Na Beatrice Lyimo -MAELEZO-DAR ES SALAAM.
UKIUKWAJI wa maadili ya Viongozi
wa Umma na Mgongano wa maslahi katika shughuli za umma ni miongoni mwa
changamoto zinazoikumba nchi nyingi duniani.
Changamoto hizo zinapishana kati
ya nchi na nchi ikiwemo ukubwa wa tatizo, madhara yake pamoja na mifumo
mbalimbali iliyowekwa katika kukubaliana na tatizo hili.
Inaelezwa kuwa matumizi mabaya ya
rasilimali za umma, kujilimbikiza mali isivyo halali, upendeleo katika
vyombo vya maamuzi, uvujishaji wa taarifa za siri za serikali, ukiukwaji
wa maadili ya kitaaluma na mienendo, ni miongoni mwa sababu
zinazosababisha ukiukwaji wa maadili.
Dhana ya maadili ya viongozi wa
umma inaelezwa ni msingi , kanuni na taratibu zinazoainisha tabia na
mienendo inayokubalika na isiyokubalika kwa viongozi wa umma na jamii
nzima.
Hivi karibuni Tanzania
iliadhimisha siku ya maadili duniani, iliyolenga kuhimiza ukuzaji wa
maadili katika utumishi wa umma, utetezi na ulinzi wa haki za binadamu,
uwajibikaji, utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi na
ubadhilifu wa mali za umma.
Akizungumza katika maadhimisho
hayo, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan anasema ili kufikia uchumi wa
viwanda ifikapo mwaka 2025 ni wajibu wa watendaji wa Serikali kuzingatia
maadili ya kazi na kuweka mbele maslahi ya umma na kuondoa malalamiko
kwa wananchi.nevu na maovu mengine na kila raia kuwa polisi kwa
mwenzake.
“Serikali itaendelea kutambua
mchango wa taasisi za uwajibikaji na utawala Bora katika jitihada zao za
kuimarisha misingi ya Utawala bora, uwazi, uadilifu na uwajibikaji”
alisema Samia.
Anazitaja taasisi hizo kuwa ni
Ofisi ya Rais-(Utumishi na Utawala bora), Takukuru, Sekretarieti ya
Maadili, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Tume ya Haki
za binadamu, Mamlaka ya Ununuzi wa Umma, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.
Makamu wa Rais anasema kuwa
Serikali itaendelea kutoa ushirikiano katika taasisi hizo ili
kuhakikisha zinatoa huduma bora za ukaguzi zenye kuleta tija kwa
wananchi na hivyo kuimarisha uwajibikaji na thamani ya fedha kwenye
makusanyo na matumizi ya rasilimali za umma.
Anasema kuwa Serikali itaendelea
kuziwezesha kiutendaji taasisi hizo ili kuhakikisha zina uwezo wa kukuza
na kusimamia viwango vya maadili kwa kutoa elimu, kufanya uchunguzi,
kupokea na kuhakiki matamko ya mali na madeni ya viongozi wa umma.
Anaongeza kuwa Serikali
itaendelea kulinda rasilimali za umma na kuondoa uonevu na dhuluma, kwa
kuimarisha TAKUKURU ili kukabiliana na tatizo hilo.
“Ni jukumu na wajibu wa Serikali
kutoa Ulinzi, Usalama na Huduma Bora kwa jamii, lakini ufanisi wa
kutekeleza wajibu huu utawezekana endapo watumishi wote wa Serikali
watawajibika ipasavyo katika utendaji kazi” aliongeza Samia.
Mkurugezi Mkuu wa Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Valentino Mlowola anasema
maadhimisho hayo yamelenga katika kuimarisha nidhamu kwa watumishi wa
umma kwa kuzingatia kasi ya maendeleo ya Taifa.
Aidha, Mlowola aliwataka viongozi
wa dini kutumia fursa waliyonayo kuhubiri maadili kwa waumini wao ili
kuweza kuwa na kizazi chenye kuzingatia maadili katika Taifa.
“Kila mmoja anatakiwa kuwajibika
kwa namna moja ama nyingine, wazazi, walezi, walimu wanapaswa kuwalea
watoto ipasavyo ili kuweza kuwa na Taifa linalozingatia maadili” alisema
Mlowola.
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora, Bahame Nyanduga alisema maadhimisho hayo
yalilenga utetezi na ulinzi wa haki za binadamu, uwajibikaji, utawala
bora na mapambano dhidi ya rushwa, wizi, ufisadi na ubadhilifu wa mali
za umma.
“Taasisi za uwajibikaji zinatoa
huduma ya kuelimisha wananchi, kutoa ushauri na kupokea malalamiko ya
wananchi kuhusu uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya
utawala bora” alisema Nyanduga.
Aidha Nyanduga alisema kumekuwa
na baadhi ya changamoto zilizoikumba taasisi hizo ikiwemo ufinyu wa
bajeti katika kuwezesha huduma za taasisi hiyo zinawafikia wananchi.
Mwakilishi wa Umoja wa Kimataifa,
Alvaro Rodrigez aliwataka wananchi kwa ujumla kushirikiana katika
kuimarisha haki za binadamu na kuipongeza Serikali ya Tanzania kwa
kuanzisha kampeni ya kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto na
albino.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
Utumishi na Utawala Bora, Angellah Kairuki aliahidi kuendeleza uhusiano
na ushirikiano uliopo baina ya Taasisi zinazohusiana na masuala ya
maadili na haki za binadamu ili kuweza kukuza maadili nchini.
“Serikali itaendeleza mapambano
dhidi ya Rushwa, kudhibiti manunuzi ya umma na kusimamia maadili
sambamba na haki za binadamu” alisema Waziri Kairuki.
No comments :
Post a Comment