*Asema mikutano ya vijiji, kata na mitaa haifanyiki kama inavyotakiwa
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema amebaini kuwa kero nyingi za wananchi hazitatuliwi na viongozi
wa ngazi ya chini kwa sababu mikutano ya vijiji, kata na mitaa imekuwa
haifanyiki kama inavyotakiwa kisheria.
“Azma ya Serikali ya Awamu ya
Tano ni kumtumikia kila Mtanzania popote pale alipo. Lakini nimebaini
baadhi ya kero za wananchi ambazo zingeweza kutatuliwa katika ngazi za
Wilaya, zinaletwa kwenye ofisi za Viongozi wa Kitaifa, au zinasubiri
ziara za viongozi hao.”
Ametoa kauli hiyo leo jioni
(Ijumaa, Februari 10, 2017) bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya
kuahirisha mkutano wa sita wa Bunge la 11.
“Nawasihi viongozi wa Mikoa na
Halmashauri, tembeleeni vijijini na mtatue kero za wananchi huko
vijijini; aidha, hakikisheni mikutano ya vijiji iliyowekwa kwa mujibu wa
sheria inafanyika na maazimio yake yanafika kwenye vikao halali vya
maamuzi. Waheshimiwa Wabunge, ninyi ni sehemu ya Halmashauri zenu,
nawasihi toeni msukumo unaostahili kwa suala hili,” amesisitiza.
Waziri Mkuu amesema suala la
kutotatua kero za wananchi katika ngazi ya Serikali za Mitaa ni kinyume
na dhamira ya Serikali ya kuwatumikia wananchi wote bila ubaguzi ambalo
pia ni kinyume na msimamo wa Ibara ya 146 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Akinukuu ibara hiyo Waziri
Mkuu amesema: “Madhumuni ya kuwapo Serikali za Mitaa ni kupeleka
madaraka kwa wananchi. Na vyombo vya Serikali za Mitaa vitakuwa na haki
na mamlaka ya kushiriki na kuwashirikisha wananchi katika mpango wa
shughuli za utekelezaji wa maendeleo katika Serikali zao na nchi kwa
ujumla.”
Akisisitiza suala hilo, Waziri
Mkuu amesema Sheria ya Serikali za Mitaa inaelekeza kuitishwa kwa
Mikutano Mikuu ya Vijiji kila baada ya miezi mitatu. Sheria pia inatoa
fursa ya kuitishwa kwa mikutano ya dharura, endapo ipo haja ya kufanya
hivyo.
“Kutokana na msimamo huo wa
kisheria na kutokana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano katika
kutatua kero za wananchi, suala la utatuzi wa kero za wananchi
halitakiwi kuendelea kusubiri ziara za viongozi, badala yake, kero hizo
zitatuliwe kwenye ngazi zinazohusika na zitatuliwe kwa wakati,”
amesisitiza.
Amesema watendaji wa kata,
vijiji na mitaa hawana budi kuitisha mikutano ya kisheria ya viijiji na
kata na mitaa na kusoma taarifa za mapato na matumizi ya miradi ya
maendeleo katika maeneo yao. Amewataka viongozi na watendaji katika
ngazi ya Mkoa, Wilaya na Halmashauri wajenge utamaduni wa kuwatembelea
wananchi vijijini na kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili ikiwa
ni pamoja na kuzitafutia ufumbuzi.
“Wakurugenzi wa Halmashauri
nao wanaagizwa kusimamia kikamilifu uitishaji wa mikutano mikuu ya
vijiji na mitaa kwa mujibu wa sheria na kuchukua hatua dhidi ya viongozi
wote watakaoshindwa kutekeleza sharti hilo la kisheria. Tembeleeni
vijiji kusikiliza kero za wananchi,” amesisitiza.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu
amesisitiza haja ya kila kaya kujiwekea akiba ya chakula ili Taifa liwe
na uhakika wa chakula. “Usalama wa chakula unaanzia katika ngazi ya
kaya, kila kaya inatakiwa iwe na utaratibu wa kuwa na chakula cha akiba.
Wakati Serikali inaendelea na wajibu wake wa kuwa na hifadhi ya
chakula, kila mwananchi anao wajibu wa kujiwekea akiba ya chakula cha
kaya yake,” amesisitiza.
Akizungumzia kuhusu
upatikanaji na usambazaji wa mbegu bora za mifugo, Waziri Mkuu amesema
Serikali kupitia mashamba ya mifugo na vituo vya taasisi za Serikali
vilivyoko kwenye maeneo mbalimbali, itaendelea kuhakikisha kuwa mbegu
bora za mifugo zinazalishwa kwa ajili ya uhamilishaji, na mitamba na
madume bora yanazalishwa kwa wingi na kusambazwa ili kukidhi mahitaji ya
wafugaji.
“Ili kukabiliana na changamoto
ya migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi, Serikali
inahimiza wananchi waondokane na mazoea ya uchungaji na kujikita katika
ufugaji wa kisasa ambao utawawezesha kuwa na mifugo michache yenye ubora
ambayo itawaongezea tija katika uzalishaji wa nyama na maziwa mengi
zaidi kwa ng’ombe mmoja.”
Amesema Serikali itaendelea kuimarisha Taasisi zinazoagiza mbegu za mifugo kutoka nje ya nchi kama vile Heifer Project International (HPI) na SAGCOT – Catalytic Trust Fund (CTF)
na kwa kushirikiana na mashamba makubwa ya kisasa ya sekta binafsi ili
wafugaji wawe na wigo mkubwa wa kuchagua aina bora zaidi za mifugo.
Vilevile, amesema Serikali
itaendelea kuboresha na kuendeleza mashamba ya mbegu za malisho ya
mifugo yaliyo chini ya Serikali katika maeneo mbalimbali nchini.
“Nitumie fursa hii kuwaagiza maafisa ugani wa mifugo katika Halmashauri
zote nchini, wafungue mashamba darasa ya kuzalisha mbegu hizo na
kuhamasisha wafugaji kupanda malisho katika maeneo yao na kutoa stadi za
ufugaji bora na wa kisasa. Baada ya miaka mitatu, Wizara husika ifanye
tathmini ya utekelezaji wa agizo hili na kuwasilisha taarifa ofisini
kwangu,” amesema.
Bunge limeahirishwa hadi Aprili 4, 2017.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
- L. P. 980,
DODOMA.
JUMAMOSI, FEBRUARI 11, 2017
No comments :
Post a Comment