Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa
na Michezo Mhe.Nape Moses Nnauye ametuma salamu za pongezi kwa Timu ya
Taifa ya Mpira wa Miguu kwa vijana wenye chini ya umri wa miaka 17
(Serengeti Boys) kwa kufuzu Fainali za Mashindano ya Africa kwa vijana
chini ya umri wa miaka 17.
Kwa mujibu wa taarifa
iliyotolewa na Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa miguu barani
Afrika (CAF) imeeleza kuwa Serengeti Boys inafuzu fainali hizo mara
baada ya kushinda kwa rufaa yao dhidi ya Timu ya Congo Brazaville ambapo
timu hiyo ilimchezesha mchezaji Langa Lese aliyezidi umri wa miaka 17.
Mhe. Nape amesema kuwa, hiyo
ni fursa kubwa ambayo Tanzania imeipata katika mashindano ya kimataifa
na kuna kila uwezo na sababu ya kushinda na kuchukua kombe hilo.
Waziri Nape ametoa shukrani
zake za dhati kwa watanzania na wadau wa michezo kwa michango yao ya
hali na mali iliyoifanya Serengeti Boys kufikia hapa ilipofika na kuzidi
kuendelea kuiunga mkono kwa hali na mali timu hiyo katika kuelekea
fainali hizo.
Mhe. Nape Moses Nnauye
amewatakia mafanikio Serengeti Boys kuelekea katika Fainali za michuano
ya AFCON zitakazofanyika nchini Gabon Aprili, 2017.
Imetolewa na:
Zawadi Msalla
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo.
03/02/2017
No comments :
Post a Comment