Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu
Kanda ya Tanga Mhe. Imani Abood akielezea utekelezaji wa Mpango Mkakati
wa Miaka Mitano wa Mahakama ya Tanzania katika Kanda ya Tanga leo
ofisini kwake jijini Tanga.
Picha na Lydia Churi-Mahakama.
…………….
Na Lydia Churi-Mahakama, Tanga
Mahakama ya Tanzania imeshauriwa
kuwa na Mpango endelevu wa kuwajengea uwezo watumishi wake wa ngazi zote
ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania kanda ya Tanga Mhe. Imani Abood alitoa
ushauri huo leo jjini
Tanga alipokuwa akielezea utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano
wa Mahakama ya Tanzania katika Kanda yake.
Alisema pamoja na kuwa Mahakama
inaendesha mafunzo mbalimbali kwa watumishi wake lakini mafunzo hayo
hayana budi kutolewa kwa watumishi wote kuanzia ngazi ya chini mpaka
ngazi ya juu kabisa katika Mahakama.
Akizungumzia nguzo ya pili ya
Mpango Mkakati wa Mahakama inayohusu upatikanaji wa haki kwa wakati,
Mhe. Abood alisema ni muhimu suala la mafunzo likapewa kipaumbele hasa
kutokana na kukua kwa sayansi na Teknolojia.
Alisema , hivi sasa katika
Mahakama upo ushahidi wa kielekitroniki unaotolewa hivyo ni muhimu
mafunzo yakatolewa ili kuleta ufanisi katika suala zima la utoaji wa
haki.
Akizungumzia mikakati iliyowekwa
na kanda yake ili kuondosha mashauri mahakamani kwa wakati, Jaji Abood
alisema wanakusudia kuziwekea umeme Mahakama za Mwanzo kupitia Mradi wa
REA na kuwapatia Mahakimu wote katika kanda yake vitendea kazi kama vile
laptops na printer ili ziwarahisishie kutoa hukumu kwa wakati.
Alisema hivi sasa Mahakimu katika
Mahakama za Mwanzo hulazimika kupeleka hukumu walizoandika kwa mkono ili
zikachapishwe kwenye Mahakama za wilaya ambapo kuna umeme.
Alisema licha ya changamoto hizo,
bado watumishi wa Mahakama Kuu kanda ya Tanga wanakuwa wakifanya kazi
kwa bidii na Mahakimu kuhakikisha hukumu zinatolewa kwa wakati ikiwa ni
pamoja na na wananchi kupatiwa nakala za hukumu ndani ya siku 21
zilizopangwa.
Mkakati mwingine uliowekwa ili
kuondosha mashauri mahakamani ni pamoja na, kufanya vikao na Mahakimu
wafawidhi wa wilaya pamoja na wadau wa Mahakama ili kurahisisha kazi kwa
kuwa kila mdau anaposhughulikia eneo lake shauri huisha mapema.
No comments :
Post a Comment