Tuesday, February 14, 2017

VITA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA, 80 WATIWA NGUVUNI ARUSHA


ARUSHA POLISI
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo akionyesha baadhi ya kete za Heroin ambazo zilikamatwa hivi karibuni kutokana na misako inayoenndelea mkoani hapa. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha).
…………
 
 
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
 
Wiki chache baada ya Jeshi la Polisi mkoani hapa kukamata gunia 58 za bhangi ambazo ziliteketezwa kwa moto  na kuharibu hekari 31 za mimea ya zao hilo katika maeneo ya Kismiri Juu na Engalaon wilayani Arumeru, Jeshi hilo limeendelea na misako dhidi ya wauzaji, watumiaji na wasafirishaji  wa dawa za kulevya na kufanikiwa kuwakata watuhumiwa 80 katika misako iliyofanyika kwa muda  wa siku 4 tu.
 
Akitoa taarifa hiyo leo asubuhi ofisini kwake mbele ya  waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo  alisema kwamba misako hiyo imefanikisha kukamata jumla ya kete 167 za madawa ya kulevya aina ya Heroin pia misokoto 3,845 ya Bhangi na mirungi kilogramu 33.
 
“Katika misako hiyo ambayo ilifanyika wilaya zote sita za mkoa huu, watuhumiwa 54 walipatikana kwenye tuhuma za Bhangi, 14 ni tuhuma za Heroin na 12 ni wa tuhuma za mirungi.” Alisema Kamanda Mkumbo.
 
“watuhumiwa 40 ni wauzaji wa madawa hayo huku 13 ni wale ambao walikuwa wanajihusisha kwa namna moja au nyingine na Bhangi na mmoja alikuwa anasafirisha, watuhumiwa 14 wa Heroin kosa lao kupatikana huku 12 makosa yao ni kupatikana na mirungi na hivyo kufanya idadi yao kuwa 80 ambao ni wanaume na wanawake”. Alifafanua Kamanda Mkumbo.
 
Kamanda wa Polisi aliwashukuru wananchi wa mkoa huu kwa ushirikiano wa utoaji wa taarifa za uhalifu na kuwaomba waendelee kufanya hivyo na kutoa onyo kwa wale wachache wanaojihusisha na uhalifu wa namna hiyo waache mara moja vinginevyo watakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

No comments :

Post a Comment