Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi, Jaji wa Rufaa Mhe. Semistocles Kaijage (Katikati) akitoa
Risala kuhusu upigaji wa Kura katika uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la
Dimani Zanzibar na Kata 19 za Tanzania Bara leo mjini Zanzibar. Kushoto
ni Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar, Mhe. Hamid
M. Hamid na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa NEC, Bw. Emmanuel Kawishe
(Kulia).
Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa
NEC, Bw. Emmanuel Kawishe (Kulia) akitoa ufafanuzi kuhusu masuala ya
Kisheria ya kuzingatiwa na wapiga Kura, Mawakala wa Vyama vya Siasa
wakati wa Uchaguzi mdogo wa Ubunge na Udiwani utakaofanyika kesho,
Januari 22, 2017. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa NEC, Jaji wa Rufaa Mhe.
Semistocles Kaijage.
Waandishi wa Habari wakiuliza maswali mbalimbali wakati wa Mkutano huo.
Picha/ Aron Msigwa – NEC.
……………
Na. Aron Msigwa –NEC, Zanzibar.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
imewataka wananchi wanaoishi katika kata 19 zitakazofanya Uchaguzi mdogo
wa Madiwani kwa upande Tanzania Bara na Ubunge katika jimbo la Dimani
Zanzibar Januari 22, 2017 wajitokeze kwa wingi kupiga kura kuwachagua
viongozi watakaowaongoza kwa kipindi cha miaka 3.
Akizungumza na vyombo vya Habari
leo mjini Zanzibar, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa
Rufaa, Mhe. Semistocles kaijage amesema kuwa maadalizi ya Uchaguzi huo
yamekamilika na wananchi wenye sifa za kupiga kura katika uchaguzi huo
wajitokeze kutimiza wajibu wao wa Kikatiba.
Mhe. Kaijage amewapongeza wananchi
wanaoishi katika Jimbo la Dimani, Zanzibar na wale wa Kata 19 za
Tanzania Bara zitakazofanya uchaguzi mdogo hapo kesho kwa utulivu
waliouonyesha wakati wa kipindi cha Kampeni za Uchaguzi huo.
Ameeleza kuwa licha ya kuwepo kwa
dosari za hapa na pale zilizojitokeza zikiwemo za ukiukwaji wa Maadili
ya Uchaguzi kwa baadhi ya Vyama na wagombea wao, Tume ya Taifa ya
Uchaguzi ilichukua hatua za kukemea vitendo hivyo ili kuwezesha Kampeni
za Uchaguzi kufanyika kwa Usalama na Amani.
“Licha ya kwamba kutakuwa na
ulinzi wa kutosha katika vituo vya kupigia kura, Ni matumaini ya Tume
kuwa hali ya Amani na Utulivu ambayo imekuwepo hadi sasa na kama
ilivyokuwa katika Chaguzi zilizopita itaendelea kudumishwa ili
kuhakikisha uchaguzi huu unafanyika kwa Utulivu, Amani na Ustawi wa
Taifa letu” Amesema Jaji Kaijage.
Ameeleza kuwa katika uchaguzi huo
jumla ya Wapiga Kura 9,280 wa Jimbo la Dimani Zanzibar wanatarajiwa
kupiga kura ili kumchagua Mbunge atakayewaongoza kwa kipindi cha miaka 3
kupitia vituo 29 vya Kupigia Kura katika Jimbo hilo.
Kwa upande wa Uchaguzi Mdogo wa
Madiwani katika Kata 19 za Tanzania Bara Wapiga Kura 134,705
walioandikishwa wanatarajia kupiga kura katika vituo 359 ambavyo
vilitumika katika Uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
“Naomba nitumie fursa hii kutoa
rai kwa wananchi waliojiandikisha wajitokeze kwenye vituo vilivyotumika
wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ili waweze kupiga kura kuwachagua
viongozi mnaowataka bila hofu, woga, wasiwasi au ushawishi” Amesisitiza.
Kuhusu mchakato mzima upigaji wa
kura ikiwemo taratibu za kuzingatiwa na wananchi kwenye vituo vya
kupigia Kura, uhesabuji wa Kura, ujumlishaji wa Kura na Utangazaji wa
matokeo amesema kuwa hatua zote zitafanywa na Wasimamizi wa Uchaguzi kwa
kuzingatia Sheria.
