Saturday, December 31, 2016

WAZIRI MKUU AAGIZA WALIMU WAHAMIE SHULENI pmpic

pmpic
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza walimu wanaishi mbali na shule wakati shule zao zina majengo wahame mara moja na warudi kuishi kwenye nyumba za shule.
Amesema haifai kuacha walimu waishi mbali na maeneo ya shule kwani hali hiyo inachangia uchelewaji kazini na inapunguza muda wa kuwasimamia wanafunzi au kuwasaidia jioni pale wanapohitajika kufanya hivyo.

Ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Chingumbwa, kata ya Mbekenyera, wilayani Ruangwa jana mchana (Ijumaa, Desemba 30, 2016) kwenye mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa shule ya msingi kijijini hapo.
“Nimeambiwa kuwa walimu wako wachache kwa sababu hapa shuleni hakuna nyumba za kuishi walimu. Mbona wanakaa Mbekenyera? Watawezaje kuwahi kazini asubuhi wakati hawana magari? Mvua ikinyesha watafikaje shuleni? Kuanzia leo, walimu wote warudi mara moja na waje kupanga hapa kijijini kwa sababu nyumba zipo,” amesisitiza.
“Uamuzi wa walimu kuishi jirani na shule ulifikiwa ili mwalimu awepo na kuwasimamia wanafunzi wakati wakifanya usafi na wakati mwingine aweze kutoa msaada kwa wanafunzi wanaojisomea jioni pindi wakihitaji msaada au ufafanuzi,” amesema.
Pia Waziri Mkuu amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Bw. Andrea Chezue asimamie zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha anapunguza walimu walioko Ruangwa mjini na kuwahamishia shule za vijijini ambako kuna upungufu wa walimu.
Amesema ili kusaidia juhudi za Serikali za kuboresha elimu nchini, ni vema kila kijiji kikaweka utaratibu wa kuchangia matofali ili iwe rahisi kuanza ujenzi wa nyumba za walimu.
Akiwa katika kijiji cha Mkutingome, Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Ruangwa aliwahamasisha wakazi wa kijiji hicho wachangie matofali 100 kutoka kila kaya ili yapatikane matofali 40,000 yatakayotumika kujenga zahanati ya kijiji hicho.
Yeye aliahidi kuwachangia mabati 150 ambayo kati yake, mabati 100 yatatumika kuezekea zahanati ya kijiji na mengine 50 yatatumika kukamilisha nyumba ya Mwalimu ambayo imekaa kwa muda mrefu bila kumaliziwa.
Katika kuhakikisha ujenzi wa zahanati hiyo unaanza mara moja, Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya Wanyumbani Construction, Bw. Fakihi J. Bakili alichangia mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo ya kijiji cha Mkutingome. Nao Umoja wa Wachimbaji Wadogo katika mgodi wa Namungo ambao uko jirani na kijiji hicho waliahidi kuchangia mifuko 50 ya saruji.

IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAMOSI, DESEMBA 31, 2016

No comments :

Post a Comment