Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema
Serikali imetoa sh. bilioni 1.4 kati ya sh. bilioni 1.8 zilizotengwa
katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya uendelezwaji wa mradi wa ujenzi
wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe.
Amesema ujenzi wa hospitali hiyo ni
utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015/2020 ya
kuwa na zahanati katika kila kijiji, kituo cha afya katika kila kata,
hospitali katika wilaya na hospitali za rufaa kwa kila mkoa.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo
(Jumamosi, Januari 21, 2017) wakati alipotembelea eneo la mtaa wa
Wikichi inapojengwa hospitali hiyo akiwa katika siku ya tatu ya ziara
yake ya kikazi mkoani Njombe.
Amesema lengo la ujenzi wa hospitali hiyo
ni kuhakikisha mwananchi anaanza kupata huduma za afya katika eneo lake
na anapokuwa na tatizo kubwa ndipo atakwenda hospitali ya wilaya na
kisha hospitali ya rufaa ya mkoa.
“Hospitali hii ikikamilika itawapunguzia
wananchi gharama za kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kufuata huduma za
rufaa. Sasa hakutakuwa na sababu ya kwenda Iringa, Mbeya wala Ruvuma
huduma zote zitakuwa zinapatikana hapa hapa Njombe,” amesema.
Amesema ujenzi huo utakapokamilika
Serikali itapeleka fedha za ununuzi wa dawa na vifaa tiba. “Hatuwezi
kukosa fedha za kununulia vifaa tiba na dawa kwani ni moja ya majukumu
yetu,”.
“Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli
ameahidi kuwahudumia na kuwatumikia wananchi wote bila ya kujali uwezo
wao, itikadi zao za kidini na kisiasa na hapa ndiyo maana ya ahadi hiyo
ya Serikali ya kuwahudumia. Watu wote watakuja kutibiwa hapa,” amesema.
Akitoa taarifa ya ujenzi mradi wa
hospitali hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Bw Jackson Saitabau
amesema kukamilika kwa ujenzi wa hospitali hiyo kutawapunguzia wananchi
gharama kubwa za kufuata huduma za rufaa katika mikoa ya jirani.
Amesema ujenzi wa hospitali hiyo ulianza
katika eneo hilo lenye ukubwa wa takribani ekari 70 katika mwaka wa
fedha wa 2013/2014, ambapo kiasi cha sh. 953.705 zilitengwa kati yake
sh. milioni 236.575 zilitumika kwa ajili ya ulipaji wa fidia.
“Hospitali hii inajengwa kwa awamu na
tulianza na jengo la wagonjwa wa nje (OPD) ambapo gharama za mradi ni
sh. bilioni 3.2 huku gharama za mtaalamu mshauri ni sh. milioni 114.160.
Mradi ulianza Julai 23, 2016 na unatarajiwa kukamilika Januari 26,
2018,” amesema.
Amesema kuwa hadi sasa kazi ya ujenzi huo
imekamilika kwa asilimia 40 na mkandarasi ameshalipwa sh. milioni
892.963 sawa na asilimia 28 ya gharama za mradi na mtaalam mshauri
amelipwa sh. milioni 51.50.
Naye Mbunge wa Jimbo la Njombe, Mheshimiwa
Edward Mwalongo ameishukuru Serikali kwa kuwawezesha kupata hospitali
ya Rufaa ya mkoa huo na amewaomba wananchi waendelee kuiunga mkono
Serikali na washiriki kikamilifu katika kuilinda miundombinu hiyo.
Pia Waziri Mkuu amezindua Ofisi ya
Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe iliyojengwa katika Kata ya
Igwachanya pamoja na kupokea taarifa ya ujenzi wa Ofisi hiyo pamoja na
kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya
Wanging’ombe.
Aidha, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa
halmashauri hiyo ambao wananshi nje ya eneo wilaya hiyo wawe wamehamia
ifikapo Februari 15 mwaka huu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, JANUARI 20, 2017.
No comments :
Post a Comment