Tuesday, February 14, 2017

PEMBA:MAHAKAMA YA MKOA WA WETE YAMUACHIA HURU MZEE WA MIAKA 60


Sheria+Picha
Na Masanja Mabula –Pemba ..
 
MAHAKAMA ya Mkoa Wete imemuachia huru mzee Ali Hamad Sadi (60) aliyekuwa anatuhumiwa kwa kosa la  kumuingia mwanamke punguwani baada ya mahakama kushindwa kujiridhisha na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka .
 
Mtuhumiwa huyo ambaye alidaiwa kutenda kosa hilo oktoba 17 mwaka 2014 majira ya saa 9;45 jioni na alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza oktoba 22 mwaka 2014 ambapo alikana kuhusika na kitendo hicho .
 
Jumla ya mashahidi watatu wameitwa kutoa ushahidi wao , ambapo kosa hilo ni kinyume na kifungu cha 133cha sheria No 6 ya mwaka 2004 sheria za Serikali ya Zanzibar.
 
Akisoma hukumu kwa mtuhumiwa huyo , Hakimu wa Mahakama hiyo Makame Mshamba Simgeni mbele ya Mwendesha mashtaka wa Serikali Juma Ali Juma  , amesema mashahidi walioitwa kutoa ushahidi dhidi ya kesi hiyo wametofautiana katika maelezo yao .
 
Aidha chengine ambacho mahakama imekibaini  ni  pamoja na mapungufu katika kesi na kukosekana kwa maelezo kutoka kwa daktari wa magonjwa ya akili ili kuthibitisha kwamba mwathirika wa tukio hilo ni punguwani .
 
Ameongeza kwamba hata kama daktari asigeweza kupatikana , mahakama ingeridhika iwapo mama mlezi wa mwathirika wa tukio hilo angeitwa mahakamani  kutoa maelezo yakuthibitisha kwamba mwathirika ni punguwani .
 
Hata hivyo upande wa mashitaka umesema hakuridhika na maamuzi hayo ambapo mwendesha mashitaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka  wa Serikali Juma Ali Juma amesema anakusudia kukata rufaa katika mahakama ya juu kupinga uwamuzi huo.
 
Mzee huyo amepewa dhamana ya maandishi wa shilingi laki tano (500,000/=) ili akiitwa mahakamani baada ya kukatwa rufaa aweze kuhudhuria  .

No comments :

Post a Comment