* Waziri Mkuu asema Serikali haitamuonea mtu yeyote
*Aomba Watanzania wote waunge mkono juhudi za Serikali
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali itapambana na janga la dawa za kulevya na kwa dhati
bila kumuonea mtu yeyote na kwa kuzingatia misingi ya sheria na haki.
Ametoa kauli hiyo leo jioni
(Ijumaa, Februari 10, 2017) bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya
kuahirisha mkutano wa sita wa Bunge la 11.
“Lengo la Serikali ni kuwasaidia
walioathirika na dawa za kulevya na kuwachukulia hatua kali wale
waliowaathiri kwa maana ya wauzaji na wasambazaji. Dhamira ya Serikali
ni kupambana na janga hili kwa dhahiri na kwa dhati bila kumuonea mtu
yeyote na kwa kuzingatia misingi ya sheria na haki,” amesema.
Akizungumzia idadi ya watu ambao
hadi sasa wamekwishakamatwa katika nchi mbalimbali, Waziri Mkuu amesema
takwimu za jumla zinaonyesha kuwa Watanzania 515 wamekamatwa na kufungwa
gerezani kwa makosa ya kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya.
“Nchini China Watanzania walioko
magerezani ni zaidi ya 200; Brazili kuna Watanzania 12; Iran wako
Watanzania 63; Ethiopia Watanzania saba na Afrika Kusini wako Watanzania
296,” amesema.
Waziri Mkuu amesema moja ya hoja
za Kamati za Kudumu za Bunge iliyojadiliwa na kuibua hisia kali katika
mkutano huu wa Bunge ni kuhusu vita inayoendelea nchini dhidi ya dawa za
kulevya na akawaomba Watanzania wote waiunge mkono Serikali juu ya vita
hiyo.
“Watanzania wote ni mashahidi
kwamba vijana wetu wengi wameendelea kudhoofika kiafya kutokana na
matumizi ya dawa za kulevya. Dawa za kulevya ni hatari sana kwa usalama
na ustawi wa Taifa letu. Vita hii inayopiganwa sasa dhidi ya uagizaji,
uzalishaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya ni kubwa. Sote
tunapaswa kuunga mkono jitihada hizo,” amesisitiza.
Amesema dawa hizo za kulevya,
huingia zaidi kutumia njia za bandari bubu kupitia Bahari ya Hindi na
mipakani kwa njia ya magari binafsi au mabasi kupitia nchi za Kenya,
Uganda na Mpaka wa Tunduma.
Ameyataja madhara ya kiafya
yanayosababishwa na matumizi ya dawa za kulevya ni pamoja na kuathirika
kwa mfumo wa fahamu kwa mtumiaji ikiwamo kuchanganyikiwa, kuwa na ulevi
usioponyeka kirahisi na kusababisha kifo kama mtumiaji atazidisha
matumizi ya dawa za kulevya. “Madhara ya kiuchumi ni pamoja na gharama
kubwa za kuwatibu waathirika wa dawa za kulevya, gharama kubwa za
uchunguzi wa kimaabara kwenye Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na
watumiaji wa dawa za kulevya kushindwa kujisimamia na kuendesha maisha
yao,” ameongeza.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu ameziagiza Halmashauri zote nchini zifanye maoteo na kuyawasilisha
Bohari Kuu ya Dawa kabla au ifikapo tarehe 05 Machi 2017 ili kutekeleza
azma ya Serikali ya kusambaza dawa kwa wakati.
“Dhamira ya Serikali ya kusambaza
dawa kwa wakati kwenye Halmashauri zetu haitafanikiwa endapo
Halmashauri zitachelewa kuwasilisha maoteo ya dawa, vifaa tiba na
vitendanishi. naomba kutoa rai kwa Waheshimiwa Wabunge, mpate wasaa wa
kufuatilia mchanganuo wa usambazaji dawa katika Halmashauri zenu ambao
hutolewa na Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto,” amesema.
Amesema hali ya upatikanaji wa
dawa nchini inaendelea kuimarika huku akitolea mfano kiasi cha sh.
bilioni 91 ambacho kimeshatolewa, kati ya sh. bilioni 251 zilizotengwa
sawa na wastani wa sh. bilioni 20 kwa mwezi.
Ili kuboresha upatikanaji wa dawa
na vifaatiba nchini, Waziri Mkuu amesema Serikali imeamua kununua
madawa na vifaa tiba moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji badala ya
mawakala.
“Napenda kuliarifu Bunge lako
tukufu kwamba, utaratibu huo umeanza na tayari Serikali imekamilisha
taratibu za kimkataba na wazalishaji watano wakubwa wa ndani ambao
watanunua baadhi ya dawa kutoka ndani ya nchi, wakati mikataba mingine
76 ya wazalishaji wa nje iko katika hatua za mwisho. Matarajio yetu ni
kwamba, utekelezaji wa mikataba ya nje utaanza katika mwaka wa fedha
2017/18,” amesema.
Amesema kutokana na uamuzi huo wa
Serikali pamoja na jitihada za Serikali za kuongeza bajeti ya ununuzi
wa dawa, Bohari ya Dawa imeweza kununua aina 105 za dawa muhimu sawa na
asilimia 78 ya aina 135 ya dawa muhimu zinazohitajika nchini.
“Shabaha yetu ni kwamba, ifikapo
Juni, 2017 usambazaji wa dawa muhimu nchini kote uwe umefikia asilimia
85. Taarifa hiyo imetolewa kwa kila Mheshimiwa Mbunge ili aweze
kufuatilia kwa karibu dawa na vifaatiba vinavyoletwa na Serikali kwenye
Halmashauri zenu,” amesema.
Bunge limeahirishwa hadi Jumanne, Aprili 4, 2017.
No comments :
Post a Comment