Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kwamba vita inayopiganwa
sasa dhidi ya uagizaji, uzalishaji, usambazaji na matumizi ya dawa ya
kulevya ni kubwa na kila Mtanzania anapaswa kuunga mkono jitihada hizo.
Kassim Majaliwa ametoa kauli hiyo
leo Bungeni, Mjini Dodoma katika hotuba yake ya kuahirisha mkutano wa
sita wa Bunge la Kumi na Moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Moja ya eneo lililojadiliwa na
kuibua hisia kali ni kuhusu vita inayoendelea nchini dhidi ya dawa za
kulevya. Watanzania wote ni mashahidi kwamba vijana wetu wengi
wameendelea kudhoofisha afya zao kutokana na matumizi ya madawa ya
kulevya. Dawa za kulevya ni hatari kwa usalama na ustawi wa Taifa,”
alifafanua Waziri Mkuu.
Aliendelea kwa kusema kuwa
kitaalamu madhara ya kiafya yanayosababishwa na matumizi ya dawa za
kulevya ni pamoja na kuathirika kwa mfumo wa fahamu kwa mtumiaji ikiwemo
kuchanganyikiwa, kuwa na ulevi usioponyeka kirahisi na kusababisha vifo
ikiwa mtumiaji atazidisha matumizi ya dawa hizo.
Aidha Waziri Mkuu amesema kuwa
madhara ya kiuchumi yanayosababishwa na magonjwa hayo ni pamoja na
kuwatibu waathirika wa dawa za kulevya, gharama kubwa za uchunguzi wa
kimaabara kwenye maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na watumiaji
wa dawa za kulevya kushindwa kujisimamia na kuendesha maisha yao.
Amesema kuwa madawa hayo huingia
nchini kwa kutumia bandari bubu kupitia Bahari ya Hindi na kwa njia ya
magari binafsi kupitia mipaka ya nchi ya Kenya, Uganda na mpaka wa
Tunduma.
Kassim Majaliwa amesema kuwa
lengo la Serikali ni kuwasaidia walioathirika na dawa hizo na
kuwachukulia hatua kali wale waliowaathiri kwa maana ya wauzaji na
wasambazaji.
Amewashukuru wabunge kwa kutoa
mchango mkubwa na ushauri wa namna nzuri zaidi ya kupambana na janga
hilo ikiwa dhamira ya Serikali ni kupambana na janga hilo kwa dhati bila
kumuonea mtu yeyote na kwa kuzingatia misingi ya sheria na haki.
Kassim Majaliwa ametoa takwimu ya
Watanzania ambao wamefungwa katika magereza mbalimbali nje ya Tanzania,
ikiwa ni pamoja na Watanzania 200 ambao wamefungwa China, Watanzania 12
nchini brazil, Watanzania 63 nchini Iran, Watanzania 7 nchini Ethiopia
na Watanzania 296 ambao wamefungwa Afrika ya Kusini.
No comments :
Post a Comment