Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akisalimiana na Makamu Mwenyekiti
wa Kampuni ya Yapi Merkezi, Bw. Erdem Arioglu kabla ya zoezi la utiliaji
saini wa Mkataba wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli ya Kisasa
(Standard Gauge). Wa pili kutoka kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo
Sekta ya Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuriho.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi
Miliki ya Rasilimali za Reli (RAHCO), Masanja Kadogosa (wa tatu kutoka
kulia waliokaa), akisaini Mkataba wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli
ya Kisasa (Standard Gauge) na wawakilishi wa Makampuni yatakayojenga
reli hiyo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi
Miliki ya Rasilimali za Reli (RAHCO), Masanja Kadogosa (wa tatu kutoka
kulia), akibadilishana Mkataba wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli ya
Kisasa (Standard Gauge), na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mota-Engil
Africa, Bw. Manuel Antonio Mota, mara baada ya kusaini mkataba huo
jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (wa tatu kutoka kulia), akiwa katika
picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali na Wakurugenzi wa
Makampuni yatakayojenga reli hiyo jijini Dar es Salaam mara baada ya
kusaini mkataba wa kuanza awamu ya kwanza ya ujenzi huo.
Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
…………….
Serikali imetiliana saini ya
makubaliano ya ujenzi wa sehemu ya kipande cha reli ya kisasa (Standard
Gauge), chenye urefu wa KM 300 kati ya mkoa wa Dar es Salaam na Morogoro
ambao ujenzi wake unatarajiwa kuanza baada ya mwezi mmoja na nusu
kutoka sasa.
Kampuni zilizotiliana saini makubaliano hayo na Serikali ni ya ubia kati ya YAPI MERKEZI ya uturuki na MOTA-ENGIL AFRIKA ya ureno kwa grahama ya dola zaidi ya bilioni moja za kimarekani.
Akishuhudia utiliaji saini
uliofanyika jijini Dar es Salaam, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema ujenzi wa reli hiyo
itayotumia umeme na kwenda kwa spidi ya kilometa 160 kwa saa itakuwa ni
ya kwanza kwa Afrika ikifuatiwa na nchi ya Morocco.
“Tunataka kuifanya nchi yetu iwe
ndogo kwa kutumia miundombinu ya kisasa ndio maana Serikali imeamua
kujenga reli hii itakayotumia umeme na kwenda spidi kubwa kuliko
nyingine zote barani Afrika”, amesema Prof. Mbarawa.
Ameongeza kuwa ujenzi wa reli hiyo
utaongeza chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi na
kubainisha kuwa Safari ya Dar hadi Moro itatumia muda wa saa 1:16 wakati
Dar hadi Dodoma itatumia muda wa saa 2:30 na safari ya Dar had Mwanza
itatumia muda wa saa 7:30.
Aidha, Prof. Mbarawa amesisitiza
kuwa gharama za ujenzi wa reli hiyo haitakuwa sawa na mikoa mingine
kutokana na kutofautiana na hali ya jiografiia kwenye mikoa ambapo reli
hiyo itapita.
Kuhusu kukamilisha mradi huu,
Waziri Prof. Mbarawa ameahidi kuongeza bajeti ya ujenzi wa reli hiyo kwa
mwaka ujao wa fedha na kuendelea kutafuta mkopo wa gharama nafuu ili
kufanikisha ukamilishawaji wake.
Waziri Prof. Mbarawa amewataka
wadau kujitokeza kwa wingi kuomba zabuni zIlizotangazwa hivi karibuni za
ujenzi wa reli hiyo kwa awamu nyingine kutoka Morogoro-Makotopora KM
336, Makotopora-Tabora KM 294, Tabora-Isaka KM 133 na Isaka hadi Mwanza
KM 248 ambazo zinatarajiwa kufunguliwa mwezi Aprili mwaka huu na kuahidi
kuwa utaratibu wake utatendeka kwa uwazi na haki.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa
Kampuni Hodhi Miliki ya Rasilimali za Reli (RAHCO), Masanja Kadogosa
amesema kuwa ujenzi wa reli hiyo utajengwa kwa muda wa miezi 30 kutokea
sasa na kuhusisha ujenzi wa miundombinu ya umeme, Stesheni sita za
abiria na sita za kupishani treni na ujenzi wa wigo wa KM 102 kwa
usalama wa watu na magari.
Kwa upande wake Balozi wa Uturuki
nchini Mhe. Yassemin Eralp ameiahidi kuendeleza ushirikiano na Serikali
katika mradi huo mkubwa na kuupongeza uongozi wa Serikali ya Awamu ya
Tano katika kufanikisha maendeleo kwa wananchi wake.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments :
Post a Comment