Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na wakazi wa Kijiji
cha Nnivata kilichopo mkoani Mtwara kuhusu mradi wa ujenzi wa barabara
ya Mtwara-Masasi yenye urefu wa KM 210 itakayojengwa kwa kiwango cha
lami wakati alipokuwa akiikagua barabara hiyo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na wananchi wa Nanyamba
katika mkutano wa hadhara kuhusu mradi wa ujenzi wa barabara ya
Mtwara-Masasi yenye urefu wa KM 210 itakayojengwa kwa kiwango cha lami
wakati alipokuwa akiikagua barabara hiyo, mkoani Mtwara.
Muonekano wa sehemu ya kwanza ya
barabara ya Mtwara-Nnivata yenye urefu wa KM 50 itakayoanza kujengwa
mwezi Aprili mwaka huu kwa kiwango cha lami. Mradi huo utagharimu kiasi
cha Shilingi bilioni 89.5
Muonekano wa Korongo lililoko
kwenye moja ya barabara za Newala Mjini ambalo limetokana na mvua
zinazoendelea kunyesha mkoani Mtwara.
Mbunge wa Jimbo la Newala Mjini
Mhe. George Mkuchika (wa pili kulia), akimuonesha Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kushoto), eneo
lililoathiriwa na mvua (halipo pichani), zinazoendelea kunyesha katika
moja ya barabara jimboni hapo mkoani Mtwara. Wa pili kushoto ni Mkuu wa
Wilaya ya Newala Bi. Aziza Mangosongo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiagana na Mbunge wa Jimbo la Newala
Mjini Mhe. George Mkuchika mara baada ya kumaliza ziara yake wilayani
Newala, mkoani Mtwara.
………………………………………………………………………………….
Serikali
imesema itaanza ujenzi wa barabara ya Mtwara-Masasi KM 210
sehemu ya
Mtwara-Nnivata yenye urefu wa KM 50 kwa kiwango cha lami mwezi Aprili
mwaka huu, ili kurahisisha usafiri kwa wakazi wa maeneo hayo na kufungua
fursa za kiuchumi katika mkoa huo na nchini jirani ya Msumbiji.
Akizungumza
na wananchi wa Nanyamba wilayani Tandahimba, mkoani Mtwara, Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa
mkandarasi Dott Services Ltd ataijenga barabara hiyo kwa viwango vya
kisasa na kwa gharama za shilingi bilioni 89.5.
“Mkandarasi
atafika eneo la mradi mwezi wa nne mwaka huu na ujenzi utaanza mara
moja, hivyo wananchi muwe na subira ili muweze kunufaika na barabara
hiyo pindi itakapokamilika kwa kuwa itazidi kuchochea maendeleo yenu na
Taifa kwa ujumla”, amesema Waziri Mbarawa.
Waziri
Profesa Mbarawa amefafanua kuwa ujenzi huo utadumu kwa miaka miwili
tangu kuanza kwa ujenzi wake hadi kukamilika, hivyo Prof. Mbarawa
amewataka wananchi wa Mtwara kutoa ushirikiano kwa mkandarasi huyo ili
kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa.
Aidha,
Waziri Mbarawa ameongeza kuwa kwa wale wananchi waliovunjiwa nyumba zao
na kustahili kulipwa fidia kisheria ili kupisha ujenzi wa barabara hiyo
watalipwa, na kazi ya kutathimini nyumba hizo itaanza mapema mwezi wa
tatu mwaka huu.
Prof.
Mbarawa amesisitiza kuwa Serikali itaongeza fedha za ujenzi wa barabara
hiyo kwa awamu nyingine katika Mwaka wa fedha 2017/2018 ili kuweza
kufungua barabara yote kwa kipindi kifupi.
Kuhusu
huduma za mtandao wa mawasiliano mkoani humo Prof. Mbarawa
amewahakikishia wananchi kuleta huduma hiyo katika wilaya zote kupitia
Mfuko wa Mawasiliano kwa wote ili kurahisisha mawasiliano ambapo kwa
sasa hali ya huduma ya mawasiliano katika baadhi ya vijiji hairidhishi.
Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Bw. Evod Mmanda amesema kuwa
barabara hiyo ikikamilika itarahisisha usafiri wa abiria na mizigo
ikiwemo mazao yanayolimwa katika mkoa huo hususan zao la Korosho ambalo
ni miongoni mwa mazao yanayoongeza pato kubwa kwa Taifa.
Mradi
wa ujenzi wa barabara ya Mtwara-Tandahimba-Newala-Masasi yenye urefu wa
KM 210 ambao unatarajiwa kuanza mwezi Aprili mwaka huu unatarajiwa
kuunganisha wilaya tano za mkoa wa Mtwara na hivyo kufungua fursa za
kiuchumi na kijamii katika Mkoa huo na nchi jirani ya Msumbiji.
No comments :
Post a Comment