Na Judith Mhina – MAELEZO
Shirika la Kimataifa la Elimu
Sayansi na Utamaduni UNESCO Tanzania limeadhimia kuwajengea uwezo wa
Waandishi wa Habari nchini ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na
kwa kufuata Sheria Kanuni na taratibu zinazosimamia taaluma yao.
Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu
Mtendaji wa UNESCO Taifa Dkt. Moshi Kimizi katika uzinduzi wa Kamati ya
Kimataifa ya Mpango wa Maendeleo ya Mawasiliano – IPDC iliyokutana Magogoni Jijini Dar-es-hivi karibuni.
Akizindua Kamati hiyo Dkt Kimizi
alisema, Kamati ya Kimataifa ya Mpango wa Maendeleo ya Mawasiliano,
inajukumu kubwa la kuelimisha, kuleta mageuzi na maendeleo katika
mawasiliano.
Shirika hilo limedhamiria
kuwajengea wanahabari uwezo katika nyanja za uhuru wa
upatikanaji wa
habari bila vikwazo, pia kuwawezesha Waandishi wa Habari, kumudu
majukumu yao na kuhakikisha haki ya mwanahabari ya kufanya kazi yake kwa
weledi bila kubughudhiwa inaenziwa.
Kamati ya kitaifa ya mpango wa
mawasiliano inaundwa na wajumbe saba ikiongozwa na Mwenyekiti Dkt. Eva
Solomon Msangi, Mhadhiri kutoka Shule Kuu ya Mawasiliano ya Chuo Kikuu
cha Dar-Es-Salaam, na wengine wane ambao ni, mjumbe mmoja kutoka Wizara
za Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,
Wadau muhimu wa Habari kutoka Baraza la Habari Tanzania – MCT na Media Institute of Southern Africa – Tanzania -MISA TAN pamoja na Wawakilishi wawili kutoka UNESCO.
Dkt Kimizi aliwajulisha wajumbe
kuwa wanajukumu la kuhakikisha sauti za walio pembezoni au
waliosahaulika zinasikika ,hivyo, Kamati inapopanga mipango yake iweke
kipaumbele kwa kutenga rasilimali kwa ajili ya kuwajengea uwezo, pamoja
na kuwaimarisha ili waweze kutoa habari na kupata habari bila vikwazo.
Akitoa taarifa ya Kikao cha Paris Ufaransa kwa kamati hiyo ya IPDC
Dkt Eva Msangi alisema kikao kilisisitiza juu ya usalama, ulinzi dhidi
ya Waandishi wa Habari uimarishwe na kuzingatiwa, kwa kuwa Waandishi
wengi duniani wako katika hatari ya kuteswa au kuuwawa wakati
wakitekeleza wajibu wao.
Dkt Msangi aliongeza kuwa baraza
la Maendeleo la Mawasiliano la Dunia lilipendekeza na kuchagua
mwenyekiti ambapo Bi Albana Shala kutoka Netherlands alichaguliwa
kuendelea kwa kipindi kingine cha miaka minne. Katika kuweka uwiano
wakijiografia wa Baraza, washirika wote wa UNESCO huwekwa katika makundi ya kikanda au kijiografia.
Makundi hayo sita ya kijiografia
ni Ulaya ya Magharibi na Mataifa ya Amerika ya Kaskazini, kundi la pili
Mataifa ya Ulaya Mashariki, kundi la tatu ni Mataifa ya Latin Amerika na
Karibiani, kundi la nne ni Asia na Mataifa ya Pasifiki na
kundi la tano ni Mataifa ya Afrika kipengele (a) na tano (b) ni Mataifa
ya Kiarabu.
Tanzania ipo katika kundi la 5 (a), ambalo lipo chini ya uenyekiti wa Zambia. Pamoja na kwamba UNESCO katika
Maendeleo ya Mawasiliano Kimataifa, imejikita katika masuala ya ulinzi
na usalama wa Waandishi wa Habari lakini nchi husika inaweza Kuandaa
miradi mingine ambayo inahusiana na maendeleo ya Waandishi naVyombo vya
Habari.
Majukumu mengine ni kuwa na
majukwaa ya kuchambua na kuelimishana il ikuwajengea uwezo kutoka ngazi
ya chini na kwa wale wasio na sauti katika jamii. Kupanga mipango
mbalimbali na kuridhia matumizi ya rasilimali fedha na kuitekeleza, Kuwa
daraja kati ya wanataaluma wa Habari na Wadau wa habari.
Naye Mratibu wa Kamati ya Kimataifa ya Maendeleo ya Mawasiliano kutoka Tume ya Taifa UNESCO
Tanzania Bi Christina Musaroche alisema ilikupanua wigo na idadi ya
wajumbe kamati ina mpango wa kuongeza wajumbe wawili kutoka Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar yaani Wizara ya Habari, Utamaduni na Utalii na
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA.
Alisema mwakilishi kutoka Zanzibar
ni muhimu katika kufanya kamati kuwa ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na mwakilishi kutoka TCRA kwa ajili ya utambuzi wa sheria
za mitandaoni sekta ya masiliano kwa ujumla.
Mwisho
No comments :
Post a Comment