Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Moses
Nnauye akioongea na Waandishi wa Habari kuhusu siku rasmi ya kuanza
kutumika kwa Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 pamoja na Kanuni
zake za 2017 katika Ukumbi wa Idara ya Habari Bungeni Mjini Dodoma
05/02/2017. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Dkt.
Hassan Abbasi.
PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM.
………………
Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Waziri wa Habari Utamaduni
Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ametanga rasmi kuanza kutumika kwa Sheria
ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2017.
Nape Nnauye ametoa taarifa hiyo
leo katika ukumbi wa Bunge, Mjini Dodoma alipokuwa akiongea na vyombo
vya habari juu ya kuanza kwa sheria hiyo na kanuni zake.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 1 cha
Sheria hiyo, ili ianze kutumika rasmi, Waziri wa Habari anatakiwa
kuitangaza tarehe ya kuanza kutumika, hivyo napenda kuufahamisha Umma
kuwa sheria hii imeanza kutumika tangu Desemba 31, 2016,” alifafanua
Nape Nnauye.
Aliendelea kwa kusema kuwa kuanza
kutumika kwa sheria hii ni jambo muhimu sana kwa tasnia hiyo kwa sababu
inaihamisha taaluma ya habari kutoka fani ambayo mtu yeyote anaweza
kujinasibu nayo hadi kuwa taaluma kamili yenye sifa mahsusi, maadili
yanayojulikana pamoja na vyombo vya kusaidia kusimamia utekelezaji wake.
Vile vile amesema kuwa, sheria
hiyo inaleta mfumo madhubuti wa kulinda haki za wanahabari kukusanya,
kuhariri na kusambaza habari zao kwa uhuru.
Pia sheria hiyo imeweka wajibu kwa
wale watakaokiuka misingi na maadili ya taaluma hiyo, hivyo ukurasa
mpya wa haki na wajibu umefunguliwa kupitia sheria hiyo.
Aidha amesema kuwa, Wizara
imechambua maoni mbalimbali kuhusiana na sheria hiyo ambapo moja ya
maoni hayo ilikuwa ni kiwango cha elimu cha mtu atakayeruhusiwa kufanya
kazi ya taaluma hiyo.
Ambapo wapo waliopendekeza
kiwango cha elimu kiwe cheti, wengine diploma, digrii na hata PhD na
wengine walitaka awe mtu yeyote anayejua kusoma na kuandika.
Amesema kuwa Serikali imesimama
katikati ya maoni hayo, na sifa ya chini kabisa kwa kuanzia itakuwa ni
Diploma ya uandishi wa Habari. Hivyo Serikali imetoa kipindi cha miaka
Mitano kuanzia Januari, 01, 2017 kwa waandishi ambao hawana sifa hizo
kujiendeleza na kufikia kiwango hicho cha elimu.
Hivyo basi, Idara ya Habari
MAELEZO itaendelea kutoa “Press Card” bila kuwabana wanahabari kwa
kuangalia vigezo hivi vya kitaaluma bali dhamana ya waajiri wao.
Sheria ya Huduma za Habari, 2016
ilisainiwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli Novemba 16, 2016 na
kuchapishwa kwenye gazeti la Serikali Novemba 18, 2016.
No comments :
Post a Comment