Monday, December 19, 2016

MWIGULU -NI MARUFUKU TAASISI ZA KUHAMASISHA USHOGA /ZITAKAZOBAINIKA ATAFUTA USAJILI WAKE


nc
Waziri wa mambo ya ndani ,Mwigulu Nchemba akizungumza na waandishi wa habari Mkoani Pwani, baada ya kutembelea kujionea shughuli utendaji  kazi wa jeshi  la  polisi mkoani humo, ikiwemo shehena ya viroba vya bangi vilivyokamatwa hivi karibuni ,vinavyoonekana nyuma yake.(picha na Mwamvua Mwinyi)
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha

WAZIRI wa mambo ya ndani ,Mwigulu Nchemba,ametoa agizo la kukamatwa mara moja, kwa watu ama taasisi binafsi zinazojihusisha kutoa elimu na kuhamasisha ndoa za jinsia moja(Ushoga) na ajulishwe ili zifutiwe usajili.
Aidha amesema katika mikoa nchini iliyotikisa mwaka huu kwenye matukio makubwa ya kiuhalifu ikiwemo ya kutumia silaha,ni mkoa wa Pwani ambapo aliwapongeza polisi mkoani humo kufanya kazi nzuri ya kupambana katika matukio hayo.
Sambamba na hayo amelitaka jeshi hilo, kuendelea kudhibiti madawa ya kulevya sanjali na bangi kwa kuwakamata wauzaji na watumiaji kuanzia vijiweni .
Mwigulu,aliyasema hayo katika ziara yake ya siku moja ya kutembelea kujionea changamoto na utendaji wa kazi wa jeshi la polisi mkoani Pwani.
Alisema serikali haina mjadala na masuala ya ushoga,matumizi ya silaha ,wahamiaji haramu,madawa ya kulevya,ubakaji,mauaji na mimba za utotoni.
Mwigulu alisema kumezuka mtindo wa taasisi mbalimbali na watu kufanya kampeni za kueneza ushoga ,ambapo alisisitiza hawastahili kufumbiwa macho hivyo ni lazima wakamatwe na taasisi hizo zifutwe.
Alisema kuanzia sasa kunafanyika operesheni za kupambana na kusaka mambo ya aina hiyo ili kuhakikisha nchi inaleta taswira nzuri kimaadili na kiusalama kwa raia na mali zake.
Alieleza kuwa operesheni hizo ni za kudumu hadi hapo watakapohakikisha wamepiga vita kikamilifu masuala ya ushoga,ubakaji,madawa ya kulevya,mimba za utotoni na uhalifu wa kutumia silaha.
Mwigulu alifafanua kuwa endapo kuna kuwa na taarifa kuhusiana na kuwepo kwa taasisi hizo kuendelea na watu kufanya vitendoi hivyo hapa nchini na taratibu za kiafya zikathibitika basi hatua za kisheria zitachukuliwa.
Akizungumzia juu ya wale mashoga wanaojitangaza kwenye mitandao ya kijamii ,waziri huyo,alisema ,kama kuna mtu anajulikana na kuthibitika sheria itafuata mkondo wake kwani nchi hairuhusu vitendo hivyo.
Katika hatua nyingine Mwigulu alilitaka jeshi hilo kuendelea kupambana na uhalifu na kutoruhusu wahalifu wakaendelea kutamaraki na kutamba hivyo ni lazima kudhibiti kwa nguvu zote.
Alisema mkoa wa Pwani umefanya kazi kubwa ndani ya mwaka huu ,lakini imewaomba wasiridhike na juhudi walizozifanya badala yake wadhibiti njia zote za panya wanazotumia wahalifu kutokana na wahalifu hao kugeuza ni lango .
“Mkoa wa Pwani ni lango la wahalifu wanatumia njia za majini,bandarini ,na njia za panya hivyo kuna kila sababu ya kuendeleza mapambano dhidi ya wahalifu hao ili kupunguza masuala ya kiuhalifu mkoani hapa”alisema Mwigulu.
Mwigulu aliwataka polisi kuwakamata wauzaji bangi wa rejareja na wenye mashamba ya madawa hayo ili kupunguza changamoto ya kuweka rehani kundi kubwa la vijana ambao ni nguvu kazi.
Aliwaasa kuongeza juhudi na kusimamia kikamilifu kupambana na njia za majini,magendo na bandari bubu .
AKIZUNGUMZIA MAITI ZILIZOKUTWA NDANI YA VIROBA MTO RUVU
Waziri huyo alisema wameweka msimamo mkali kwa magari yatakayokamatwa kusafirisha wahamiaji haramu kuwa yatataifishwa na wahusika watakaobainika kusafirisha watu kutoka nchi nyingine kinyume na sheria watafungwa jela miaka 20.
Alisema jeshi la polisi bado linaendelea kuchunguza tukio hilo ili kujiridhisha chanzo halisi cha kilichosababisha vifo hivyo.
Mwigulu alisema wizara yake ipo kazini muda wote na kuhakikisha usalama wa watu na mali zao,ambapo kinachohitajika ni uzalendo kwa vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii kuhusu hilo.
Alisema anasikitishwa na taarifa zinazozidi kupotoshwa na baadhi ya watu na mitandao ya kijamii kutokana na ufafanuzi alioutoa hivi karibu juu ya wahamiaji haramu 81 ambao walikamatwa mkoani hapo kwa kudai inawezekana ni kati ya hao waliokufa.
