Siku ya ugonjwa wa kifafa duniani
huadhimishwa duniani kote Jumatatu ya pili ya mwezi wa Februari kila
mwaka. Kauli mbiu ya siku hii kwa mwaka huu 2017 ni ‘WEKA UGONJWA WA
KIFAFA KWENYE TASWIRA’, kwa kiingereza ni ‘PUTTING EPILEPSY IN THE
PICTURE’ . Kauli mbiu hii ina lengo la kuhamasisha Jamii kuutambua zaidi ugonjwa huu.
Tanzania ina idadi kubwa ya
wagonjwa wa kifafa na katika Afrika na Duniani kwa ujumla, na ni
mojawapo kati ya nchi zenye wagonjwa wengi zaidi. Mfano vijiji vya
Mahenge idadi ya wagonjwa hawa ni kubwa hadi kufikia wagonjwa 37.5 kwa
kila idadi ya watu1000. Hivyo kuna zaidi ya idadi ya watu milioni moja
(1) nchini hapa ambao wana ugonjwa wa kifafa.
Ugonjwa wa kifafa ni moja wapo ya
sababu zinazochangia vifo nchini na ugonjwa huu unakadiriwa kuchukua
nafasi ya saba (7) hadi nafasi ya kumi na tano (15) kama kisababibishi
cha vifo Tanzania. Wagonjwa wa kifafa katika Tanzania wako katika hatari
ya kifo mara sita zaidi ukilinganisha na mwananchi wa kawaida kwenye
jamii. Zaidi ya 60% ya vifo vinavyotokana na matatizo ya kifafa,
husababishwa na athari za ugonjwa wa kifafa moja kwa moja.
Wagonjwa wengi wa kifafa ni
vijana, wakiwa na umri wa wastani wa miaka 15. Zaidi ya 24% ya wagonjwa
wa kifafa wana ulemavu mwingine wengi wao kutokana na kuangukia moto
wakati mgonjwa anapopatwa na degedege.
Mambo mengi yanayosababisha
kifafa yanazuilika kuanzia kuumia ubongo wakati mama anapojifungua,
magonjwa yanayosababishwa na vijidudu kama ‘parasite’ na ‘bacteria’. Pia
katika kipindi cha sasa watu wengi wanaopata ajali za magari , bodaboda
na kadhalika hupelekea kuumia kichwani na ubongo kuathirika na hivyo
kuugua ugonjwa huu wa kifafa.
Idadi kubwa ya watu nchini wana
mtazamo hasi kuhusu kifafa. Zaidi ya 36% ya watu bado wanaamini kuwa
ugonjwa kifafa unatokana na nguvu za giza au kulogwa.
Ugonjwa huu wa kifafa umefanywa
kuwa ugonjwa wa siri na zaidi ya 58% ya idadi ya watu huamini unaleta
ugonjwa sugu wa akili. Miongoni mwa jamii yetu bado inaaminika ni
ugonjwa wa kuambukiza na 50% ya wagonjwa wa kifafa hupatwa na msongo wa
mawazo na kukosa furaha.
Mfano watoto wenye umri wa
kuanza shule wenye tatizo hili la kifafa 45% hawapelekwi shule na 68% ya
wanaoenda shule mahudhurio yao hayaridhishi na 37% tu ndio humaliza
elimu ya msingi (Primary school education). Watoto hawa hawaruhusiwi
kucheza pamoja na wengine hivyo hubakia kufichwa katika jamii.
Zaidi ya 55% ya watu wenye kifafa
Tanzania hawana ajira. Watu pia huwakwepa kuwaoa ama kuolewa nao, na
kama wakioa au kuolewa wengi wao huachika ndani ya muda mfupi tu.
Ni asilimia hamsini (50%) tu ya
wagonjwa wa kifafa na ndugu zao hutafuta ushauri miezi miwili baada ya
dalili za kifafa kuanza. Zaidi ya 70% huenda kuwaona waganga wa jadi na
wengine viongozi wa dini. Aidha, ni 60% tu ya wagonjwa wa kifafa hufika
kwenye vituo vya afya ndani mwaka mmoja baada ya dalili za kifafa
kuanza. Hata hivyo 5-10% ndio huweza kupata matibabu sahihi. Hivyo idadi
kubwa ya watu wanaoishi na kifafa Tanzania huendelea kuwa tatizo la
ugonjwa huu.
Matibabu ya wagonjwa wenye tatizo
hili hutolewa bure kama ilivyo kwenye sera ya Afya ya Taifa kwani
ugonjwa huu ni mmoja wapo kati ya magonjwa sugu yaliyoainishwa kwenye
sera hii. Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
inagharamia matibabu haya kwa kutoa dawa 3 muhimu katika vituo vya
kutolea huduma za afya, dawa hizi ni Phenobarbitone , Phenytoin na
Carbamazepine. Hata hivyo kuna kipindi huwa kunatokea changamoto za
kukosekana kwa dawa hizi kwa baadhi ya maeneo, ambapo inapobainika
hushughulikiwa.
Zipo changamoto katika kutoa
elimu kwa pande zote mbili kwa upande wa wahudumu wa afya na jamii kwa
ujumla ili maisha ya watu yasikatishwe kwa sababu ya ugonjwa huu hapa
nchini.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Chama cha wataalamu
wa ugonjwa wa kifafa Tanzania tunaendelea kufanya kazi pamoja katika
kuimarisha afya za wale wanaoishi na ugonjwa huu kwa kuwapatia elimu
maalumu ya afya dhidi ya ugonjwa wa kifafa.
Jamii inapaswa kutambua na
kuelewa kuwa Hospitali ndio sehemu sahihi pa kwenda pale wanapokuwa na
dalili za ugonjwa huu. Kifafa ni ugonjwa au tatizo la mfumo wa fahamu
linalosababishwa na magonjwa mengi na unatibika. Hivyo tushirikiane
pamoja kuhamasisha watu wenye matatizo haya wanafika kwenye vituo vya
kutolea huduma za afya ili kupatiwa matibabu husika.
KIFAFA KINATIBIKA, WAHI UPATE MATIBABU SAHIHI.
Imetolewa na ;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
14/2/2017
No comments :
Post a Comment