- Kaimu Katibu Mtendaji kutoka Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (aliyevaa suti) akiwa pamoja na maofisa wa mamlaka ya viwanja vya ndege na wa Tume ya Mipango wakielekea kukagua maeneo mbalimbali ya kiwanja hicho.
- Meneja wa Teknolojia na
Mawasiliano kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini , Bw. Abdulatif
Min-Hajj (aliyekaa kulia kwa Kaimu Katibu Mtendaji) akielezea mpango wa
kuboresha kiwanja cha ndege Mtwara mbele ya timu ya Ukaguzi wa Miradi
ya Maendeleo kutoka Tume ya Mipango.
- Kaimu Katibu Mtendaji, Tume ya Mipango Bibi Florence Mwanri akitoa ushauri kwa maofisa wa mamlaka ya viwanja vya ndege juu ya umuhimu wa kuwa na hati miliki ya eneo hilo.
- Mchumi Mkuu kutoka Tume ya
Mipango, Bibi Salome Kingdom akiongea jambo na Bw. Daniel Werema kutoka
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, wengine ni Mhandisi Omary
Othman (aliyevaa t-shirt) na Bw. Hekima Chengula kutoka Tume ya Mipango.
- Sehemu ya barabara inayotumika katika kutua na kuruka ndege (Runway) ya Kiwanja cha Mtwara. Urefu wa barabara hiyo ni mita 2258 na ina upana wa mita 30.
……………..
Na Adili Mhina, Mtwara.
Katika kutekeleza Malengo ya Dira
ya Taifa ya Maendeleo 2025, Mamlaka ya viwanja vya
Ndege imedhamiria
kufanya maboresho katika Kiwanja cha Ndege Mtwara kwa kiwango cha
Kimataifa ili kuendelea kuimarisha huduma za usafiri wa anga nchini.
Mapango huo umeelezwa hivi
karibuni na Meneja wa Teknolojia na Mawasiliano kutoka Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege nchini , Bw. Abdulatif Min-Hajj wakati akitoa taarifa
ya maendeleo ya Kiwanja hicho kwa Kaimu Katibu Mtendaji Tume ya
Mipango, Bibi Florence Mwanri alipofanya ziara katika kiwanja hicho
ikiwa ni mfululizo wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo unaofanywa
na timu kutoka Tume ya Mipango.
Meneja huyo alieleza kuwa mradi
huo amabao ni mpango wa muda mrefu unaolenga katika kufanya upanuzi wa
kiwanja pamoja na ujenzi wa jengo la kisasa kwa ajili ya abiria upo
katika hatua za awali ambapo mkandarasi mshauri tayari amewasilisha
rasimu ya taarifa ya mpango mkuu (maste plan).
“Katika mradi huu kiwanja cha
Mtwara kitapanualiwa na kufikia code 4E ambapo kitakuwa na uwezo wa
kuhudumia ndege kama A340-200. Katika ujenzi wa jengo la abiria, kwa
awamu ya kwanza tutajenga jengo lenye mita za mraba 6570 ili kufikia
mahitaji ya mwaka 2023 na awamu ya pili tunatarajia kuwa na jengo la
mita za mraba 10,880 ili kukidhi mahitaji ya abiria kwa mwaka 2033”,
alieleza Meneja huyo.
Kwa upande wake Kaimu Katibu
Mtendaji wa Tume ya Mipango, Florence Mwanri alieleza kuwa Dira ya Taifa
ya Maendeleo inasisitiza kuwa na vianzio mbalimbali vya uchumi na
kuwepo kwa miundombinu ya kutosha kuiwezesha Tanzania kuingia katika
nchi za kipato cha kati. Hivyo, mradi huo utasaidia kuimarisha uchumi wa
nchi sambamba na kuongeza ufanisi katika usafiri wa anga.
Aliongeza kuwa upanuzi wa kiwanja
hicho utakapokamilika sio kwamba tu utasaidia usafiri wa anga peke yake
bali kwa upande mwingine utafungua fursa mbalimbali za uwekezaji kwa
sekta binafsi na kusaidia kuongeza uchumi kwa watanzania.
“Nimeelezwa kuwa mradi huo
ukikamilika kutajitokeza fursa za uwekezaji kama kujenga mahoteli
makubwa ya hadhi ya nyota tano, kujenga eneo la biashara, ujenzi wa
maduka na migahawa ya kisasa, ujenzi wa visima vya mafuta ya ndege,
kutakuwa na jengo kubwa la kuhifadhia mizigo, na majengo ya kutengenezea
ndege. Hizi zote ni fursa zitakazosaidia kuinua uchumi wa wananchi
wetu,” alieleza.
Hata hivyo Mwanri alishauri kuwa
pamoja na kuwa na malengo mazuri ya muda mrefu mamlaka ya hiyo inapaswa
kuendelea kutekeleza malengo yake ya muda mfupi katika kutatua
changamoto za miundombinu ya barabara za ndege kiwanjani hapo ili
kuendelea kuimarisha huduma za usafiri huku akishauri mamlaka hiyo
kufanya jitihada za haraka kupata hati miliki pamoja na kufikiria
kujenga uzio katika eneo la kiwanja hicho.
“Mnapaswa kuendelea kutekeleza
mipango ya muda mfupi wakati mnasubiri mradi mkubwa utekelezwe. Najua
katika bejeti yenu ya sasa mtaendelea kukarabati miundombinu ili ndege
ziendelee kutua na kuondoka kwa usalama. Vile vile angalieni namna ya
kupata hati miliki na kujenga uzio wa eneo lote kwa ajili ya usalama na
kuwadhibiti watu wenye tabia ya kuvamia maeneo”, Alieleza Mwanri
No comments :
Post a Comment