Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amewashukuru Mabalozi na
Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa kwa ushirikiano na mchango wao kwa
Serikali ya Tanzania ambao umesaidia kufikia malengo ya Serikali kwa
mwaka uliopita wa 2016. Rais Magufuli aliwasihi Waheshimiwa Mabalozi
waendelee kuisaidia Serikali ili kufikia malengo iliyojiwekea kwa mwaka
2017.
Mhe. Rais Magufuli ametoa
shukrani hizo leo wakati wa hafla ya kuukaribisha mwaka mpya (Diplomatic
Sherry Party) iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam kati yake, Mabalozi na
Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa yaliyopo nchini.
Katika hotuba yake, Mhe. Rais
Magufuli alisema kuwa mwaka 2016 ambao ulikuwa mwaka wake wa kwanza
tangu achaguliwe kuwa Rais wa Awamu ya Tano umekuwa wa mafanikio makubwa
ambapo nchi imendelea kudumisha amani, mshikamano, umoja na Muungano
umeimarika. Aidha katika mwaka huo, Serikali imeongeza jitihada za
kuimarisha demokrasia, kupiga vita rushwa, ujangili na ufisadi.
Mhe. Rais Magufuli aliongeza
kusema kuwa, Serikali ya Tanzania imefanikiwa kiuchumi na kuwa nchi ya
pili yenye uchumi unaokua kwa kasi barani Afrika ikitanguliwa na Ivory
Coast. Uchumi wa Tanzania ulitarajiwa kukua kwa asilimia 7.2 mwaka jana
kutoka asilimia 7.0 mwaka uliotangulia. Pia kiwango cha mfumuko wa bei
kilipungua kutoka asilimia 6.5 mwezi Januari 2016 hadi kufikia asilimia
2.5 mwezi Oktoba mwaka huohuo.
Akizungumzia suala la ukusanyaji
mapato, Mhe. Rais Magufuli alisema kwamba Serikali inasimamia kikamilifu
suala hilo ambapo kwa sasa kiwango cha ukusanyaji wa mapato
kimeongezeka kutoka shilingi bilioni 850 hadi kufikia shilingi trilioni
1.2 kwa mwezi.
Kuhusu mpango wa maendeleo wa
miaka mitano 2016/2021, Rais Magufuli aliwaeleza Mabalozi hao kuwa,
mpango huu unalenga kujenga Uchumi wa Viwanda ili kuiwezesha Tanzania
kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kama Dira ya Maendeleo ya
Taifa inavyoelekeza.
Alieleza kuwa katika kutekeleza
Mpango huo kiasi cha shilingi Trilioni 107 kinahitajika na kati ya hizo
Serikali itatoa shilingi trilioni 59 ambazo ni wastani wa shilingi
trilioni 11.8 kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Utekelezaji
wa mpango huo umeshaanza ambapo Serikali katika Bajeti yake ya mwaka
2016 imetenga kiasi cha shilingi trilioni 29.5 ambazo ni sawa na
asilimia 40 ya Bajeti ya Serikali kwa ajili ya Bajeti ya Maendeleo.
Kiwango hicho ni cha juu zaidi kuwahi kutengwa kwenye bajeti ya
maendeleo katika historia ya Tanzania.
Fedha hizo zimeelekezwa kwenye
ujenzi wa miundombinu wezeshi kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda kama
vile nishati, barabara, reli na maji. Aliongeza kusema kuwa Kati ya
fedha hizo shilingi trilioni 5.5 zimetengwa kwa ajili ya miundombinu ya
usafirishaji na shilingi trilioni 1.2 zimetengwa kwa ajili ya nishati ya
umeme. “Hii imetuwezesha kuendelea au kuanza utekelezaji wa miradi
mikubwa ya usafiri ikiwemo reli, barabara, anga, maji pamoja na miradi
ya umeme. Tuliweza pia kununua ndege mpya sita ambazo bila shaka
zitasaidia kukuza sekta ya utalii nchini”
Kwa muktadha huo, Rais Magufuli
aliwaomba Mabalozi kushawishi wawekezaji kuja kuwekeza katika ujenzi wa
Reli wa kiwango cha kimataifa kutoka Dar Es Salaam hadi Mwanza na Kigoma
na kuunganisha hadi nchi za Burundi, DRC na Rwanda. Serikali kwa
kutumia fedha zake za ndani itaanza kujenga kilomita 300 kuanzia Dar Es
Salaam hadi Morogoro.
Vile vile, Serikali imeweka
kipaumbele kwenye kuboresha huduma za jamii ikiwemo sekta ya elimu
iliyotengewa trilioni 4.8 na sekta ya afya kiasi cha trilioni 1.9.
