza mradi huo bila kuchelewa kwa maana  Serikali imeshaweka mazingira mazuri  ya utekelezaji wa mradi ikiwa ni pamoja na masuala ya usalama, upatikanaji wa ardhi, kodi  hivyo kupunguza gharama za ujenzi Tanzania.
Pamoja na mambo mengine mawaziri, maafisa na wataalam wa pande zote husika walikaa na kukubaliana kwamba, rasimu ya makubaliano rasmi ya kuanza kwa mradi yawe yamekamilika na kuwa tayari katika kipindi cha wiki mbili  ili kuwezesha Marais wa Tanzania na Uganda, kuweka jiwe la msingi kuashiria  ujenzi wa kihistoria  wa mradi huo wa bomba la mafuta kutoka Hoima Nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga-Tanzania.
Mradi huu upo katika hatua ya awali ya tahmini ya mazingira pamoja na kubaini maeneo mradi utakapopita ili mradi kuweza kutekelezwa kwa kasi pindi utakapoanza.
Imetolewa na:-
Kitengo cha Mawasilino Serikalini
Wizara ya Nishati na Madini
Machi 29, 2017

No comments :

Post a Comment