Saturday, December 31, 2016

HAKUNA UHABA WA DAWA YA USINGIZI HOSPITALI YA BOMBO


uukkkuuuu
Na Frank Mvungi (MAELEZO)
 
Serikali yasema hakuna uhaba wa dawa ya usingizi katika Hospitali ya Rufaa Bombo Mkoani Tanga kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari hapa nchini kuwa hali hiyo inachochea kuzorota kwa huduma za upasuaji.
 
Akifafanua suala hilo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga  Dkt. Asha Mahita amesema kuwa taarifa kuwa huduma za upasuaji katika hosipitali hiyo zimesimama si za kweli na ukweli ni kwamba huduma zinaendelea kama kawaida.
 
“Huduma za upasuaji katika Hosipitali yetu zinaendelea kama kawaida na hakuna tatizo kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari” Alisisitiza Dkt. Mahita.
 
Akifafanua zaidi Dkt. Mahita alisema kuna mgonjwa mmoja tu ambaye upasuaji wake ulisogezwa mbele kutokana na sababu za kitabibu na si kwa sababu ya kukosekana kwa dawa ya usingizi.
 
Aliongeza kuwa sababu zinazoweza kusababisha kuahirishwa kwa upasuaji wa mgonjwa aliye kwenye ratiba ni pamoja na uwepo wa wagonjwa wengi wa dharura hali inayoweza kuchangia nguvu kubwa kuelekezwa katika kuhudumia wagonjwa hao wakiwemo wahanga wa ajali.
 
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kuwahudumia wananchi na kuhakikisha kuna dawa za kutosha na vifaa tiba katika hospitali na vituo vya kutolea huduma hapa nchini.

No comments :

Post a Comment