Mtumishi wa Umma atakayeshindwa kuwasilisha cheti cha elimu na taaluma au “Index number” ya mtihani ili zihakikiwe na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), itakapofika tarehe 1 Machi, 2017atakua kajiondoa kazini mwenyewe.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah J.
Kairuki (Mb) alibainisha hayo mwishoni mwa wiki wakati akifungua mkutano
wa Watendaji Wakuu wa Wakala za Serikali jijini Dar es salaam.
“Watendaji Wakuu ninawaomba
msimamie uhakiki wa vyeti ili watumishi wenu wafanye kazi kwa sifa
stahiki” Waziri Kairuki alisisitiza.
Aliongeza Serikali ilisitisha
ajira mpya ili kupisha zoezi la kuondoa Watumishi hewa, zoezi ambalo
limefika ukingoni na siku za karibuni ajira zitarudishwa.
Waziri Kairuki aliwataka Watendaji
Wakuu kuweka mikakati ya kuepuka watumishi hewa na kusimamia kwa dhati
kwasababu jambo hilo limeumiza na kupoteza rasilimalifedha nyingi za
Serikali.
Alisema anatambua kuna Wakala
zenye upungufu wa Watumishi hivyo zinaingia gharama kubwa za kuajiri
wafanyakazi wa mikataba, hata hivyo alielekeza kila Mtendaji Mkuu
ajiridhishe kwa kuandaa taarifa ya mahitaji halisi ya Watumishi.
Waziri Kairuki, pamoja na hilo
alielekeza Wakala zenye Watumishi wa mikataba zifanye tathmini na
kuhakiki kama kweli watumishi hao wanahitajika kwa kuwa eneo hilo ni
moja ya maeneo yenye ajira za mashaka kwa baadhi ya Taasisi.
Waziri Kairuki aliongeza kuwa yapo
malalamiko kuhusu suala la maadili na uwajibikaji yanayozigusa Wakala
za Serikali. Aliainisha masuala hayo ni pamoja na Watumishi hewa,
taarifa chafu za Watumishi, matumizi mabaya ya madaraka na rasilimali za
Umma, kutosimamia ipasavyo utekelezaji wa mifumo ya utendaji kazi na
wakati mwingine kutotekeleza majukumu ya msingi ya wakala.
Alifafanua kuwa amegundua kupitia
taarifa mbalimbali kuwepo kwa changamoto ya mawasiliano hafifu kati ya
Wizara mama na Wakala zilizo chini yao ambapo taarifa kutoka katika
Wakala hazichambuliwi inavyostahili na hata zinapochambuliwa na wizara
mama, hazitoa mrejesho kwenda katika Wakala.
Awali, Katibu Mkuu Ofisi ya
Rais-Utumishi Dkt. Laurean Ndumbaro alizitaka Wakala za Serikali
kuimarisha eneo la ufuatiliaji na tathmini ili kuimarisha utendaji kazi
na kuleta mabadiliko yanayotarajiwa na Watanzania.
Alisema matarajio ya Serikali ya
Awamu ya Tano ni kuhakikisha Wakala za Serikali zinapunguza utegemezi
kwa Serikali kwa kujitegemea kimapato kutokana na vyanzo vyake vya ndani
hasa kwa Wakala zinazoingiza mapato makubwa kutokana na huduma
zinazotoa.
Serikali ilianzisha Wakala kwa
lengo la kuzifanya vyombo vya kutekeleza majukumu kwa niaba ya Serikali
kwa tija na ufanisi zaidi, pia kupunguza urasimu na hivyo kutoa huduma
bora kwa wakati kwa wananchi.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
No comments :
Post a Comment