Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)
lenye dhamana ya kuratibu ukuzaji na uendelezaji wa sekta ya Sanaa
nchini litatoa tuzo kwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini
waliofanya vizuri kitaifa katika masomo ya Sanaa za Muziki, Ufundi na
Maonyesho kwenye matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne
uliofanyika mwezi Oktoba,2016 na matokeo yake kutoka
hivi karibuni.
Aidha, sambamba na kutunuku vyeti na Zawadi za fedha taslimu kwa
wanafunzi hao BASATA litatambua mchango wa walimu wa masomo husika na
shule zilizofanya vizuri katika mchepuo wa Sanaa.
Hafla hiyo ambayo itawakutanisha
wanafunzi hao, walimu wao pamoja na wadau mbalimbali wa Sanaa itafanyika
siku ya Jumatatu tarehe 27/03/2017 saa 4:00 asubuhi katika Ukumbi wa
BASATA ulioko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam.
Ili kutambua,kuibua na kukuza
vipaji vya Sanaa kutoka ngazi za chini na kuamsha ari ya masomo ya
mchepuo wa Sanaa katika mitaala yetu ya elimu sambamba na kujenga weledi
katika tasnia ya Sanaa kwa ujumla wake Baraza limeamua kurejesha
programu hii ya utoaji wa tuzo kwa wanafunzi wa shule za sekondari kila
mwaka ambao wanashika nafasi za juu kitaifa katika masomo ya sanaa
husasan Sanaa za Ufundi, Maonyesho na Muziki
Itakumbukwa kuwa BASATA limekuwa
na mwendelezo wa programu mbalimbali za Sanaa kwa watoto zilizoanza
tangu miaka ya 1980 ambazo zimepata kuibua na kukuza vipaji vya wasanii.
BASATA linachukua fursa hii kuwaalika wananchi na wadau wote wa sanaa
kufika kwa wingi kushuhudia utoaji wa tuzo hizi.
Sanaa ni kazi, tuipende, tuikuze na kuithamini
Godfrey Mngereza, Katibu MTENDAJI. 23 MACHI, 2017
No comments :
Post a Comment