WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa
amesema Serikali imeunda tume kuchunguza taarifa inayoelezea utaratibu
uliotumika kumhamisha faru John kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda
Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko kwenye Hifadhi ya Grumeti
Serengeti pamoja na kutafuta kaburi la faru huyo.
Amesema timu hiyo ya wataalamu
tayari imeshafika Sasakwa VIP Grumet kwa ajili ya kutafuta kaburi na
kuchukua vinasaba vya masalia ya faru John na kisha watakwenda kwenye
Hifadhi ya Ngorongoro kuchukua vinasaba vya watoto wake na
kuvilinganisha na pembe hiyo ili kubaini kama kweli pembe aliyopelekewa
ni ya faru John au laa.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo
(Jumapili, Desemba 18, 2016) wakati wa majumuisho ya ziara yake ya
kikazi mkoani Arusha. Ziara hiyo ililenga kukagua utekelezaji wa
shughuli za maendeleo na kuona utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Tume niliyounda kwa ajili ya
uchunguzi wa faru John imetua VIP Grumet Serengeti kujiridhisha kama
kuna kaburi la faru John na kama lipo wachukue vinasaba na baada ya hapo
watakwenda Creter na kuchukua vinasaba vya watoto wa faru John na
kuvipima kwa pamoja. Lengo ni kutaka kubaini kama pembe iliyowasilishwa
kwangu Disemba 9 mwaka huu ni ya faru John,” amesema.
Waziri Mkuu amesema wakati faru
John akiwa V I P Grumet taarifa zilisema ni mgonjwa na daktari
alipompima mara ya kwanza akabaini faru huyo hakuna na ugonjwa
wowote.”Daktari alimpima tena kwa mara ya pili taarifa zikasema tena si
mgonjwa ghafla wakasema amekufa. Hili haliwezekani,”.
Waziri Mkuu amesema ameiagiza timu
hiyo kufanya kazi ya uchunguzi wa taarifa hizo kikamilifu kwa sababu
Serikali imetumia fedha nyingi kuwaleta faru hao kutoka nchini Afrika
Kusini. Ni lazima nyara hizo za Serikali zilindwe kwa manufaa Taifa.
Waziri Mkuu alipokea taarifa
inayoelezea utaratibu uliotumika kumhamisha faru John kutoka Hifadhi ya
Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko kwenye Hifadhi
ya Grumeti Desemba 9, 2016 katika kikao kilichofanyika kwenye makazi ya
Waziri Mkuu Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Kikao hicho kilihudhuriwa na
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe na baadhi ya
watendaji wa wizara yake, Baada ya kupokea taarifa hiyo Waziri Mkuu
alisema taarifa hiyo itafanyiwa kazi na wataalamu wa ofisi yake.
Akisoma taarifa hiyo mbele ya
Waziri Mkuu, Prof. Maghembe alisema hadi kufikia Desemba 2015 wakati
faru John anahamishwa alikuwa na watoto 26 (sawa na asilimia 70.2) ya
faru wote waliokuwepo ndani ya kreta.
“Kati ya faru 37 waliokuwepo ndani
ya kreta, watoto wake walikuwa 26 sawa na asilimia 70.2. Uamuzi wa
kumuondoa John ulikuwa ni muhimu ili kuwezesha kuongezeka kwa faru weusi
na kupunguza tatizo la ‘inbreeding’ ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro,”
alisema Waziri Maghembe.
Baada ya kuhamishiwa Sasakwa,
Waziri Maghembe alisema Julai 10, 2016 afya ya faru John ilianza
kudorora na alikufa tarehe 18 Agosti, mwaka huu. Taarifa hiyo
iliandaliwa na Kamati ya Taifa ya Kuwalinda Tembo na Faru. Kamati hiyo
inaundwa na Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI, Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA,
Mkurugenzi Mkuu wa NCAA na Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro.
Akikabidhi pembe za faru huyo
mbele ya Waziri Mkuu, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana
na Ujangili wa Wanyamapori, Bw. Robert Mande alimweleza kwamba pembe
kubwa ya faru John ilikuwa na uzito wa kilo 3.6 na pembe ndogo ilikuwa
na uzito wa kilo 2.3.
Desemba 6, mwaka huu, akiwa
ziarani mkoani Arusha, Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa Mamlaka ya
Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), umletee nyaraka zote zilizotumika
kumhamisha faru maarufu kwa jina la ‘John’ kutoka kwenye hifadhi hiyo
ifikapo Alhamisi, Desemba 8.
Alitoa agizo hilo alipotembelea
ofisi za makao makuu ya NCAA zilizoko wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha
na kuzungumza na watumishi wa mamlaka hiyo pamoja na Wajumbe wa Baraza
la Wafugaji ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, DESEMBA 18, 2016.
No comments :
Post a Comment