Amesema kuwa siku ya uchaguzi
Januari 22, 2017 vituo vyote vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa
saa 10:00 jioni na kufafanua kuwa iwapo wakati wa kufunga Kituo
watakuwepo Wapiga Kura katika mstari ambao wamefika kabla ya saa kumi
jioni na hawajapiga wataruhusiwa Kupiga Kura.
Jaji Semistocles amesisitiza
kwamba mtu yeyote hataruhusiwa kujiunga katika mstari wa Wapiga Kura
baada ya saa kumi (10:00) jioni muda ulioainishwa kisheria.
Ameeleza kuwa kwa kila mpiga kura
katika jimbo hilo akumbuke kubeba Kadi yake ya Mpiga Kura kwa kuwa
Sheria ya Uchaguzi inaelekeza kuwa ili Mpiga Kura aruhusiwe kupiga kura
ni lazima awe na kadi ya Mpiga Kura.
“ Naomba ieleweke wazi kuwa Fomu
Na. 17 sio mbadala wa Kadi ya Mpiga Kura, Wapiga Kura ambao wana Kadi ya
Mpiga Kura lakini taarifa zao hazimo katika Daftari la Kudumu la Wapiga
Kura Kituoni, hawataruhusiwa kupiga kura” Amesisitiza Jaji Kaijage.
Amesema kuwa ni marufuku na ni
kosa la jinai kumkataza mtu kwenda Kupiga Kura akisisitiza kwamba siku
hiyo ya kupiga kura kipaumbele kitatolewa kwa wagonjwa, watu wenye
ulemavu, wanawake wajawazito au wenye watoto wachanga na wazee ambao
hawatatakiwa kupanga mstari.
Jaji Semistocles amefafanua kuwa
wakati wote wa Kupiga Kura na Kuhesabu Kura, Mawakala wa Vyama vya Siasa
watakuwepo kwenye vituo kwa kuwa wajibu wao ni kulinda maslahi ya Vyama
vyao vya Siasa na Wagombea wao.
Hata hivyo amesema hawatakiwi kuingilia masuala ya utendaji ambayo yamekabidhiwa kwa Msimamizi wa Kituo.
Amesema Mawakala hao wataruhusiwa
kuwepo Vituoni kwa mujibu wa Sheria na Kanuni na kusisitiza kwamba
Wakala asiyekuwa na barua ya utambulisho kutoka kwa Msimamizi wa
Uchaguzi na ambaye hatakula kiapo cha kutunza siri hataruhusiwa kuingia
katika Kituo cha Kupigia, Kuhesabia na Kujumlishia Kura.
Katika hatua nyingine Jaji Kaijage
amebainisha kuwa Kura zilizopigwa zitahesabiwa katika Kituo cha
Kupigia Kura mara tu Upigaji Kura utakapokamilika na matokeo husika ya
Kituo kujazwa kwenye Fomu za Matokeo Na. 21B kwa upande wa Ubunge na
Fomu Na. 21C kwa upande wa Udiwani kisha fomu hizo kutiwa saini na
Msimamizi wa Kituo/Msimamizi Msaidizi wa Kituo, Mawakala wa Vyama au
Mgombea aliye Kituoni.
Amesema nakala moja watapewa
Mawakala/Mgombea na nakala nyingine itabandikwa nje ya Kituo cha
Kuhesabia kura ambapo Wakala wa kila Chama cha Siasa na mlinzi wa Kituo
watakaokuwa Kituoni wataruhusiwa kusindikiza msafara wa kupeleka matokeo
ya Uchaguzi kwenda kwa Msimamizi wa Uchaguzi/Msimamizi Msaidizi wa
Uchaguzi wa Kata kwa upande wa Tanzania Bara na kwa Msimamizi wa
Uchaguzi/Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Dimani kwa upande wa
Zanzibar.
