MBUNGE wa jimbo la Arumeru
Mashariki, Mheshimiwa Joshua Nassari amepongeza na kusifu jitihada
kubwa zianazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuwaletea
maendeleo wananchi wa maeneo mbalimbali nchini wakiwemo wa jimbo lake.
Kufuatia hatua hiyo Mheshimiwa
Nassari ameahidi kushirikiana bega kwa bega na Serikali ili kuhakikisha
maendeleo yanakuwa endelevu.
Mheshimiwa Nassari ametoa pongezi
hizo leo (Jumapili, Desemba 18, 2016) mbele ya Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa ambaye alikuwa katika majumuisho ya ziara yake ya siku 10 ya
kikazi mkoani Arusha.
Mbunge huyo ambaye alilazimika
kuja nchini kwa dharura akitokea masomoni nchini Uingereza ili kumuwahi
Waziri Mkuu, amesema ameridhishwa na hatua za utatuzi wa migogoro ya
ardhi zinazochukuliwa na Serikali.
Amesema ziara ya Waziri Mkuu
mkoani Arusha, imesaidia kutibu majeraha na makovu makubwa yalitokana na
matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana.”Kama kuna kiongozi ambaye
hawezi kuunga mkono jitihada hizi za kuwaletea maendeleo watu wetu,
atakuwa na matatizo,” amesema.
Ameongeza kuwa kitendo cha Waziri
Mkuu kuweka mikakati ya kushughulikia migogoro ya ardhi iliyodumu kwa
miaka mingi ni ushahidi tosha kwamba Serikali ya Awamu ya Tano
imedhamiria kuwasaidia wananchi wa kawaida.
Mheshimiwa Nassari amesema mwaka
1952 wazee wa Meru walimtuma mtu kwenda Uingereza kuomba uhuru wa
wananchi wa Arumeru ili waweze kujitawala na kumiliki ardhi yao kutoka
kwa wakoloni.
Amesema wazee hao walichukua
uamuzi huo baada ya kuchoshwa na vitendo vya unyanyasaji vilivyokuwa
vinafanywa na wakoloni dhidi yao. Lakini miaka 55 imepita tangu nchi
ipate Uhuru bado migogoro na mateso hayo yapo.
Hivyo amempongeza Waziri Mkuu kwa
kuamua kuitafutia ufumbuzi changamoto ya ardhi wilayani Arumeru jambo
ambalo litawawezesha wananchi kupata ardhi kwa ajili ya kuendesha
shughuli zao za kimaendeleo zikiwemo za kilimo na ufugaji.
Waziri Mkuu jana (Jumamosi,
Desemba 17, 2016) alifanya ziara katika wilaya ya Arumeru ambapo alisema
Serikali itawanyang’anya ardhi wamiliki wote wa mashamba makubwa
wilayani Arumeru ambao hawajayaendeleza kwa sababu wamekiuka mkataba wa
umiliki.
Alisema Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William Lukuvi atakuja mkoani Arusha
kwa ajili ya kufanya mapitio ya mashamba yote makubwa ambayo
hayajaendelezwa na kuyarudishwa Serikalini.
“Tufanya mapitio ya kila shamba
ili kujua linamilikiwa na nani na alipewa lini na tangu alipokabidhiwa
amefanya nini. Shamba lisiloendelezwa litarudisha kwa wananchi. Kama mtu
ameshindwa kupata mtaji kwa muda wa miaka 10 atapata leo,” amesema.
Amesema Serikali haiko tayari
kuona wananchi wakinyanyaswa kwa kukosa ardhi ya kilimo kwa sababu ya
watu wachache kumiliki maeneo makubwa bila ya kuyaendeleza..
“Ninataarifa kwamba hapa Arumeru
kuna baadhi ya wawekezaji wanamiliki mashamba makubwa na
hawajayaendeleza. Wengine wanakodisha kwa wananchi ili kujipatia fedha
kinyume na mikataba yao ya umiliki. Hatutawavumilia,” alisema.
Alisema wilaya ya Arumeru
inaongoza kwa migogoro ya ardhi na maeneo mengi yametwaliwa na mtu mmoja
mmoja na baadhi yao wamekuwa wakilitumia vibaya Jeshi la Polisi kwa
kuwanyanyasa wananchi wanaokatiza au kulima kwenye maeneo hayo, ambapo
aliwataka polisi kuacha tabia hiyo mara moja.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, DESEMBA 18, 2016.
No comments :
Post a Comment