Na Benny Mwaipaja, WFM, Songwe
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na
Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda, amewaonya mawakala wa forodha katika
mpaka wa Tanzania na Zambia wa Tunduma/Nakonde kuacha Mara moja tabia ya
kuwachelewesha madereva wa malori yaendayo masafa marefu kwa makusudi
ili wapewe rushwa.
Prof. Mkenda ametoa
onyo hilo katika mpaka huo wa Tunduma na Nakonde, baada ya kupokea
malalamiko kutoka kwa baadhi ya madereva wa malori waliodai wamekuwa
wakicheleweshwa kuvuka mpaka huo kwa zaidi ya siku tatu hadi tano.
Wadereva hao wameeleza
kuwa mawakala wa forodha wamekuwa wakiwaambia kuwa nyaraka zao
zinazohusika na mizigo wanayosafirisha zimekuwa zilicheleshwa na kituo
cha Forodha upande wa Zambia.
Hata hivyo Meneja wa
Mamlaka ya Mapato Zambia (ZRA), Kituo cha Nakonde, Bw. Nase Lungu,
amekana kuhusika na ucheleweshaji huo na baada ya ukaguzi wa moja ya
nyaraka hizo ilibainika kuwa upande wa Zambia unatoa nyaraka hizo kwa
wakati lakini zimekuwa zikifichwa na Mawakala wa Forodha upande wa
Tanzania.
Wakitoa ufafanuzi wa
tuhuma hizo, madereva hao wamesema kuwa mawakala wa forodha kwa muda
mrefu wamekuwa wakiwaeleza kuwa mtandao wa intaneti wa Upande wa Zambia
unaotumika kuchakata nyaraka zao uko chini, hivyo walitakiwa kutoa
shilingi 10,000 kwa kila nyaraka ili “kurahisisha” kazi hiyo kwa kuwapa
kitu kidogo maafisa wa forodha wa Zambia.
“Mawakala wengine wa
forodha wana nyumba zao za kulala wageni hapa Tunduma kumbe
wanatulazimisha kukaa hapa ili tulale kwenye nyumba hizo hali inayotutia
hasara na wanatumia kutokujua kwetu kutudanganya kwamba mtandao uko
chini wakijua hatuna uwezo wa kufuatilia huko Zambia” alieleza kwa
masikitiko dereva mmoja
Baada ya kubaini uwepo
wa vitendo hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na
Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda, ameagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA
upande wa Tunduma kuandika kibao chenye namba za simu za Mkuu wa TRA
mpakani hapo zitakazotumiwa na madereva wanaocheleweshwa kwa makusudi
kutoa malalamiko yao.
“Tunataka madereva
mtumie siku moja tu kukamilisha nyaraka zenu ili muendelee na safari
yenu vinginevyo tutadumaza biashara kati ya Zambia na Tanzania na pia
tutaifanya Bandari yetu ya Dar es salaam kushindwa kuleta tija”
aliongeza Prof. Mkenda
Alisema kuwa wakala wa
forodha atakayebainika kufanya mchezo huo mchafu wa kuwarubuni madereva
na kuwachelewesha kupeleka mizigo nchini Zambia, watanyang’anywa leseni
zao za biashara.
Meneja Msaidizi wa
Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, mikoa ya Songwe na Mbeya, Bw.
Jomimassa Nsindo, amesema kuwa ofisi yake itashirikiana na madereva
kukomesha vitendo hivyo ambavyo amesema vinaharibu uchumi na biashara
mpakani hapo.
Naye Mkuu wa wilaya ya
Momba, mkoani Songwe, Bw. Juma Irando, alisema kuwa ataitisha kikao cha
Madereva, Mawakala wa Forodha na Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA katika
Mpaka huo wa Tunduma/Nakonde mapema, ili kuweka msimamo wa serikali na
kuwaeleza wahusika wanaokiuka taratibu hatua watakazochukuliwa.
Prof. Mkenda na Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban,
walikwenda katika mpaka huo wa Tunduma na Nakonde, kuangalia maandalizi
ya uanzishwaji wa Kituo cha Pamoja cha Mpakani kati ya Tanzania na
Zambia, unaotarajiwa kuanza Februari mosi, 2017, baada ya kusainiwa kwa
mikataba kati ya nchi hizo mbili, juzi.
No comments :
Post a Comment