Mkuu wa Chuo cha Maji Dkt.Shija
Kazumba akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu
mkakati wa Chuo kuhakikisha Tanzania inakuwa na Mafundi Sanifu wa
kutosha katika sekta ya maji ili kuendana na kasi ya Serikali kufikisha
huduma ya maji kwa wananchi wote. Kulia ni Afisa Habari na Masoko wa
chuo hicho Bw. George Karumuna.
.Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano wa Chuo cha Maji na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
(Picha na MAELEZO)
………………………………………………………………..
Fatma Salum-MAELEZO
Serikali imedhamiria kuzalisha
wataalamu wa maji wa kutosha kukidhi mahitaji ya sasa na kuwafikishia
wananchi wote maji safi na salama kupitia miradi mbalimbali
inayotekelezwa
kote nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini
Dar es Salaam na Mkuu wa Chuo cha Maji cha Dar es Salaam Dkt. Shija
Kazumba wakati wa mkutano na vyombo vya habari uliolenga kueleza
mikakati ya chuo hicho ya kuzalisha wataalamu wenye sifa na weledi.
“Wanafunzi waliopo sasa ni 1849,
kati yao 489 ni wanawake na dhamira yetu ni kuhakikisha kuwa kuna
mafundi sanifu wa kutosha kulingana na mahitaji ya sasa na ukuaji wa
sekta ya maji”alisisitiza Dkt. Kazumba.
Alifafanua kuwa chuo hicho
kimeanzisha mfuko maalum kwa ajili ya kuwainua wanafunzi wa kike ili
wajiunge katika masomo ya uhandisi wa maji, mafundi sanifu, upimaji wa
ubora wa maji, umwagiliaji na hali ya hewa lengo likiwa ni kuchochea
ukuaji wa sekta hiyo.
“Dhamira ya kuwainua wanafunzi wa
kike inaonyesha nia ya Serikali kuwawezesha wanawake kushiriki
kikamilifu katika kukuza na kuendeleza sekta mbalimbali hapa nchini
ikiwemo sekta ya maji”. Aliongeza Dkt. Kazumba
Pia alibainisha kuwa Serikali
imewezesha kuwepo kwa maabara ya kisasa kwa ajili ya kupima ubora wa
maji, kupima ubora wa mita na maabara ya kukata mabomba zote zikiwa na
lengo la kuboresha hali ya upatikanaji wa maji safi na salama.
Dkt Kazumba alitoa rai kwa
Halmashuri zote nchini kuajiri Mafundi Sanifu na Wahandisi wa Maji kwa
ajili ya kuongeza tija katika sekta ya maji.
Alifafanua kuwa Mafundi Sanifu
waliohitajika kwa kipindi cha mwaka 2013 ilikuwa ni 3000 na mwaka 2014
ilifikia 6000 na dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa kila mhandisi
mmoja anakuwa na mafundi 5 wa kumsaidia kutekeleza majukumu yake.
Chuo cha Maji kilianzishwa mwaka
1974 kwa lengo la kuendeleza na kuzalisha wataalamu wa sekta ya maji
kupitia mafunzo, ushauri na tafiti mbalimbali.
No comments :
Post a Comment