Benny Mwaipaja-WFM, Dodoma
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt.
Philip Mpango, amezitaka Kampuni kubwa na za kati kuchangamkia fursa ya
uwepo wa Sekta ya Soko la Mipaji, kwa kujiorodhesha katika soko la hisa
la Dar es salaam ili kushiriki moja kwa moja katika umiliki wa uchumi wa
nchi.
Dkt. Mpango ametoa rai hiyo
Bungeni Mjini Dodoma, wakati akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa
Jimbo la Magomeni, Mhe. Jamal Kassim Ali, aliyetaka kujua mchango wa
Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) na Soko la Hisa la Dar es
saam (DSE), kwa wafanyabiashara wazawa.
Alifafanua kuwa kampuni kadhaa,
ikiwemo Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), TOL Gases, Kiwanda cha Sigara
(TCC), Kiwanda cha Saruji Tanga, Wakala wa Huduma za Mizigo kwenye
viwanja vya ndege-Swissport na Benki ya NMB, ni baadhi ya kampuni
zinazouza hisa zake katika Soko la Hisa la Dar es salaam.
Dkt. Mpango alisema kuwa kampuni
hizo zimechangia kukuza uchumi wa nchi ikiwemo ajira, kutoa gawiwo kwa
Serikali na wanahisa, lakini pia ni miongoni mwa walipa kodi wakubwa.
“Kwa mfano kwa mwaka 2015 NMB,
ilitoa gawiwo Serikalini kiasi cha shilingi bilioni 16.5 na TCC shilingi
billion 1.4 kwa hisa zinazomilikiwa na Serikali huku mapato yatokanayo
na kodi pamoja na gawiwo, hutumiwa katika kutoa huduma mbalimbali ambazo
jamii ikijumuisha wafanyabiashara wadogo hunufaika nazo”alisema Dkt.
Mpango
“Vilevile, Serikali imekuwa
ikitumia masoko ya mitaji kama chanzo cha upatikanaji wa fedha za bajeti
(Treasury Bonds), Miradi inayotekelezwa na fedha hizi, pamoja na mambo
mengine, imekuwa ikitoa ajira na fursa za kibiashara kwa wafanyabiashara
wazawa; wadogo na wa kati” aliongeza Dkt. Mpango
Dkt. Mpango, alibainisha kuwa
Serikali inatambua mchango mkubwa wa kampuni ndogo ndogo katika kukuza
uchumi wa nchi ndio maana mwaka 2013 Soko la Hisa la Dar es Salaam
lilianzisha dirisha linaloziwezesha kampuni ndogo na za kati za wazawa
zisizokidhi vigezo vya kujiunga na soko hilo kupitia dirisha kuu,
kutumia Soko la Hisa katika kupata mitaji kutoka kwa umma wa watanzania.
Dkt. Mpango alibainisha kuwa
watanzania wengi wananufaika na uwepo wa soko la hisa, na kushiriki moja
kwa moja katika umiliki wa uchumi wa nchi huku akizitaja baadhi ya
kampuni zilizonufaika na utaratibu huo wa dirisha dogo la hisa kuwa ni
Benki ya Mwalimu Commercial Bank, Swala Oil and Gas Tanzania, Maendeleo
Bank PLC, Yetu Microfinance na Mkombozi Commercial Bank, ambazo zina
jumla ya mitaji isiyopungua shilingi bilioni 120
No comments :
Post a Comment