Sunday, January 29, 2017

KAMPENI YA KUCHEZA OLIMPIKI 2020 KUZINDULIWA KESHO UWANJA WA KARUME


UIKO
Mkurugenzi wa Michezo, Yusuph Omari; Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kwa kushirikiana na Makamu Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Henry Tandau kesho Jumatatu Januari 30, kwa pamoja watazindua kampeni maalumu za kuifanikisha Tanzania kushiriki michuano ijayo ya Olimpiki itakayofanyika Tokyo, Japan.
Uzinduzi wa kampeni hizo unaopewa jina la ‘The Road to Tokyo 2020’ utafanyika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam saa 5.00 asubuhi ambako wadau na wafamilia wa mpira wa miguu wanakaribishwa.

Tayari timu ya Tanzania ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 23 ‘Kilimanjaro Warriors’ imeingia kambini kwa ajili ya maandalizi ya awali ya kucheza mechi za kufuzu fainali hizo za za Olimipiki.
Kambi hiyo imepigwa kwenye Hosteli za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambako pia kuna Uwanja wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mazoezi kulingana na program za walimu.
Tanzania haijapata kushiriki Michuano ya Olimpiki kwa upande wa mpira wa miguu jambo ambalo limeisukuma TFF kuona kuwa ni fursa ya mpira wa miguu kuchezwa hivyo inashirikiana na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), kufanikisha mipango na taratibu.
 ..………………………………………………………………………………………………
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments :

Post a Comment