Amefafanua kuwa matokeo yote
yakishapokelewa na Msimamizi wa Uchaguzi kwa upande wa Uchaguzi wa
Ubunge na Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi kwa upande wa Uchaguzi wa
Udiwani, yatajumlishwa mbele ya Mawakala na wote wanaoruhusiwa kuingia
kwenye vituo vya Kujumlishia Kura.
“ Kama ilivyokuwa wakati wa
Kuhesabu Kura, baada ya Ujumlishaji kukamilika matokeo ya Ubunge ngazi
ya Jimbo yatajazwa katika Fomu Na. 24B na yale ya Diwani katika Kata
yatajazwa katika Fomu Na. 24C, Fomu za Matokeo hayo zitatiwa saini na
Msimamizi wa Uchaguzi na Mawakala watakaokuwepo watapewa nakala za Fomu
za Matokeo na Nakala moja itawekwa mahali pa wazi nje ya Kituo cha
Kujumlisha Kura”
Akitoa ufafanuzi kuhusu kampeni za
uchaguzi huo amesema zitamalizika leo (Januari 21) saa 12 jioni na
Vyama, Wagombea na mashabiki hawataruhusiwa kufanya kampeni za aina
yoyote ikiwa ni pamoja na kutumia alama zozote zinazoashiria Kampeni
kama vile bendera na mavazi ya vyama vyao.
Kuhusu uwazi katika uendeshaji wa
uchaguzi huo amefafanua kuwa vyama vyote vya Siasa vinavyoshiriki katika
Uchaguzi vinatakiwa kuhakikisha kwamba vinaweka Mawakala katika vituo
vyote vya Kupigia Kura na Kujumlishia Kura ambao watatimiza majukumu
yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa.
Jaji Kaijage amesisitiza kuwa kwa
kuzingatia Maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2015 yaliyokubaliwa na Vyama
vyote vya Siasa, Wapiga Kura wanatakiwa kuondoka Vituoni mara baada ya
kupiga kura ili kuendelea na shughuli zao kwa kuwa Vyama vya Siasa
vyenye wagombea vitakuwa na Mawakala vituoni ambao watalinda maslahi ya
Vyama na Wagombea wao huku watu waliotajwa kwenye Sheria ya Uchaguzi
wakiwemo wagombea, mawakala, Afisa wa Tume, msimamizi wa Uchaguzi na
Afisa Usalama ndiyo wanaoruhusiwa kuingia kwenye Vituo vya Kupigia,
Kuhesabia na Kujumlishia Kura.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa
Idara ya Huduma za Sheria wa NEC, Bw. Emmanuel Kawishe amewaaeleza
waandishi wa Habari kuwa kwa mujibu wa sheria mwenye mamlaka ya
kumtangaza Mshindi ngazi ya Ubunge ni Msimamizi wa Uchaguzi na kwa ngazi
ya Udiwani mwenye mamlaka ya kufanya hivyo ni Msimamizi Msaidizi wa
Uchaguzi.
Amesema kuwa zoezi la Kupiga Kura,
Kuhesabu kura ,Kujumlisha Matokeo na Kutangaza matokeo litafanywa kwa
uwazi na kwa kuzingatia Sheria na kutoa wito kwa wananchi wajitokeze kwa
wingi kuwachagua viongozi wao.
Amesema kuwa wananchi
watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale wenye sifa ambao watakuwa na kadi za
kupigia kura na ambao majina yao yameonekana kwenye Daftari la kudumu
la kupigia Kura na kusisitiza kwamba mwananchi ambaye jina lake
halitakuwa kwenye Daftari la Kudumu la kupigia kura hataruhusiwa kupiga
kura.
“Utaratibu wa kupiga kura
umeelezwa katika Sheria, Ukisoma kifungu cha 63 kifungu kidogo cha 3 cha
Sheria ya Taifa ya Uchaguzi A, kinaeleza wazi mwananchi anapofika
kituoni alipopangiwa na Tume anaonyesha kadi yake ya kupigia kura na
kisha jina lake linaitwa kwa sauti na ikiwa amekidhi sifa anaruhusiwa
kupiga kura asipokidhi sifa Msimamizi wa Uchaguzi anayo Mamlaka ya
kumzuia asipige Kura” Amesema.
No comments :
Post a Comment