WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema katika mwaka huu wa fedha Serikali imetenga sh. bilioni 19 kwa
ajili ya ujenzi wa barabara ya Njombe-Makete yenye urefu wa kilomita
109.4 kwa kiwango cha lami.
Ametoa kauli hiyo jana (Ijumaa,
Januari 20, 2017) wakati akizungumza na viongozi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Makete alipowasili katika kata ya Mtamba wilayani hapa akiwa
katika ziara yake ya kikazi mkoani Njombe.
Waziri Mkuu amesema usanifu wa
kina wa barabara ya Njombe-Makete kwa ujenzi wa kiwango cha lami
umekamilika hivyo amewataka wananchi waendelee kuwa na subira.
Amesema barabara nyingine
inayotarajiwa kujengwa ni ya kutoka Makete hadi Mbeya kupitia Isyonji
yenye urefu wa kilomita 96 ambayo imetengewa sh. milioni 50 kwa ajili ya
kufanyiwa usanifu.
Waziri Mkuu amesema wananchi
waendelee kushirikiana na Serikali kwani imedhamiria kuwatumikia kwa
kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maeneo yao.
Aidha, Waziri Mkuu amewataka
wahandisi wa wilaya hiyo kuhakikisha wanawasimamia vizuri wakandarasi
wanaojenga miradi mbalimbali katika halmashauri zao kuhakikisha kama
viwango vinalingana na thamani halisi ya fedha zinazotolewa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
aliwataka wakuu wa Idara katika halmashauri kupambana na vitendo vya
rushwa na wahakikishe watumishi hawatowi huduma kwa kuomba rushwa.
“Kwanza watumishi watambue kwamba
rushwa ni dhambi. Pia kiutumishi ni makosa makubwa hivyo wajiepushe na
vitemdo hivyo,” amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya
Makete Bi. Veronica Kessy amesema kujengwa kwa barabara hizo kwa kiwango
cha lami kutaimarisha ukuaji wa uchumi wa wilaya hiyo na Mkoa wa Njombe
kiujumla hivyo wananchi kupata tija.
“Mfano barabara ya kutoka Makete
hadi Mbeya kupitia Bulongwa, Iniho, Kikondo na Isyonje itasaidia wilaya
kufunguka hivyo kurahisisha usafirishaji wa mazao ya misitu kama mbao,”
amesema.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya
amesema barabara hii pia itaunganisha Wilaya hiyo na kiwanja cha ndege
cha kimataifa cha Songwe hivyo watapata fursa ya kuanzisha kilimo cha
maua. Awali walishindwa kulima maua kwa sababu hakukuwa na usafiri wa
uhakika.
Awali Waziri Mkuu alitembelea
shamba la mifugo la Kitulo linalomilikiwa na Wizara ya Kilimo, Mifugo na
Uvuvi lenye jumla ya Ng’ombe 750 wakiwemo ndama 61, majike 212, mitamba
273, madume 21, na madume wadogo 183.
Shamba hilo linazalisha wastani wa lita 450,000 za maziwa kwa mwaka kutokana na ng’ombe 123 wanaokamuliwa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, JANUARI 21, 2017.
No comments :
Post a Comment