Kaimu
Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),
Dk Julieth Magandi akikata utepe kuzindua sehemu ya kuchezea watoto
wanaotibiwa Muhimbili. Dk Magandi amezindua sehemu ya kuchezea watoto
kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa
Tiba Muhimbili, Dk Hedwiga Swai na mwakilishi wa Human Welfare Trust,
Bi. Veena Jog.
Kaimu
Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),
Dk Julieth Magandi akizungumza kabla ya kuzindua sehemu ya watoto
kuchezea. Kushoto ni Ofisa Mkuu Mtendaji wa Benki M, Anil Verma.
Baadhi ya wageni waliofika Muhimbili kushuhudia uzinduzi huo wakimsikiliza mgeni rasmi Dk Magandi.
Baadhi ya watoto, wauguzi, madaktari na wageni wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi Dk Magandi leo.
Mwakilishi kutoka Human Welfare Trust, Bi. Veena Jog akizungumza kabla ya uzinduzi huo.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa hospitali hiyo, Aminiel Aligaesha akishiriki kuimba na watoto hao leo.
Watoto wakicheza baada ya sehemu ya kuchezea kuzinduliwa leo katika hospitali hiyo.
……………
Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto leo imezindua
sehemu ya kuchezea watoto wanaolazwa na wale wanaofika katika Hospitali
ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya kupatiwa matibabu mbalimbali.
Sehemu
ya kuchezea watoto imezinduliwa leo na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za
Upasuaji wa hospitali hiyo, Dk Julieth Magandi kwa niaba ya Katibu Mkuu
wa wizara hiyo, Dk Mpoki Ulisubisya.
Akizindua
sehemu ya kuchezea watoto, Dk Magandi amesema kuwapo kwa sehemu ya
kuchezea kutaongeza chachu ya watoto kuacha kuogopa hospitali kwani
watavutiwa na kutambua kwamba wapo katika mazingira salama na rafiki
wakati wakipatiwa huduma za matibabu.
“Nawapongeza
Hospitali ya Taifa Muhimbili licha ya kufungua sehemu hii ya michezo
leo bado ndani ya jengo mmeweka vivutio vingi kwenye kuta zote za jengo
la watoto ili kuhakikisha watoto wanafurahi,” amesema Dk Magandi.
Dk
Magandi amesema kuwa sehemu hiyo ya michezo ambako pamefungwa vifaa vya
kisasa vya kuchezea itawasaidia watoto wanaokaa muda mrefu hospitalini
kuanzia mwezi mmoja hadi mwaka mmoja kupata faraja.
“Nina imani
kuwa sehemu hii itawapa uhuru wa kucheza kwa nafasi na usalama zaidi
ukilinganisha na hali ilivyokuwa awali. Ni kweli ndani ya jengo kuna
michoro ya wanyama mbalimbali na katuni zinazotoa taswira rafiki kwa
watoto na kuondoa mawazo ya kwamba hospitali ni sehemu ya maumivu muda
wote, lakini kuongezeka kwa sehemu hii ya michezo itachochea zaidi hali
ya watoto kupenda kutibiwa na kujisikia huru zaidi,” amesema.
Pia,
Dk Magandi amewashukuru Human Welfare Trust Fund kwa kujenga sehemu ya
kuchezea watoto kwani wameonyesha wanawajali watoto wetu.
Naye
Mkurugenzi wa Tiba katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dk
Hedwiga Swai akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali
hiyo, Profesa Lawrence Museru amesema kwamba watoto wanaolazwa katika
Jengo la Watoto ni wale wanaohitaji tiba za upasuaji, wenye majeraha ya
moto, utapiamlo, matatizo ya moyo, wenye matatizo ya mishipa ya fahamu,
figo, magonjwa ya tezi na kisukari, magonjwa ya mfumo wa damu, macho na
watoto wanaohitaji ushauri wa lishe bora.
“Sehemu
hii ya michezo itatumika kwa watoto wanaokuja kliniki kwa ajili ya
uchunguzi wa magonjwa mbalimbali, wale wanaofatiliwa maendeleo yao baada
ya kupata nafuu na wale wanaopata ruhusa ya kurudi nyumbani na watoto
waliolazwa wodini,” amesema Dk Swai.
No comments :
Post a Comment