Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (katikati), hii leo akizungumza na wanahabari baada ya kikao baina yake na viongozi
wa Tanesco pamoja na wawakilishi wa kampuni zilizohusika na
utengenezaji na ufungaji wa mitambo katika kituo cha kuzalisha umeme kwa
kutumia mafuta mazito cha Nyakato Jijini Mwanza.
Kushoto
ni balozi wa Norway nchini Tanzania, Hanne-Marie Kaarstad na kulia ni
balozi wa Denimark hapa nchini, Einar Jensen. Mabalozi hao wamehudhuria
kikao hicho ikiwa ni sehemu ya kusaidia kutatua mvutano baina ya kampuni
zinazotoka katika nchi zao na Tanesco kutokana na baadhi ya mitambo
iliyofungwa na kampuni hizo katika kituo cha Tanesco Nyakato Jijini
Mwanza kuharibika. Mradi huo uligharibu shilingi bilioni 129 hadi
kukamilika kwake na una uwezo wa kuzalisha Megawati 60 za umeme.
#BMGHabari
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (katikati), balozi
wa Norway nchini Tanzania, Hanne-Marie Kaarstad (kushoto) pamoja na
kulia ni balozi wa Denimark hapa nchini, Einar Jensen (kulia)
Waziri
wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo, ameliagiza Shirika la
Umeme nchini Tanesco kufanya matengenezo kwenye mitambo yake minne ya
kuzalisha umeme iliyoharibika katika Kituo cha Nyakato Jijini Mwanza
kabla ya kufikia Februari 28 mwakani.
Profesa
Muhongo ametoa agizo hilo hii leo Jijini Mwanza, baada ya kukutana na
viongozi wa Tanesco pamoja na wawakilishi wa kampuni zilizohusika na
utengenezaji na ufungaji wa mitambo hiyo kutoka nchi za Norway na
Denmark ambapo pia mabalozi wa nchi hizo wamehudhuria kikao hicho.
Aidha
Profesa Muhongo ameiagiza Tanesco kuhakikisha mitambo sita iliyosalia
haiharibiki tena na kwamba inamaliza kazi ya kusafisha mitambo yote
katika kituo hicho kabla ya kufikia mwezi Februari 28 mwakani ambapo
imeelezwa kwamba baadhi ya mapungufu katika mitambo hiyo yalitokana na
kutosafishwa kwa wakati. Kampuni zote mbili zimekubali kushirikiana na
Tanesco katika kutekeleza makubaliano hayo.
Awali
kulikuwa na mvutano baina ya Tanesco na Kampuni ya Rolls Royce ya
nchini Norway iliyotengeneza mitambo hiyo pamoja na kampuni ya Semco ya
nchini Denmark iliyofunga mitambo hiyo, baada ya mitambo minne kati ya
10 kuharibika ndani ya kipindi cha miaka miwili na hivyo kusababisha
uzalishaji wa megawati 18 kati ya 60 zilizopaswa kuzalishwa kupungua.
Hata
hivyo pande zote zinazolalamikiana zimeonekana kuwa na hoja ambapo
Profesa Muhongo ameitaka Tanesco kuandika malalamiko yake na
kuyawasilisha kwa kampuni Rolls Royce iliyotengeneza mitambo hiyo kabla
ya februari 28 mwakani, malalamiko ambayo yanapaswa kujibiwa hadi
kufikia tarehe 30 mwezi Machi mwakani ili kujua maamuz yatayofuata.
Mabalozi
wa pande zote mbili, ambao ni Hanne-Marie Kaarstad kutoka nchini Norway
pamoja na Einar Jensen wa Denmark, wameeleza kuridhishwa na makubaliano
ya kikao hicho wakiamini kwamba mwafaka huo utasaidia uzalishaji wa
umeme kama ilivyokusudiwa ili kufikisha huduma ya umeme kwa wananchi.
No comments :
Post a Comment