Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Kebwe S.
Kebwe ametoa rai kwa vijana kujiweka katika vikundi ili wapate fursa za
kupata mikopo kutoka Serikalini na kwa wadau mbalimbali.
Mkuu wa Mkoa ametoa rai hiyo leo
mkoani Morogoro alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hii juu ya
maendeleo ya vijana wenye ulemavu waliopo chini ya Mradi wa Uwezeshaji
Vijana Kiuchumi (YEE) unaoratibiwa na shirika la Plan International.
Mhe. Kebwe amesema suala la vijana
na wanawake kuunda vikundi ni la muhimu kwani
Serikali kupitia
Halmashauri zote nchini ina utaratibu wa kutenga asilimia kumi kutoka
katika mapato ya ndani ya Halmashauri husika kwa ajili ya kuwasaidia
wanawake na vijana ili waweze kujikwamua hasa katika nyanja ya kiuchumi.
“Serikali pekee haiwezi kufanya
kila kitu hivyo kupata mradi kama huu wa kuwasaidia vijana kiuchumi
kutoka Umoja wa Ulaya ni fursa nzuri kwa vijana kujikomboa na njia
rahisi ya kuoneka mna uhitaji ni dhahiri kuwa mnatakiwa muwe katika
vikundi,”alisema Mhe. Kebwe.
Mhe. Kebwe ameongeza, uundwaji wa
vikundi unasaidia kufahamu ukubwa wa kikundi, kiasi cha msaada, eneo
kikundi kilipo na aina ya shughuli inayofanywa na kikundi husika.
Amefafanua kuwa kwa hali halisi
fedha za mradi haziwezi kutolewa kwa mtu mmoja mmoja bali ni kwa njia ya
vikundi ili kurahisisha ufatiliaji na kupunguza gharama za uendeshaji
hivyo vijana wasitarajie kupata mkopo au kusaidiwa na shirika wakiwa
wamekaa vijiweni.
Aidha,amewasisitiza vijana hasa
walemavu kujitokeza kwa wingi katika awamu ya mwisho ya mradi huo kwani
mradi huo upo kwa ajili ya vijana wote.
Mradi huo wa miaka mitatu
(2015/2018) unatekelezwa kwa ushirikiano wa mashirika ya VSO, CCBRT,
VETA, UHIKI, CODERT pamoja na Serikali ya Tanzania huku ukiratibiwa na
Shirika la Plan International chini ya ufadhili wa Umoja wa Nchi za
Ulaya (EU)
No comments :
Post a Comment