Saturday, February 4, 2017

Serikali Yaahidi Kufanyia Kazi Mapungufu Yaliyojitokeza Mradi wa TASAF

ANGEL
Na: Lilian Lundo – MAELEZO – DOdoma
Serikali imesema kwamba itafanya uchunguzi juu ya changamoto na matatizo ambayo yamejitokeza katika mradi wa TASAF ili kuja na mfumo mwingine bora zaidi kwa ajili ya wanufaika wa mradi huo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki ameyasema hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa mwaka 2016/2017 ambapo wabunge waliulalamikia mradi huo kuwa na matatizo katika maeneo ambayo wanayasimamia.
Angellah Kairuki alisema kuwa wizara yake itafuatilia changamato zote ambazo wabunge wamezianisha ikiwemo utoaji wa fedha kwa kaya ambazo hazina sifa, matumizi mabaya ya fedha za mradi kwa baadhi ya wanufaika pamoja na usimamizi mbovu wa fedha za mradi kwa watendaji wa Halmashauri.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Nzega Hussein Bashe ameishauri Serikali kutafuta mfumo mzuri wa kuzitoa fedha hizo ili wanufaika waweze kuzitumia kwa kuanzisha biashara ndogondoga ambazo zitawasaidia kujikimu na kuziendeleza familia zao kiuchumi.
Aliendelea kwa kusema kuwa, kuwe na utaratibu wa wanufaika kutoa mchanganuo wa namna walivyozitumia fedha hizo ili kuleta nidhamu kwa wanufaika wanaotumia fedha hizo kinyume na malengo yaliyowekwa.
Aidha, Mbunge wa Jimbo la Nanyamba, Abdallah Chikota amesema kuwa katika jimbo lake kuna kaya ambazo zimetolewa katika mradi huo kwa kukosa sifa. Kaya hizo zimeagizwa kurejesha fedha zote ambazo walipatiwa kupitia mradhi huo, na wengi wao hawana uwezo wa kurejesha fedha hizo.
Hivyo basi, ameiomba Serikali kuwachukulia hatua Waratibu wa Mradi huo kwani ndio waliotoa fedha kwa watu wasio na sifa,  badala ya kuwaambia wananchi kurejesha fedha walizopewa  kwani wengi wao hawana huwezo wa kuzirejesha kutokana na vipato vyao kwa vya chini.
Akiwasilisha taarifa ya Kamati hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. Pudenciana Kikwembe amesema kuwa, mpango wa TASAF wa kunusuru kaya maskini nchini umeonyesha mafanikio makubwa, licha ya kasoro kadhaa zinazotokana na baadhi ya Watendaji wa Halmashauri wanaohusika kukosa uwazi na uadilifu katika uwajibikaji wao.
Hivyo basi, hali hiyo imesababisha kubainika kwa Kaya 55, 692 zisizo na sifa stahiki  lakini zilikuwa zikinufaika na mpango hu o wa kunusuru Kaya Masikini.
Aidha Kamati imeishauri serikali kuimarisha uwezo wa Halmashauri katika kusimamia miradi ya TASAF ili itekelezwe kikamilifu na kwa ufanisi pamoja na kuimarisha mifumo ya kuwatambua walengwa wa Mpango huo na kuzuia kaya zisizo na sifa kunufaika

No comments :

Post a Comment