Mwigulu alisema alichosisitiza ni kwamba kama huwa wakiwasaidia wahamiaji haramu waliodhoofika kwa kukosa lishe itakuaje baadhi ya watu hao waseme wameuawa na polisi.
Aliomba jamii iwe na uzalendo na kuacha kupotosha kauli zinazotolewa ufafanuazi na serikali ili kuondoa taarifa zinazoleta utata.
“Nilisema inawezekana au huenda ni wahamiaji haramu kutokana na mkoa wa Pwani unaongoza kwa njia za panya za majini ya kuingia wahamiaji hao,na hivi karibu kuna gari lilikamatwa na wahamiaji haramu na sio vinginevyo”alieleza Mwigulu.
Mwigulu alisema mkoa wa Pwani hasa Bagamoyo na Kibaha ndio yanayoongoza kukamata wahamiaji haramu na bandari bubu.
Hivi karibuni maiti sita ambazo hazijatambulika ziliokotwa zikielea Mto Ruvu zikiwa zimehifadhiwa kwenye mifuko ya Salfet maarufu kama viroba vya uzito wa kilogramu 200 huku zikiwa zimeharibika vibaya.
Nae mbunge wa jimbo la Mji wa Kibaha,Silvestry Koka,alimueleza waziri huyo,kuhusu changamoto ya gereza la wafungwa la Mkuza(mahabusu) kwani ni dogo ambapo linauwezo wa kuchukua watu 70 lakini linaweka watu 200 na halipo kwenye hadhi kutokana na kujengwa kwa mbavu za mbwa.
Aliomba wizara hiyo iangalie suala hilo kwa kuzingatia haki za binadamu hali itakayosababisha wafungwa kuishi mahala penye sehemu inayofaa na sio kama ilivyo sasa.
Koka alitaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na uhaba wa nyumba za polisi ambao hupata adha ya kupanga mitaani hivyo serikali itupie macho suala hilo.
Hata hivyo mbunge huyo alisema polisi pia wanakabiliwa na upungufu wa vitendea kazi ikiwemo,mafuta ya kutosha,matengenezo ya magari yao ya doria maslahi na kiutendaji ambapo yakiangaliwa watafanyakazi kikamilifu.
Koka alimshukuru Mwigulu kwa kutembelea mkoa huo kujionea changamoto zilizopo na kutoa maelekezo ambayo yanaashiria kuongeza ufanisi wa jeshi hilo .
MWIGULU-MIGOGORO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI
Mwigulu aliyaasa makundi hayo yaheshimiane na kuacha kuhalalisha kuweka rehani maisha ya kundi moja ama jingine kwa kumwaga damu pasipo sababu za msingi.
Alisema hakuna shamba lenye thamani sawa na maisha ya binadamu wala mifugo yenye thamani sawa na uhai wa mtu.
Mwigulu alieleza kuwa hakuna sababu ya kuhalalisha vifo ama kumtia mtu kilema kutokana na visasi vyao,hivyo atakaebainiaka kwa sasa kuleta madhara baina ya makaundi hayo hatua za kisheria zichukuliwe.
Alitoa rai elimu itolewe kati ya makundi hayo ili kuhakikisha wanaheshimiana ndani ya jamii na kuwachukulia hatua wale watakaosababisha migogoro kwa lengo la kukomesha migogoro hiyo.
Alisema sheria isipochukua mkondo wake na kupunguza makali ndipo jamii inapojichukulia sheria za mkononi.
KUHUSU MAUAJI YA REJAREJA KWA VIONGOZI MBAMBALI  
Waziri huyo alieleza kwamba watu wanaofanya vitendo vya aina hiyo ni lazima wabainike ili sheria ifuate mkondo wake.
Alilitaka jeshi hilo liendelee kuwasaka wanaohusika kusababisha vifo vya viongozi hao ama watu wanaofanyiana visasi  .
Aliyasema hayo baada ya kupata taarifa kutoka kwa kamanda wa polisi mkoani hapo,Boniventure Mushongi kuwa kumekuwepo kwa matukio mbalimbali ya baadhi ya watu kufanya mauaji ya viongozi hasa wa vijiji na vitongoji .
Mushongi alisema kumekuwepo na matukio hayo ambapo hadi sasa wanawatafuta na kufanya uchunguzi ili kuwakamata wahusika.
MWIGULU-MAKAZI YA POLISI
Mwigulu alisema kuna kila sababu ya kuweka mkakati wa kutumia fedha za makusanyo  mbalimbali yanayofanywa na jeshi la polisi katika kujenga nyumba za maaskari ili kupunguza tatizo la upungufu wa makazi na kukaa kwenye nyumba za kupanga.
Alisema mkoa wa Pwani unakusanya zaidi ya sh.bil 5 kwa mwaka hivyo endapo zingetumika kwa miaka mitatu kujenga nyumba hizo kungekuwa na nyumba nyingi zaidi ya idadi ya maaskari waliopo.
Mwigulu alieleza kuwa serikali ipo bega kwa bega kwa kusimamia kero za jeshi la polisi ikiwemo makazi ,sare na kujali maslahi na stahiki zao sio kama hisani.
Alisema uwezekano mwingine ni kutumia wafungwa nchini kwa kufanya kazi ya kujenga nyumba hizo katika maeneo mbalimbali .
Mwigulu aliwaomba ikifika muda wa kujengewa nyumba za askari kujenga kwa ramani za kisasa na kuachana na ramani za kikoloni

No comments :

Post a Comment