Kupitia mpango huu wa kuboresha sekta ya elimu, kiwango cha udahili kwa
watoto wanaojiunga na darasa la kwanza na kidato cha kwanza na wale
wanaopokea ufadhili wa masomo ya juu kimeongezeka mara dufu
ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Akizungumzia masuala ya
Diplomasia, Mhe. Rais Magufuli aliwaeleza Mabalozi na Wawakilishi hao wa
Mashirika ya Kimatifa kuwa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania
na nchi ningine yameimarika ambapo Viongozi Wakuu kutoka nchi
mbalimbali wamefanya ziara nchini Tanzania. Aidha, yeye binafsi, Makamu
wa Rais, Waziri Mkuu na Viongozi wengine Serikalini wamefanya ziara za
kuimarisha ushirikiano kwenye nchi mbalimbali. Katika ziara hizo,
Tanzania imesaini mikataba mbalimbali ya ushirikiano. Mhe. Rais aliahidi
kuwa Tanzania itaendelea kuwa mwanachama mwaminifu kwenye Mashirika ya
Kimataifa na Kikanda ikiwemo Umoja wa Afrika (AU), Umoja wa Mataifa
(UN), Jumuiya ya Madola, Jumuiya ya Afrika Mashariki na mengine.
“Tunawashukuru sana Mabalozi na
Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa na Kikanda kwa kazi nzuri
mnayoifanya hapa nchini kwetu. Mafanikio yote haya niliyoainisha
yamewezeshwa na ushirikiano wenu na naahidi Serikali itaendelea kutoa
ushirikiano kwenu ili muweze kufanya kazi zenu vizuri” alisema Rais
Magufuli.
Vilevile aliwaomba Mabalozi hao
kuendelea kushirikiana na Tanzania ili kuiwezesha kufikia malengo yake
na aliwakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza nchini na kutumia fursa za
malighafi, nguvukazi na soko kubwa lililopo nchini.
Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli
alianisha changamoto zinazochangia kukwamisha jitihada mbalimbali za
Serikali ikiwa ni pamoja na Mabadiliko ya Tabianchi na kuiomba Jumuiya
ya Kimataifa kushirikiana katika kukabiliana na changamoto hii ili
kuziwezesha jamii zetu kufikia maendeleo na ustawi. Pia kupitia Mabalozi
hao alizipongeza nchi zilizoridhia Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko
ya Tabianchi na kueleza kuwa Tanzania imeanza mchakato wa kuridhia
Mkataba huo tangu mwezi Aprili, 2016.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rais
aliwaeleza rasmi Mabalozi hao azma ya Serikali ya kuhamishia Makao Makuu
mjini Dodoma katika kipindi cha miaka mitano ya utawala wake na
kuwaomba Mabalozi hao nao waanze mchakato wa kuhamia Dodoma.
“Mwaka jana wakati nakabidhiwa
uenyekiti wa Chama cha Mapinduzi niliahidi ndani ya miaka mitano
Serikali itahamia Dodoma. Tayari Waziri Mkuu na baadhi ya Wizara zipo
Dodoma. Nawaomba Mabalozi nanyi muanze kufikiria kuhamia Dodoma kwani
Serikali imekwishatenga viwanja kwa ajili yenu, alisisitiza Rais
Magufuli.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa
Mabalozi ambaye pia ni Balozi wa Zimbabwe hapa nchini, Mhe. Edzai
Chimonyo alisema kuwa anaipongeza Serikali ya Tanzania chini ya uongozi
wa Rais Magufuli kwa hatua kubwa ya maendeleo iliyopiga katika kipindi
cha mwaka mmoja wa utawala wake. Alisema kuwa katika kipindi hiki
wameshuhudia uchumi ukikua, nidhamu katika utumishi wa umma, ukusanyaji
wa mapato kuongezeka, na kiwango cha mfumuko wa bei kupungua.
Aidha, aliongeza kuwa wanaunga
mkono mpango wa Serikali wa kujenga miundombinu wezeshi ikiwemo Reli kwa
vile kutawezesha kukuza biashara na nchi jirani na mataifa mengine kwa
ujumla. Pia alipongeza jitihada za Serikali katika kukuza ushirikiano na
Sekta Binafsi ambayo ina mchango mkubwa kwenye maendeleo na kupongeza
juhudi za Tanzania kwenye usuluhishi wa migogoro kwenye Ukanda wa Maziwa
Makuu na kuitaja Tanzania kuwa ni Kisiwa cha Amani.
Kuhusu Mabalozi kuhamia Dodoma,
Balozi Chimonyo alisema Jumuiya ya Mabalozi inaunga mkono wazo hilo na
wapo tayari kuhamia Dodoma kama ilivyopangwa.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 10 Februari, 2017
No comments :
Post a Comment