Waziri wa Afya Mahmoud Thabit
Kombo akipata maelezo ya matumizi ya huduma za uzazi wa mpango kutoka
kwa mhamasishaji wa Shirika la Engender Health Joyce Ishengoma
alipotembelea banda la maonyesho wakati wa uzinduzi wa kampeni ya
kuhamasisha huduma hiyo iliyofanyika kijiji cha Mkwajuni Wilaya
Kaskazini A.
Mwakilishi wa Shirika la Engender
Health Dkt. Martha Kisanga akizungumza na wananchi wa Wilaya ya
Kaskazini A wakati wa uzinduzi wa kampeni maalumu ya uhamasishaji wa
uzazi wa mpango katika kijiji cha Mkwajuni.
Wananchi waliojitokeza katika
uzinduzi wa kampeni maalum ya uzazi wa mpango wakifuatilia uzinduzi huo
uliofanyika Mkwajuni Wilaya ya Kaskazini A Unguja.
Baadhi ya watoto walioshiriki
uzinduzi wa kampeni maalum ya kuwahamasisha wazazi wao kujiunga na uzazi
wa mpango wakifuatilia uzinduzi huo uliofanyika kijiji cha Mkwajuni.
Waziri wa Afya Mahmoud Thabit
Kombo akizungumza na wananchi na wageni waalikwa katika uzinduzi wa
kampeni ya uhamasishaji uzazi wa mpango uliofanyika Mkwajuni Wilaya ya
Kasakazi A Unguja.
Picha na Makame Mshenga-Maelezo
……………..
Na Ramadhani Ali/Maelezo
Zaidi ya akinamama 236 kati ya
laki moja wanaofika hospitali na vituo vya afya kujifungua Zanzibar
wanafariki kila mwaka kutokana na sababu mbali mbali zikiwemo kuacha
kutumia huduma za uzazi wa mpango.
Kutokana na tatizo hilo Wizara ya
Afya imeanzisha kampeni maalum ya wiki moja ya kuwahamasisha akina mama
na akinababa kujiunga na uzazi wa mpango katika juhudi za kuokoa maisha
ya wazazi na watoto.
Waziri wa Afya Mahmoud Thabit
Kombo alizindua kampeni hiyo katika kijiji cha Mkwajuni Wilaya ya
Kaskazini ‘A’ na kuwashauri akinababa kuwaruhusu wake zao kujiunga na
uzazi wa mpango .
Alisema hidi sasa wanawake
wanaostahiki kujiunga na uzazi wa mpango Zanzibar ni asilimia 14 tu
waliojiunga na juhudi inatakiwa ifanywe ili iweze kufikia asilimia 20
ifikapo mwaka 2020 ili kulinda afya ya mama na mtoto.
Waziri Mahmoud alisema idadi ya
akinamama wanaofariki ni kubwa zaidi ya takwimu zilizopo kwani
wanaojifungulia hospitali ni asilimia hamsini tu na asilimia iliyobaki
wanajifungulia majumbani na hakuna takwimu zao.
Aliongeza kuwa Serikali imefanya
juhudi kubwa za kusambaza huduma za uzazi wa mpango katika vituo vyote
vya afya mijini na vijijini ili kuwaondoshea usumbufu wananchi hivyo
amewashauri kuvitumia.
Akizungumzia vifo vya watoto chini
ya miaka mitano, Waziri wa Afya alisema bado ni tatizo kubwa Zanzibar
watoto 56 kati ya 1000 wanaozaliwa wakiwa hao hufariki dunia.
Alisema sababu kubwa ya vifo hivyo
inatokana na wazazi kucheleweshwa kupelekwa hospitali ama kutopelekwa
kabisa na kupelekea kujifungua katika mazingira yasiyo salama.
Kutokana na matatizo mengi
yanayowapata akinamama wajawazito na watoto wakati wa kujifungua na
baada ya kujifungua, Waziri Mahmoud Thabit Kombo ameagiza kuundwa Kamati
ya kitaifa itakayowashirikisha viongozi kutoka kada mbali mbali na
washirika wa maendeleo kukabiliana nalo.
Mwakilishi wa Shirika la Engender
Health Dkt. Martha Kisanga alisema ushiriki mdogo wa akinababa katika
huduma ya uzazi wa mpango unachangia wanawake wengi kutojiunga na huduma
hizo.
Katika risala ya wananchi wa
Wilaya Kaskazini A iliyosomwa na Tatu Khamis Kombo walisema pamoja na
vituo vingi vya afya kutoa huduma za uzazi wa mpango, mwamko bado ni
mdogo na kufanyika kwa kampeni hiyo katika wilaya yao itasaidia wananchi
wengi kujiunga.
Wilaya Kaskazini A na Wilaya ya
Micheweni Pemba ndizo zenye asilimia ndogo zaidi ya akinamama
waliojiunga na huduma ya uzazi wa mpango Zanzibar.
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR
No comments :
Post a Comment